Pacha aliyeungana sasa atolewa ICU

pacha1 2e1b7
Mtoto Kudra aliyekuwa ameunganika na kiwiliwili cha pacha mwenza, anaendelea vizuri na matibabu katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili (MNH).
Mtoto huyo alifanyiwa upasuaji Alhamisi iliyopita katika Taasisi ya Mifupa ya Muhimbili (Moi) na kulazwa katika wodi ya wagonjwa wanaohitaji uangalizi maalumu (ICU), lakini mwishoni mwa wiki iliyopita alitolewa katika wodi hiyo.
Mama mzazi wa mtoto huyo, Pili Hija, alisema hivi sasa Kudra ananyonya vizuri na kwamba amekuwa akitaka kufanya hivyo kila wakati .
"Kwa kweli kudra za Mwenyezi Mungu ndizo zimemweka hai mpaka leo hii, nilikuwa nimeshakata tamaa kuwa nampoteza mwanangu, nazidi kumuomba Mungu amwekee mkono wake apone kabisa," alisema Hija.
Daktari Bingwa wa Upasuaji wa Watoto katika Hospitali ya Muhimbili, Dk Zaitun Bokhary, alisema mtoto huyo anaendelea vizuri na mwishoni mwa mwezi huu atafanyiwa upasuaji mwingine.
"Tunamwacha achangamke kwanza, mwishoni mwa mwezi huu tutamfanyia upasuaji mwingine wa kumwekea njia ya muda ya kutolewa haja kubwa, kwa kumpasua ubavuni baada ya hapo ataruhusiwa kwenda nyumbani," alisema Dk Bokhary.
Kudra alipewa jina hilo Alhamisi usiku, saa kadhaa baada ya upasuaji kufanyika chini ya jopo la madaktari saba, walioongozwa na Dk Hamis Shaaban, mtaalamu wa Ubongo na Uti wa Mgongo kutoka Moi.
Alizaliwa Agosti 18, baada ya mwanamke huyo kujifungulia nyumbani watoto pacha, huku mmoja akiwa hajakamilika viungo vyote. Pia, kiwiliwili kilichoungana hakikuwa na kichwa, macho, maini, figo ila alikuwa na mshipa mmoja wa fahamu ambao ulikuwa umeshikana na mwenzake na kulazimisha madaktari hao kumfanyia upasuaji.
CHANZO:MWANANCHI

Comments

Popular posts from this blog