Waliopanda mbegu DECI hatarini kutolipwa
WATEJA wa
Kampuni ya DECI waliopanda mbegu, wanaweza wasilipwe fedha zao,
MTANZANIA Jumatatu limebaini. Wateja hao ambao wanaidai kampuni hiyo Sh
bilioni 39.27, huenda wasilipwe fedha zao kwa kuwa mchezo wa upatu
hautambuliki kisheria. Utata huo ulijulikana mwishoni mwa wiki, baada ya
Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT), Profesa Benno Ndullu, kuzungumza
na MTANZANIA Jumatatu.
"Kwanza
kabisa, niseme tu kwamba hadi sasa hatujapata nakala ya hukumu hiyo ili
kujua inatuelekeza nini kuhusu mchakato wa kuwalipa hao waliopanda
mbegu.
"Tukipata
hukumu hiyo, ndiyo tutaisoma na kufahamu tumepewa jukumu gani na
gharama zitalipwa na nani katika kutekeleza mchakato huo.
"Sisi
tunataka tujue hiyo hukumu inamaanisha nini, maana kwa kawaida
anayechezesha na anayecheza upatu wote wana makosa, sasa utamlipaje
aliyecheza?
"Lakini,
kwa kuwa hatujaiona hiyo hukumu, hatujui imetuelekeza nini, lakini
itakuwa ajabu kidogo kwa sababu kwa uzoefu wa nchi nyingine, waliocheza
mchezo huo na waliokuwa wakiuchezesha, wote wanastahili hukumu.
"Lakini
tutakachokifanya sisi, tutakaa na DPP (Mkurugenzi wa Mashtaka), ili
tuweze kupata tafsiri ya sheria maana huwezi kurudi na kumzawadia fedha
mcheza upatu na kumhukumu mchezeshaji," alisema Gavana Ndulu.
Akifafanua
uzoefu wa nchi nyingine ambazo kesi za aina hii zimewahi kutokea,
alisema fedha na mali zote za waendeshaji na wacheza upatu, huwa
zinataifishwa na Serikali.
"Kesi ya
DECI haikuwa ya madai bali ilikuwa ni ya jinai, na hapa nchini haijawahi
kutokea kesi kama hiyo labda ndiyo maana imeleta utata. Lakini ukweli
ni kwamba, suluhisho lake litapatikana baada ya kuketi na DPP na
kushauriana," alisema.
Wakati
Gavana Ndulu akisema hayo, wanasheria waliozungumza na MTANZANIA
Jumatatu, walisema mchezo wa upatu unasimamiwa na sheria zinazosimamia
upatu na kamari.
Kwa
mujibu wa wanasheria hao ambao hawakutaka kutaja majina yao gazetini,
sheria za upatu ziko katika michezo ya bahati nasibu na kamari ambazo
zinachezeshwa kisheria kwenye Casino.
Agosti 19
mwaka huu, Hakimu Mkazi wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Aloyce
Katemana, aliiagiza Serikali kufanya mchanganuo wa mali za DECI ambazo
inazishikilia kisha wateja wa taasisi hiyo walipwe.
Kesi ya
DECI namba 109 ya mwaka 2009, ilifunguliwa Juni 12, mwaka 2009 katika
Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, baada ya kugundulika kuwa, kampuni hiyo
ilikuwa ikiendesha mchezo huo kinyume cha sheria.
Washtakiwa
katika kesi hiyo walikuwa ni Jackson Mtares, Dominick Kigendi, Timotheo
Ole Loitginye, Samwel Mtares na Arbogast Kipilimba, ambao walikuwa
wanatetewa na mawakili wa kujitegemea, Hudson Ndusyepo na Onesmo Kyauke.
Washtakiwa
hao walikuwa wanakabiliwa na mashtaka mawili, ambayo ni kuendesha na
kusimamia mradi wa upatu kinyume na kifungu cha 111A (1, 3) cha Sheria
ya Kanuni ya Adhabu Sura ya 16.
Wakati wa
shitaka hilo, ilidaiwa kuwa, kati ya mwaka 2007 na Machi 2009, katika
makao makuu ya DECI, Mabibo Mwisho, jijini Dar es Salaam, washtakiwa
waliendesha na kusimamia mradi wa upatu katika sehemu tofauti nchini,
kwa ahadi ya kuwapa wanachama wao fedha zaidi ambazo katika mazingira ya
kibiashara ni kubwa kuliko mradi waliokuwa wakiufanya.
Shitaka
la pili ni kupokea amana za umma bila kuwa na leseni, kinyume cha
kifungu cha 6 (1, 2) cha Sheria ya mabenki na Taasisi za Fedha namba
tano ya mwaka 2006 na kwamba, washtakiwa wote katika kipindi hicho
wakiwa kwenye ofisi zao za DECI, walipokea amana kutoka kwa umma bila
leseni.
DECI ilikuwa na matawi 40 katika mikoa 18 ya Tanzania Bara.
CHANZO MTANZANIA.
CHANZO MTANZANIA.
Comments
Post a Comment