MCHUNGAJI ATOA SIRI ALIVYOJIHUSISHA NA MADAWA YA KULEVYA
- Get link
- X
- Other Apps
Mchungaji
Donald Mwakisambwe wa kanisa la Kipendekoste la Kiinjili Tanzania,
kwenye ofisi za gazeti hili wakati akitoa ushuhuda wa kufanya biashara
haramu ya madawa ya kulevya.
Kinara
wa kimataifa wa kuuza madawa ya kulevya aliyezunguka sehemu mbalimbali
duniani kuuza mihadarati, ameacha biashara hiyo na sasa anahubiri Injili
kupiga vita dawa hizo. Kigogo huyo Mtanzania na mzaliwa wa Mbeya,
ambaye sasa anajiita kiumbe kipya katika Kristo, ni Mchungaji Macdonald
Mwakisambwe wa Kanisa la Kipentekoste la Kiinjili jijini Dar es Salaam.
Akizungumza katika mahojiano maalumu Jumamosi jana, Mwakisambwe alisema
alianza biashara ya unga mwaka 1990 na kuifanya kwa miaka 10,
akisafirisha dawa kwa maelfu ya wateja walioko Afrika, Asia, Ulaya na
Amerika. Alisema katika kutimiza azma hiyo, alitumia pasi za kusafiria
za mataifa mbalimbali zenye majina tofauti, zikimuonyesha kuwa ni raia
wa Msumbiji, Tanzania, Kenya, Namibia, Afrika Kusini na Namibia.
Alieleza kuwa, kumiliki pasi hizo kulilenga kuficha wanausalama
wasimgundue kuwa ni ‘mzungu wa unga’ aliyekuwa anasafiri nchi mbalimbali
duniani ndiyo maana kila alipomaliza mzunguko aliziharibu pasi hizo .
Alisema mwaka 1999, Yesu Kristo, alimtokea akiwa rumande kwenye gereza
la Industrial Area jijini Nairobi, baada ya kuwasili Kenya akitokea
Karachi, Pakistani akiwa na karibu kilo moja ya kete za heroin tumboni.
Mwakisambwe alisema alipotua Nairobi, alikamatwa na maofisa wa polisi
kadhaa waliomueleza kuwa ni muuza unga wa kimataifa na kuwekwa chini ya
ulinzi kwenye kizuizi cha Uwanja wa Ndege wa Jomo Kenyatta. “Nilikuwa na
pasi ya Msumbiji yenye jina la Danilo Silva Jalla, licha ya kwamba ni
Mtanzania”,anasema.
Anaongeza kusema kuwa ili kupata pasi hizo, alibadilishwa sura halisi
kwa kujiwekea ndevu za bandia, nyusi na nywele nyingi zilizompa sura
tofauti na muonekano mpya kila alipouhitaji. Alisema pasi hizo zilikuwa
zikitengenezwa na magenge ya wanaojihusisha na madawa hayo ambao wapo
kila mahali na wamewekwa mahsusi kufanikisha usambazaji wa mihadarati
kila sehemu inapohitajika.
Alisema hata hapa Tanzania, kuna magenge hayo ya ‘mafia’ na mtandao huo
unashirikiana na maofisa wa Idara ya Uhamiaji wasio waaminifu. Mchungaji
Mwakisambwe alisema kupitia biashara hiyo, alijenga nyumba kadhaa
zilizoko Dar es Salaam na Mbeya pia alikuwa na utajiri mkubwa wa magari
ya kifahari na mengine ya kutanulia.
Alieleza kwa kirefu jinsi dawa hizo zinavyomezwa na kusafirishwa na
kukanusha madai kuwa yanaingizwa tumboni kupitia njia ya haja kubwa.
Alisema yanamezwa kama vidonge vingine baada ya kufungwa ndani ya vifuko
ya nailoni, kisha kuzungushiwa gundi ya karatasi ya nailoni, kuzongwa
na vipande vya glovu nyepesi ambazo hufungwa kikamilifu na kuchomwa kwa
moto kama pipi kifua ili kuvidhibiti visifunguke na dawa kuyeyuka
tumboni. “Kete zinazomezwa zina ukubwa wa kidole gumba cha mtu mzima na
hutofautiana kwa uzito, zipo zenye gramu 10 na ndogo zina gramu tano.
Ukiwa mzoefu unaweza kumeza hata 100 na kubeba pipi zenye uzito wa kilo moja. ”
Mchungaji huyo ambaye sasa anasema anachohitaji ni kuwaeleza watu kuwa
Mungu hapendi biashara ya madawa na kutangaza wokovu, na kusisitiza kuwa
aliyemuondoa kwenye biashara hiyo ni Yesu Kristo. *Mahojiano kamili
kuhusu jinsi Mwakisambwe alivyoanza kuuza mihadarati, nchi
alizotembelea, majina aliyotumia, familia yake, mtandao wa nje na ndani
alioshirikiana nao na jinsi alivyokutana na Yesu akamuokoa,
zitachapishwa kesho kwenye Safu ya NIPASHE Jumapili ya Anayemulikwa.
USILIKOSE.
SOURCE: NIPASHE
- Get link
- X
- Other Apps
Comments
Post a Comment