Neno Fupi La Leo: Tumekuwa Manabii Wa 'Siku Za Mwisho Za Upinzani..'

1471342_10201800111417251_351940333_n_7cd81.jpg
" Kipofu akinivamia na kuniumiza, nikakasirika kwa sababu ya maumivu aliyonitia, ni jambo la kibinadamu. Lakini, nikijitoboa macho ili na mimi nimvamie na kumwumiza haitakuwa nimefanya jambo la busara". - Julius Nyerere.
Ndugu zangu,
Kuna mawili yamenisikitisha ; maandiko ya ndugu yangu Julius Mtatiro na katuni ya ndugu yangu Marco Tibasima.

Julius Mtatiro anaandika kwa masikitiko; " Na migogoro yote huwa inafurahiwa na vyama dola".
Julius amezungumzia juu ya migogoro katika vyama vya upinzani inavyoumiza vyama na demokrasia. Namfahamu Julius, nimekaa na kuongea nae mara kadhaa. Ni kijana anayeifikiria zaidi Nchi aliyozaliwa. Najua kuwa yanayotokea yanamwumiza sana.
Na katuni ya Marco inajieleza. Inahuzunisha pia.  
Na jioni hii kwenye redio ya Ujerumani mtangazaji ameniuliza juu ya hatma ya upinzani kuelekea 2015. Jibu langu; ni mapema mno kuzungumzia ya 2015 kwa kuangalia kinachotokea leo katika Chadema.
Lakini, ni ukweli kuwa kuna wanaozungumzia hatma ya siasa za upinzani kuelekea 2015 kwa kuangalia yanayotokea leo ndani ya Chadema. Na hakika kumeibuka pia Manabii wa Siku za Mwisho za Upinzani...
Hata kama suioni uwezekano wa upinzani kukamata mamlaka ya dola ifikapo 2015, lakini, mimi ni muumini wa siasa za vyama vingi na uwepo wa upinzani. Siasa za upinzani zimekuwepo na zitaendelea kuwepo. Kwa nchi yeyote inayotaka kupiga hatua za maana za maendeleo, uwepo wa siasa za upinzani ni jambo la siha. Enzi za Chama Kimoja kimsingi ilikuwa na maana moja tu, ya kukandamiza fikra tofauti. Kwamba kufikiri tofauti ni sawa na uhaini.
Naamini, kuwa Vyama Vya Upinzani vinaweza kuzaliwa na kufa, lakini, fikra za upinzani kwa wanadamu zitadumu milele. Wanadamu hata kwenye familia ya kuzaliwa tumbo moja hutofautiana kimawazo. Kwamba wanaweza kupingana kifikra. Wote hatuwezi kufikiri sawa.
Naamini, kuwa bila uwepo wa vyama vya upinzani, Chama Cha Mapinduzi kinaweza kuwa chama chenye nguvu, lakini hakiwezi kuwa chama bora. Kitakuwa kimejijenga kwenye msingi wa matope. Kuna tofauti ya chama chenye nguvu na chama bora. Hilo la mwisho linahusu weledi na umakini wa wenye kushiriki uongozi wa chama. Ndio wenye kuchangia kukifanya chama kiwe bora.
Kwa chama makini, uwepo wa upinzani wa ndani na nje hupelekea kupata viongozi imara hata kiakili, lakini bila upinzani hupelekea chama kuwapata hata mazezeta kiakili kama viongozi wake.
 Na hakika, upinzani wa ndani na nje ya chama hepelekea kwenye ubora wa chama na ustawi wa nchi. Kama Wazalendo wa nchi hii, hatupaswi hata kidogo kushiriki kwa namna yeyote ile, kuchangia , kwa makusudi, na kwa maslahi binafsi, kwenye kudidimiza siasa za upinzani za ndani na nje ya vyama.
Miaka 20 iliyopita Mwalimu Julius Nyerere aliyasema haya; " Bila upinzani mzuri wa nje, na bila demokrasia halisi ndani ya Chama Cha Mapinduzi, Chama hiki kitazidi kudidimia chini ya uzito wa uongozi mbovu. Kwa hali yetu ya kisiasa ilivyo nchini hili si jambo la kutarajia bila hofu na wasi wasi1"- Julius Nyerere ( Uongozi Wetu Na Hatma Ya Tanzania, Uk. 67)
... Na tusiwe manabii wa ' Siku za Mwisho' za Upinzani...

Ni Neno Fupi La Leo.
Phars Msirikale. 

Dar. 
+255713-35 78 07

Comments

Popular posts from this blog