NELSON MANDELA ARUHUSIWA KUTOKA HOSPITALI


RAIS wa zamani wa Afrika Kusini, Nelson Mandela (95), jana aliondolewa hospitali na kurejeshwa nyumbani ambako ataendelea na matibabu ya maradhi ya mapafu. 


Hata hivyo, taarifa ya Serikali ya Afrika Kusini imesema uamuzi huo hauna maana kwamba Mandela amepata nafuu kwa vile hali yake bado ni mbaya na wakati mwingine hudorora zaidi.

Taarifa hiyo imeongeza timu ya madaktari wa Mandela inaamini ataendelea kupata matibabu katika makazi yake mjini Houghton kwa kiwango sawa na anayopata akiwa hospitalini mjini Pretoria.

Tangazo hilo limekuja siku moja tu baada ya maofisa wa serikali kukanusha ripoti kuwa shujaa huyo wa taifa hilo, alisharuhusiwa.

Mshindi huyo wa tuzo ya amani ya Nobel aliyekuwa amelazwa hospitali tangu Juni 8, mwaka huu anaheshimiwa duniani kwa kuongoza mapambano dhidi ya utawala wa kibaguzi wa wazungu wachache na kuhubiri upatanisho na maridhiano na jamii za weupe pamoja na kufungwa miaka 27 jela.

“Timu ya madaktari imetuhakikishia kuwa Mandela atapokea matibabu kwa sawa na anachopata hospitalini mjini Pretoria atakapokuwa katika makazi yake ya Houghton,” taarifa ya Ofisi ya Rais ilisema.

“Lakini ikibidi, atarejeshwa hospitali,” taarifa hiyo ilisema na kuongeza kwamba inamtakia Mandela afya njema.

Nyumba ya Mandela imerekebishwa kwa ajili ya kumruhusu kupata matibabu ya mgonjwa mahututi akiwa hapo.

Wachambuzi wa mambo wanasema kuruhusiwa kwa Mandela hakumaanishi mtu aliyepata nafuu bali kumhamisha kutoka wodi ya hospitali kwenda wodi iliyotengenezwa maalumu ya nyumbani kwa matakwa ya familia yake.

Hata hivyo, wanasema inachotia moyo ni kwamba madaktari wake wamesema Mandela yuko imara kuweza kuhimili safari ya kilomita 55 kutoka hospitalini kwenda nyumbani kwake.

Comments

Popular posts from this blog