POLISI TANZANIA KUPATA MAFUNZO YA UPELELEZI NCHINI UTURUKI


Mademu jumla
Na Tamimu Adam, Jeshi la Polisi
Jeshi la Polisi la Uturuki limetoa ufadhili wa masomo kwa  askari kumi na saba ( 17) wa Jeshi la Polisi Tanzania kupata mafunzo mbalimbali yakiwemo ya upelelezi wa wahalifu na mbinu za uchunguzi wa kimaabara pamoja na usimamizi na uendeshaji wa gari la matukio yatakayochukua muda wa mwezi mmoja nchini Uturuki.
Mkurugenzi wa Upelelezi wa makosa ya jinai nchini (DCI) Kamishina Robart Manumba aliyasema hayo jana wakati wa kikao cha kazi kilichofanyika Makao Makuu ya Polisi.
Alisema kuwa mafunzo hayo ni sehemu ya maboresho yanayolenga kuwaongezea askari weledi na kuwajengea uwezo wataalamu wa Maabara ya uchunguzi ya Polisi juu ya mbinu mbalimbali za kiuchunguzi na  upelelezi pamoja na matumizi sahihi ya vifaa  vya kiupelelezi.
Aliongeza kuwa mafunzo hayo yatasaidia wataalamu wa Maabara ya uchunguzi ya Polisi kuweza kufanikisha kuwakamata wahalifu na kutambua   uhalifu uliotendeka kwa haraka,  hivyo, kupunguza uhalifu nchini.
Kwa upande wake Mkuu wa Maabara ya uchunguzi ya Jeshi la Polisi Naibu Kamishina wa Polisi, (DCP) Abdularahaman Kaniki alisema kuwa mafunzo hayo ni muendelezo wa ushirikiano uliopo baina ya Jeshi la Polisi Tanzania na Jeshi la Polisi la Uturuki ambao ulianza katika mafunzo ya upelelezi na ukusanyaji wa vielelezo katika eneo la tukio uliofanyika hapa nchini mwishoni mwa mwezi juni mwaka huu.
Aidha, aliwataka askari waliochaguliwa kushiriki mafunzo hayo kutumia fursa hiyo kujifunza kwa bidii ili kuongeza ufanisi pamoja na kuboresha utendaji  katika  maeneo mbalimbali ya upelelezi na Maabara ya  uchunguzi ya Polisi ili kufanikisha utambuzi wa uhalifu na wahalifu kwa haraka.

Comments

Popular posts from this blog