PICHA YA MWANAMKE. ALIYEKATWA MKONO NA MPENZIWE KISA MAPENZI



Baada ya kuwa katika mapenzi na mwanaume huyo kwa zaidi ya miaka 17, wakipendana na kuitana majina yote mazuri unayoyajua yakiwamo kuambiwa ‘mpenzi wangu nakupenda, nikinywa maji nakuona kwenye glasi’…leo mapenzi yamegeuka shubiri.Kuna mikasa mbalimbali huwatokea watu katika suala zima la mapenzi, kiasi cha kusababisha baadhi yao kutopenda tena kuingia kwenye jambo hilo wakiliona kama ni kitu kisichofaa, ingawa ukweli unaweza kuwa sio huo.“Sitaki tena wanaume, ni watu wabaya, wameniumiza moyo wangu mno,” anasema Hawa Francis, mkazi wa Ubungo, Dar es Salaam. Sababu kubwa ni kero ambazo amewahi kuzipata katika suala zima la uhusiano. Vivyo hivyo wapo wanaume hawataki kuoa, kwa maelezo kuwa kuna wanawake wamewahi kuwatesa.
Kama wewe ni kati ya watu ambao umekata tamaa na suala la uhusiano, fahamu kuwa si wewe pekee.Kuna kundi kubwa la watu wameshatendewa kiasi cha kufanya wasiwe na raha tena.

Mkasa wa mwanamke kukatwa mkono

Ilikuwa Agosti 7, mwaka huu, saa mbili usiku. Ilikuwa ni siku iliyobadili historia ya maisha yake. Baada ya kuwa katika mapenzi na mwanaume huyo kwa zaidi ya miaka 17, wakipendana na kuitana majina yote mazuri unayoyajua yakiwamo kuambiwa ‘mpenzi wangu nakupenda, nikinywa maji nakuona kwenye glasi’…leo mapenzi yamegeuka shubiri.

Mwanamke huyo, Mchali Kihiyo (35), mama wa watoto sita, aliyepoteza viungo vyake kutokana na ukatili wa kijinsia uliofanywa na mwanaume ambaye wamekuwa na uhusiano nae (jina limehifadhiwa).

“Uhusiano wetu ulikuwa mzuri, hata hivyo kwa sasa naona mambo yamekuwa magumu kwangu, leo hii mimi sina mkono wa kushoto na nimeondolewa sehemu ya viungo vyangu vya upande mmoja,”anasema Mchali,akibubujikwa machozi kutokana na ulemavu alioupata.

Chanzo cha ulemavu

Anasema maisha yao ya uhusiano yalikuwa ya furaha kwa kipindi chote lakini yamegeuka shubiri baada ya mwanamume wake huyo kuonyesha dalili ya kutompenda kama awali, hali ambayo anaitafsiri kama labda alikuwa na mwanamke mwingine.

Mchali, anasema mikasa na mateso ilianza miaka mitatu iliyopita baada ya kuhisi kwamba mwanamume wake huyo amezaa na mwanamke mwingine. Ubaya zaidi ulimtokea baada ya mtoto wa huyo mwanamke mwingine, kutumbukia kwenye kisima cha maji na kisha kupoteza maisha.

 “Kifo cha mtoto huyo, ndicho kilichozaa tatizo hili la ukatili dhidi yangu na kunisababishia ulemavu, kwa kuwa huyo mwanaume wangu na huyo mwanamke aliyezaa nae, walidai kwamba mimi ndiyo nilimtupia majini marehemu mtoto wao ili afe,”anasema mama huyo.

 Vitisho kabla ya ulemavu

Mchali, anasema mara baada ya msiba wa mtoto kumalizika, mwanamume wake huyo alihamia kwa mke mdogo lakini akawa anarejea nyumbani na kumtukana huku akitishia kufanya lolote analofikiri linafaa.

Anasema baada ya mateso na vitisho kuzidi aliamua kuondoka kwa mumewe huyo toka mwezi Aprili mwaka huu na kuamua kurudi kwa wazazi wake huku akiwaacha watoto wake kwenye nyumba waliyokuwa wakiishi.

Anasema alilazimika kuwaacha watoto kutokana na agizo la mumewe, aliyekataa asiwachukue, hivyo akaanza maisha mengine ya upweke bila watoto huku akiendesha maisha yake kwa biashara ya kuuza samaki.

Anasema mwanzoni mwa mwezi huu, aliugua malaria na kukaa nyumbani bila kwenda kwenye biashara zake. Agosti saba mwaka huu, alipata nafuu na kuamua  kwenda kumsalimia kaka yake, anayeishi mbali kidogo na nyumbani kwao na ndipo yakamkuta yaliyomkuta.

Anaeleza kuwa alikaa kwa kaka yake hadi muda wa futari wakafuturu na kushangaa simu yake ikiita, kuangalia ni namba ya mpenzi wake huyo. Alipoipokea, aliulizwa aliko, yeye alimweleza yuko kwa kaka yake na kumtaka amfuate mnadani akale nyama kitendo ambacho anasema alipingana nacho.

Anasema baadaye aliamua  kurudi nyumbani na kusindikizwa na wifi yake hadi karibu na nyumba yao ikiwa ni saa mbili usiku.Walipoagana, ghafla akashangaa kusikia sauti ya mumewe ikimuita, alipogeuka alimwona, kisha akamuuliza  alikotoka na kumwambia alikuwa kwa kaka yake.

Kipigo na ulemavu

Anasema mara baada ya kumjibu mwanamume huyo alianza kumpiga na hatimaye alianguka chini na mumewe akatoa panga na kuanza kumkatakata sehemu mbalimbali za mwili wake.

Hakika hujafa hujaumbika. Mchali amecharangwa kwa mapanga kuanzia chini ya goti mguu wa kushoto hadi kwenye makalio, amekatwa sehemu zaidi ya saba mwilini.

Ni kama alitaka kumkata shingo

Anasema kwa namna anavyoona ni kama alidhamiria kumuua akisema kuwa mara nyingi akiwa na huo upanga alikuwa analenga kumtenganisha shingo. Alichofanya mama huyo ni kuweka mikono shingoni kuzuia panga, kitendo kilichosababisha  mkono wake wa kushoto kukatwa kabisa.

Hawezi kukaa

Mwandishi wa makala haya baadaye alimwomba mwanamke huyo angalau akae chini, kwani muda mwingi wa mahojiano alikuwa amelala, ndipo alipojibiwa kwamba hawezi kukaa kwa vile kuna nyama kubwa kwenye makalio ambayo imeshindikana kushonwa.

Mama huyo anasema wakati mumewe akimcharanga mapanga, mama yake mzazi aliendelea kupiga ngolo (yowe) kuomba msaada, kaka yake alikwenda lakini akashindwa kutoa msaada kwa kuwa shemeji yake huyo alikuwa akimkimbiza na panga.

Anasema kelele za mama yake zilisaidia kuokoa maisha yake, kwa kuwa majirani walijitokeza, hivyo mwanamume huyo akaanza kuwakimbiza akitaka kuwadhuru kitendo ambacho mama huyo aliona ndiyo nafasi pekee kukimbilia ndani.

Matibabu

Mchali, anasema baadaye ndugu zake, walitafuta usafiri na kufanikiwa kupata matibabu katika Hospitali ya Rufaa ya KCMC ambako alilazwa kwa siku nne na kurejea nyumbani kutokana na ushauri wa daktari anayemhudumia.

Kwa mujibu wa mama huyo, daktari anayemtibu alimtaka Mchali akubali kutibiwa majeraha akiwa nyumbani ili kuepuka maambukizi ya magonjwa nyemelezi pamoja na kuepuka gharama za matibabu.

“Sina uwezo wa kukabiliana na gharama za matibabu kwa kuwa siwezi kutembea, nalazimika kukodi gari na kwa wiki naoshwa mara tatu. Nisaidieni ndugu zangu, ndoa yangu imenifikisha hapa,” anasema.

Mchali na hali ya ukatili mkoani Manyara

Kamanda wa Polisi mkoa wa Manyara, Akili Mpwapwa anasema mtuhumiwa bado hajakamatwa kwa vile hajulikani aliko, huku akiahidi kuendelea kulifanyia kazi suala hilo.

Akielezea zaidi ukatili mkoani Manyara, anasema upo, japo ni mdogo ikilinganishwa na mikoa mingine. Anaamini kuwa bado changamoto ni kubwa  kwa wanawake ambao wengi wao wamekuwa wakinyanyasika.

Sababu kubwa za kunyanyasika kwa wanawake ni mfumodume. Akasisitiza kuwa Jeshi la Polisi mkoani humo linaendelea kuelimisha jamii madhara ya ukatili na kusema jitihada hizo zinapaswa kuigwa na wananchi na asasi nyingine kuhakikisha ukatili wa kijinsia unatokomezwa.

Comments

Popular posts from this blog