RAIS KIKWETE KUHUTUBIA BUNGE LEO
- Get link
- X
- Other Apps
Rais Jakaya Kikwete, leoo anatarajiwa kulihutubia Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Habari
zilizopatikana Mjini Dodoma jana na kuthibitishwa na uongozi wa Bunge
pamoja na Ikulu, Dar es Salaam zinasema atahutubia mchana.
Kutokana
na ujio huo, Serikali imewaelekeza Mawaziri na Manaibu Waziri kutotoka
nje ya Dodoma hadi hapo Rais atakapokuwa amehutubia Bunge. Kadhalika
safari zote za Kamati za Bunge ambazo zilikuwa katika mchakato wa
kutekelezwa zimeahirishwa hadi baada ya leo, ili kutoa fursa kwa wabunge
wote kuwapo wakati wa hotuba hiyo.
Katibu Mkuu
Kiongozi, Balozi Ombeni Sefue alisema jana kuwa hata yeye amesikia
taarifa kuwa Rais atazungumza bungeni lakini hajui atazungumza kitu
gani... "Hata mimi nimesikia kuwa atazungumza lakini sijui atazungumza
jambo gani kwa kuwa siyo miongoni mwa watu wanaomwandalia hotuba,"
alisema Balozi Sefue.
Kadhalika,
Mkurugenzi wa Mawasiliano Ikulu, Salva Rweyemamu alithibitisha kuwa
Rais Kikwete atalihutubia Bunge, Alhamisi... "Nathibitisha ni kweli, ila
kwa taarifa nyingine watafuteni watendaji wa Bunge, kama Katibu wa
Bunge nadhani wana taarifa zaidi."
Katibu wa
Bunge, Dk Thomas Kashililah alithibitisha jana katika Viwanja vya Bunge
Dodoma kuwapo kwa ratiba ya Rais Kikwete kulihutubia Bunge na kwamba
taarifa rasmi ingetolewa jana jioni kwa wabunge.
"Ni kweli Rais anatarajiwa kuja kulihutubia Bunge na leo (jana) jioni, tutatoa taarifa rasmi bungeni," alisema Dk Kashililah.
Mara ya
mwisho Rais Kikwete alilihutubia Bunge wakati akifungua rasmi Bunge la
Kumi, Novemba 18, 2010 alipoeleza vipaumbele vya Serikali yake katika
awamu ya pili ya uongozi wake. Rais Kikwete analihutubia Bunge wakati
likisubiri kujadili mapendekezo ya marekebisho katika Sheria ya
Marekebisho ya Sheria ya Mabadiliko ya Katiba ya 2013 ambayo ilipitishwa
katika mkutano uliopita.
Tayari
Muswada wa Marekebisho unaopendekezwa umewasilishwa katika Ofisi ya
Katibu wa Bunge chini ya hati ya dharura na leo utajadiliwa katika Kikao
cha Kamati ya Uongozi ili kupata kibali cha kuingizwa ndani ya Kamati
ya Katiba, Sheria na Utawala na baadaye Bungeni.
Dk
Kashililah alisema amepokea muswada huo na kwamba uamuzi wa lini
utafikishwa bungeni utafanywa na Kamati ya Uongozi ya Bunge ambayo
itakutana na jana.
Kamati
hiyo ndiyo yenye mamlaka ya kuifanyia marekebisho ratiba ya vikao vya
Bunge na kuruhusu mambo yanayopaswa kuingizwa bungeni kujadiliwa.
Muswada
huo ni matokeo ya majadiliano baina ya Serikali kwa upande mmoja na
vyama vya siasa vyenye wabunge chini ya uratibu wa Kituo cha Demokrasia
Tanzania (TCD) kwa upande mwingine, baada ya vyama vya siasa
kutoridhishwa na muswada ulipitishwa katika mkutano wa Bunge uliopita.
Itakumbukwa
kwamba wabunge wa vyama vya upinzani vya Chadema, NCCR Mageuzi na CUF
walisusia shughuli za mchakato wa kupitishwa kwa marekebisho ya sheria
hiyo bungeni, hivyo kutoa fursa kwa wabunge wa CCM kufanya watakavyo
kisha kupitisha sheria hiyo.
Baada ya
kupitishwa huko, vyama hivyo viliendesha kampeni ya kuitisha maandamano
nchi nzima, lakini kabla hayajafanyika Rais Kikwete aliwaalika viongozi
wake katika meza ya majadiliano, mchakato ambao umezaa mabadiliko
yanayokusudiwa kuingizwa bungeni wiki hii.
Katika
mazingira hayo kumekuwa na hofu kwamba huenda wabunge hasa wa CCM
wakatumia wingi wao kukwamisha mabadiliko yanayopendekezwa kutokana na
kukasirishwa kwao na kile kilichoonekana kuwa ni Rais Kikwete
kuwasikiliza wapinzani.
Hiyo
inaweza kuwa ndiyo sababu kubwa ya Rais Kikwete kuamua kulihutubia Bunge
kwa lengo la kujenga msingi wa maridhiano katika mchakato wa kuandikwa
kwa Katiba Mpya kama ambavyo amekuwa akisisitiza mara kwa mara.
WOTE MNAKARIBISHWA KUMSIKILIZA KUPITIA RUNINGA ZETU NA REDIO
- Get link
- X
- Other Apps
Comments
Post a Comment