WAPIGA DEBE WAGOMBEA ...

Na Dustan Shekidele, Morogoro
NI jambo la kusikitisha kweli.
Kijana mmoja aliyefahamika kwa jina la Komba Faustine Aloyce ambaye ni mpiga debe, amefariki dunia baada ya kugongwa na gari wakati akipigana na mwenzake katikati ya barabara wakigombea shilingi elfu moja waliyopewa kama ujira katika kituo cha daladala kilichopo Kasanga nje kidogo ya Manispaa ya Morogoro.

Tukio hilo la kusikitisha lilitokea Jumamosi iliyopita kwenye kituo hicho cha daladala zitokazo Mzumbe, Mlali, Mgeta Melela, Doman na Morogoro mjini kilichopo kando kando ya Barabara Kuu ya Morogoro-lringa.
Mashuhuda wa tukio hilo walililiambia gazeti hili kwamba Komba na mwenzake huyo aliyefahamika kwa jina moja la Alunaki, waligombea fedha hiyo waliyopewa baada ya kufanya kupiga debe ambapo kila mmoja alidai ilikuwa yake.
Wakati wakiendelea kupigana, gari moja lilitokea kwa kasi, Alunaki aliwahi kukimbia lakini bahati mbaya Komba akakanyagwa na kufariki papo hapo. Kabla ya kupigana, inadaiwa wawili hao walizozana kwa muda mrefu.
Dada wa marehemu, Mary Osward alisema mdogo wake huyo alifika na kuishi nyumbani kwake tokea mwaka jana akitokea Kilosa na kwamba kupiga debe ndiyo ilikuwa kazi yake.
“Mdogo wangu alikunywa chai kisha akaniaga anaelekea kazini kwake, lakini baada ya muda nikaona watu wanakimbilia barabarani nilipowauliza kuna nini wakaniambia mdogo wangu amegongwa na gari, nilipofika nikamkuta ndiyo anakata roho,” alisema kwa masikitiko dada huyo.

Comments

Popular posts from this blog