UDOM yashindwa kudahili wanafunzi wengi kutokana na wanafunzi hao kutokuwa na VIGEZO



CHUO Kikuu cha Dodoma (UDOM), kimeshindwa kudahili wanafunzi wa kutosha kutokana na wahitimu kutokuwa na vigezo. Malengo ya kuanzishwa kwa chuo hicho ni kudahili wanafunzi 40,000 ifikapo mwaka 2015 lakini hadi sasa idadi ya wanafunzi waliopo hawazidi 15,000.

Taarifa hiyo ilitolewa jana na Mwenyekiti wa Baraza la Wafanyakazi wa Chuo hicho, Profesa Idris Kikula wakati wa uzinduzi wa baraza la pili la wafanyakazi la chuo hicho.

Profesa Kikula alisema idadi ya wanafunzi wanaodahiliwa chuoni hapo inaendelea kushuka siku hadi siku ikilinganishwa na nafasi zilizopo.

"Changamoto zinazotukabili ni nyingi lakini za msingi ni idadi ya wanafunzi wanaodahiliwa imendeelea kushuka mwaka hadi mwaka kutokana na ukosefu wa wahitimu wa kutosha wenye vigezo vya kudahiliwa katika kozi zetu.

"Changamoto nyingine ni ufinyu wa bajeti unaotokana na vyanzo vichache vya mapato ya chuo na pia ufinyu wa ruzuku ya Serikali ndiyo vinakwamisha chuo kufikia malengo yake kama ilivyotarajiwa awali," alisema.

Alisema katika kukabiliana na changamoto ya kuongeza udahili, chuo kimeanzisha programu za cheti na stashahada kuanzia mwaka huu wa masomo.

Alisema kwa sasa Chuo hicho kina wanafunzi 13,376 wa shahada za awali, wanafunzi 1,403 wa shahada ya uzamili, wafanyakazi 1,181 na wataalamu 66 kutoka nje.

Comments

Popular posts from this blog