NYALLA, NYAULINGO, NYENZI WASHINDA RUFANI


Boniface-Wambura1 655d3
Kamati ya Rufani ya Uchaguzi ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) imewarejesha warufani wote watatu katika kinyang'anyiro cha uchaguzi wa Kamati mpya ya Utendaji ya TFF utakaofanyika Oktoba 27 mwaka huu jijini Dar es Salaam. (HM)


Samwel Nyalla, Ayubu Nyaulingo na Ayoub Nyenzi walikata rufani mbele ya Kamati hiyo inayoongozwa na Jaji wa Mahakama ya Rufani Tanzania, Bernard Luanda kupinga uamuzi wa Kamati ya Uchaguzi ya TFF kuwaondoa katika uchaguzi huo ambapo wote wanagombea ujumbe wa Kamati ya Utendaji kuwakilisha kanda mbalimbali.
Akisoma uamuzi wao leo (Oktoba 11 mwaka huu) mbele ya Waandishi wa Habari kwenye ofisi za TFF, Jaji Luanda amesema baada ya kusikiliza hoja za Mrufani Nyalla walipitia Kanuni za Uchaguzi za TFF na kugundua yafuatayo;
Ibara ya 10(3) imeweka masharti makuu mawili ya ujazaji wa fomu za kugombea uongozi. Fomu hiyo ni lazima iwe na saini ya mgombea na ni lazima ithibitishwe na viongozi wa shirikisho.
Kamati imepitia Kanuni za Uchaguzi haijaona sehemu fomu hiyo ya uongozi imeambatanishwa ili kuifanya kuwa Kanuni ya Uchaguzi. Ni maoni ya Kamati kuwa ni vizuri fomu za kugombea zikawa ni sehemu ya Kanuni za Uchaguzi.
Kwa vile Kanuni za Uchaguzi za TFF za 2013 pia hazijaainisha nini adhabu kwa mgombea aliyekosea kujaza Fomu namba 1 ya kugombea uongozi, Kamati inaona itakuwa si haki kumnyima mgombea nafasi ya kushiriki katika uchaguzi kwa vile tu fomu yake haijajazwa vipengele vyote.
Nyalla aliondolewa kwenye uchaguzi na Kamati ya Uchaguzi ya TFF kwa maelezo kuwa si mtu makini anayeweza kutekeleza majukumu yake kikamilifu baada ya kushindwa kujaza Fomu namba 1 kipengele cha 15 kinachohusu malengo ya mgombea uongozi.

Kwa upande wa Nyaulingo ambaye aliondolewa kwa kukosa uzoefu uliothibitika kulingana na Ibara ya 29(3) ya Katiba ya TFF na Kanuni ya 9(3) ya Kanuni za Uchaguzi za TFF, Kamati ya Rufani imeamua ifuatavyo;
Kamati ya Rufani ya Uchaguzi imepokea sababu za rufani na imepata fursa ya kusikiliza hoja na maelezo kutoka kwa Mrufani juu ya sababu zake alizozitoa kupinga uamuzi wa Kamati ya Uchaguzi.
Mrufani alifafanua historia yake katika masuala ya michezo kuanzia alipokuwa anasema Chuo Kikuu kuanzia 2005-2009 na pia ushiriki wake kama mchezaji wa Rukwa United iliyowahi kushiriki Ligi ya Mkoa wa Rukwa na ligi nyingine za kitaifa.
Kwa kusoma maana ya 'Familia ya TFF' iliyoko kwenye utangulizi wa Katiba ya TFF, pamoja na Ibara ya 29(3) na 29(6) ya Katiba hiyo, Kamati imejiridhisha kuwa Mrufani ana sifa za kugombea uongozi wa Shirikisho na amekidhi kigezo cha sifa za ugombea.
Ameshiriki kwenye mchezo wa mpira wa miguu kama mchezaji na mtawala, hivyo kutimiza kigezo kilichohitajika cha ushiriki katika uongozi na utawala wa mchezo wa mpira wa miguu kwa muda usiopungua miaka mitano.
Kwa kuzingatia hayo, Kamati ya Rufani ya Uchaguzi inaruhusu rufani ya Mrufani. Uamuzi wa Kamati ya Uchaguzi umetenguliwa na Mrufani anapewa nafasi ya kushiriki katika uchaguzi.
Kuhusu Ayubu Nyenzi aliyeondolewa kwa kukosa uzoefu kwa mujibu wa Ibara ya 29(3) ya Katiba ya TFF na Kanuni ya 9(3) ya Kanuni za Uchaguzi za TFF, na pia kushindwa kuthibitisha uraia wake mbele ya Kamati ya Uchaguzi, Kamati ya Rufani katika uamuzi wake imesema;
Imepokea sababu za rufani na imepata fursa ya kusikiliza hoja na maelezo kutoka kwa Mrufani juu ya sababu zake alizozitoa kupinga uamuzi wa Kamati ya Uchaguzi.
Baada ya uchambuzi wa kina, Kamati imeona kuwa kulingana na maelezo yaliyotolewa na Mrufani na viambatanisho vilivyowasilishwa, Kamati haina shaka kuhusu uraia wake. Uthibitisho wa uraia unapaswa kufanywa kwa umakini na taasisi yenye mamlaka ya kiserikali kufanya hivyo.
Kamati pia imejiridhisha kupitia Fomu namba 1 iliyojazwa na kusainiwa na Mrufani kuwa kuanzia mwaka 2004 mpaka 2010, Nyenzi ameshika nyadhifa za utawala wa mpira wa miguu na hasa katika klabu ya Yanga, uzoefu unaomfanya kuwa na sifa ya kugombea nafasi ya uongozi katika TFF kulingana na Ibara ya 29(3) ikisomwa pamoja na Ibara ya 29(6).
Kwa kuzingatia hayo, Kamati ya Rufani ya Uchaguzi inaruhusu rufani ya Mrufani. Uamuzi wa Kamati ya Uchaguzi umetenguliwa na Mrufani atashiriki katika uchaguzi wa TFF kwa nafasi anayogombea.

Wakati huo huo, Kamati ya Rufani ya Maadili ya TFF inakutana keshokutwa (Oktoba 13 mwaka huu), kufanyia mapitio (revision) ya uamuzi wa Kamati ya Maadili kwa waombaji uongozi wanane kama ilivyoombwa na Sekretarieti ili kutoa mwongozo wa utekelezaji wa uamuzi huo.
Chanzo: TFF



 

Comments

Popular posts from this blog