NILIKUWA NAOMBA MUNGU KILA SIKU ILI AFUKUZWE CHADEMA’ - MAMA ZITTO
- Get link
- X
- Other Apps
Siku moja
baada ya Kamati Kuu ya Chadema kumvua uongozi aliyekuwa Naibu Katibu
Mkuu Taifa wa chama hicho, Zitto Kabwe, mama yake mzazi, Shida Salum
ametoa ya moyoni akieleza kuwa kilichomkuta mwanaye kimefunika mabaya
mengi yaliyopangwa afanyiwe.
"Kwa
upande wangu naona kama ni ushindi kwa Zitto kutokana na jinsi
ninavyojua hali ilivyo, mambo yalikuwa ni mengi mno na nikwambie tu,
Zitto kuvuliwa uongozi kumefunika hayo yaliyokuwa yamekusudiwa kufanywa
dhidi yake. Nilikuwa naomba Mungu kila siku ili afukuzwe Chadema,"
alisema mama huyo wakati akizungumza na gazeti hili nyumbani kwake
Tabata, Dar es Salaam.
Shida Salum
alisema kuwa Mungu amemnusuru mwanaye na kusisitiza, "Watu walikaa na
kutengeneza ripoti ya siri kuhusu Zitto na kuiweka kwenye mtandao kisha
kuituma kwa wanachama wa Chadema wanaowafahamu. Mpaka wanafikia hatua
hiyo maana yake ni kwamba wamejaribu njia zote za kummaliza, lakini
wameshindwa.
Alisema
kutokana na hali ilivyo hivi sasa amemnyang'anya mwanaye kwa muda simu
zake zote za mkononi, kompyuta mpakato (Laptop) pamoja na iPad ili
asiwasiliane na watu, kwa maelezo kuwa wapo wenye nia mbaya wanaomsaka
kumpa pole za kinafiki. "Kwa sasa nataka mwanangu atulize akili."
Shida
Salum, mbali na kuwa Mjumbe wa Kamati Kuu ya Chadema, pia ni mwasisi wa
Shirikisho la Vyama vya Watu Wenye Ulemavu (Shivyawata) na Mwenyekiti wa
Chama cha Watu Wenye Ulemavu wa Viungo (Chawata).
Zitto
pamoja na Mjumbe wa Kamati Kuu ya chama hicho, Dk Kitila Mkumbo juzi
walivuliwa uongozi kutokana na uamuzi wa kikao cha Kamati Kuu
kilichokutana kwa siku mbili, kuanzia Novemba 20 mwaka huu katika Ukumbi
wa Blue Pearl jijini Dar es Salaam, wakituhumiwa kukisaliti chama.
Mbali ya
kuwavua uongozi Zitto, Dk Mkumbo pamoja na aliyekuwa Mwenyekiti wa chama
hicho mkoani Arusha, Samson Mwigamba, pia Kamati Kuu imewapa siku 14
wajieleze kwa nini wasifukuzwe uanachama.
Kwa
uamuzi huo Zitto amebaki na wadhifa wa ubunge wake wa Jimbo la Kigoma
Kaskazini na Uenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC).
Katika
ufafanuzi wake wa jana, Shida aliwataka wanachama wa Chadema kuwa
watulivu kwa maelezo kuwa Zitto hajafukuzwa uanachama, "Siku nyingi
walikuwa wanamwinda na hata hilo jambo ambalo Chadema wanasema amefanya,
hawana uhakika nalo."
Juzi
wakati akisoma uamuzi wa Kamati Kuu, mwanasheria wa Chadema, Tundu Lissu
alisema wamebaini kuwapo kwa mkakati mkubwa wa watu hao kutimiza
malengo hayo ambao umeandikwa katika waraka unaoitwa 'Mkakati wa
Mabadiliko 2013', ambao umeandaliwa na kikundi kinachojiita 'Mtandao wa
Ushindi'.
Alisema
kikundi hicho vinara wake wapo wanne, Zitto anajulikana kama Mhusika
Mkuu (MM), Mkumbo (M1), Mwigamba (M3) na mtu mwingine wa nne ambaye
alieleza kuwa hajatambulika na anatumia jina la M2.
Atoa ya moyoni
Mama
Zitto ambaye wakati akizungumza na gazeti hili alikuwa amelala kutokana
na kusumbuliwa na maradhi alisema, "Kutolewa katika uongozi ni jambo la
kawaida. Zitto hajafukuzwa chama ila anaweza akafukuzwa maana kapewa
siku 14 tu za kujieleza."
Alisema
kauli iliyotolewa na Katibu Mkuu wa Chadema, Dk Willibroad Slaa, kwamba
chama hicho walimwondoa Aman Kabourou (aliwahi kuwa Mbunge wa Kigoma
Mjini-Chadema) itakuwa Zitto, inaonyesha jinsi watu walivyo na chuki na
mwanaye.
"Hayo ni
maneno ya chuki, maana hata Zitto naye ana watu wake ambao wanaweza
kutengeneza aina fulani ya chuki kwa viongozi wa chama na wanaweza
kupata wakati mgumu kufanya safari au mikutano yao mikoani," alisema.
Alisema
tangu siku nyingi ndani ya Chadema kulikuwa na mpango wa kumng'oa Zitto,
akifafanua kuwa hata katika kikao cha Kamati Kuu iliibuliwa hoja ya
ruzuku za vyama, huku wajumbe wakimshutumu Zitto kwamba kwa nafasi yake
na Naibu Katibu Mkuu alitakiwa kuitetea Chadema kuhusu ruzuku.
Katika
vikao vya Kamati ya PAC, Zitto aliingia katika malumbano na chama chake
baada ya kutuhumu vyama vya siasa kuwa hesabu zake hazikaguliwi na
Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), huku akitaka
ruzuku kwenye vyama hivyo isimamishwe.
"Zitto
alipoingia katika kikao cha Kamati Kuu alishikilia msimamo wake kwamba
kama Chadema inachukia ufisadi, nacho lazima kihakikishe kinakaguliwa,"
alisema na kuongeza;
"Wao
wanaona ili waweze kusalimika katika suala hili la ruzuku ni lazima
wamfukuze Zitto. Chadema hawako sawa, hesabu zao haziko sawa."
Alisema
kuwa tatizo lililopo ni kuwapo kwa mkakati wa watu fulani kuiyumbisha
Chadema , hivyo kila juhudi zinafanywa ili kukitingisha chama hicho
kipoteze mwelekeo.
"Siwezi
kusema wamemwonea au hawajamwonea, wao wametumia waraka wa Mwigamba
ambao Zitto amekiri katika Kamati Kuu kwamba hajawahi kuusikia wala
kuuona, tofauti na Dk Kitila ambaye amesema amewahi kuuona," alisema na
kuongeza;
"Zitto
anahusishwa na kitu ambacho Chadema hawana uhakika nacho, ukiusoma ule
waraka katika aya ya mwisho umeandikwa hivi, 'Huyu mtu tunayefikiria awe
mwenyekiti hajaoa,
tumshauri
aoe akikataa tutafute mtu mwingine', maana yake ni kwamba waraka huo
ulikuwa haujamfikia Zitto, kama ungekuwa umemfikia Zitto watu hao
wasingemwomba Zitto agombee uenyekiti." Alipoulizwa nafasi yake ndani ya
Chadema kutokana na yaliyomkuta mwanaye alisema, "Mimi hawawezi
kunitengenezea jambo. Hivi Zitto anaweza kuwa mbaya mimi nikawa mzuri."
Mama huyo
alieleza kuwa tangu alipovamiwa na majambazi nyumbani kwake, Aprili 19
mwaka huu hajawahi kuhudhuria kikao chochote cha Chadema. "Wale
wanaodhani Zitto kaonewa wanatakiwa kuwa wavumilivu na wapole, wasubiri
kwani kila kitu kinawezekana."
Ushauri kwa mwanaye
Alisema
kuwa mwanaye ana uamuzi wake na kwamba hata kama Chadema itamfukuza
uanachama, haitaweza kumnyang'anya vyeti vyake vya elimu aliyoipata.
"Zitto
anaweza kufanya kazi mahali popote duniani, lakini pia ni mwalimu
anaweza kuamua kufundisha. Ubunge ni mgawanyo wa madaraka. Watu wote
hatuwezi kuwa wabunge," alisisitiza.
Alisema
wakati Kikao cha Kamati Kuu kikifanyika Zitto alikuwa nje ya nchi na
kwamba yeye alimshauri kuhakikisha kuwa anahudhuria kikao hicho.
"Alipotua
tu na ndege aliniambia kuwa kuna foleni na alitaka kukodi pikipiki ili
awahi kikao, aliniambia lazima aende ili kujua hatima yake.
Aliacha
gari lake na kwenda na hata mimi nilimsisitizia kwamba ni lazima aende
katika kikao," alisema. Alisema kuwa Zitto alipofika katika kikao hicho
aliweza kuzima hoja zote zilizomhusu ikiwamo ya ruzuku za vyama, kwamba
baadhi ya wajumbe walipoona amebadili mwelekeo wa kikao, mjumbe mmoja
(akamtaja kwa jina) aliibua waraka uliomng'oa Zitto katika wadhifa wake.
"Unajua
Kamati Kuu ilijadili zaidi kuhusu ruzuku. Hata ule waraka uliongezwa
maneno baada ya baadhi ya wanachama kumpora Mwigamba laptop yake
alipokuwa mkoani Arusha katika kikao cha Chadema," alisema.
Huku
akiwataja wanachama wa Chadema walioongeza maneno katika waraka huo
(wakiwamo wabunge wawili) na viongozi wa ngazi za juu wa Chadema, mama
Zitto alisema kilichomkuta mwanaye ni ushindi mkubwa, kwamba alipangiwa
kufanyiwa makubwa zaidi ya yaliyomkuta.
"Hakuna
amani maana ukisikia kengele inagongwa hapa nyumbani unasema hao ndiyo
wamekuja kumuua Zitto nini, hivi sasa mpaka walinzi wanaolinda hapa
wakisikia unakuja nyumbani kwa Zitto lazima wakuandike jina na
kukufuatilia," alisema mama huyo.
Dk Kitila alonga
Akizungumza
na gazeti hili jana, Dk Mkumbo alisema kutokana na ushauri wa watu
mbalimbali, yeye na Zitto wamepanga kukutana na waandishi wa habari na
kutoa tamko.
"Tumepanga mimi na Zitto tutatoa ufafanuzi kuhusu jambo hili, nadhani ni kesho (leo), tutawajulisha lakini," alisema.
Baada ya
chama hicho kutangaza kuwaengua katika uongozi Zitto na Dk Kitila, saa
mbili baadaye Makamu Mwenyekiti Taifa wa Chadema, Said Arfi aliandika
barua ya kujiuzulu.
NINI MTAZAMO WAKO?
- Get link
- X
- Other Apps
Comments
Post a Comment