JACKSON KISWAGA AWAKUMBUKA WAJAWAZITO NYUMBANI KWAKE ATOA MSAADA WA VITANDA


kiswaga1_56765.png
Mkazi wa jimbo la Kalenga Bw Jackson Kiswaga kushoto akiwa na wafanyakazi wa Hospital teule ya wilaya ya Iringa -Ipamba
kiswaga_995e2.png
Diwani wa viti maalum tarafa ya Kalenga Bi Shakra Kiwanga kulia na wafanyakazi wa Hospital Teule ya Iringa wakipokea msaada wa vitanda viwili vyenye thamani ya Tsh milioni 3 kutoka kwa Bw Jackson Kiswaga ambae ni mkuu wa kitengo cha M- Pesa na ukuzaji wa biashara ,msaada ambao ameutoa yeye binafsi kama mkazi wa jimbo la Kalenga
kiswaga2_c8e0b.png
Mkuu wa kitengo cha M-Pesa na ukuzaji wa biashara Voda Com Bw Jackson Kiswaga akimfariji Bi Stella Kalinga ambae amelazwa wodi la wajawazito katika Hospital teule ya wilaya ya Iringa jana alipofika kutoa msaada binafsi wa vitanda viwili kwa ajili ya kuongeza idadi ya vitanda kwa wajawazito hospitalini hapo
MKAZI wa Kalenga wilaya ya Iringa mkoani hapa Bw Jackson Kiswaga ametoa msaada wa vitenda viwili vyenye thamani ya Tsh milioni 3.6 kwa Hospital teule ya wilaya ya Iringa Hospital ya Ipamba ili kunusuru wanawake wajawazito kujifungulia chini.
Kiswaga ambae pia ni mkuu wa M-Pesa na ukuzaji wa biashara alikabidhi msaada huo jana mbele ya uongozi wa Hospital hiyo na viongozi wa kata hiyo ya Kalenga .
Bw Kiswaga alisema kuwa amelazimika kutoa msaada huo wa vitanda katika Hospital hiyo kama njia ya kuhamasisha wakazi wengine wa wilaya ya Iringa ambao wapo nje ya mkoa wa Iringa kujenga utamaduni wa kuchangia shughuli za kimaendeleo katika wilaya hiyo ya Iringa na mkoa kwa ujumla badala ya kuendelea kuiachia serikali na wahisani kufanya kila jambo hata yale ambayo yapo chini ya uwezo wa wananchi wenyewe.
"Kuna baadhi ya shughuli za kimaendeleo hazipaswi kusubiri serikali wala kusubiri wafadhili kutoka nje ya Tanzania ...tujikipanga wenyewe wananchi tunaweza kufadhili shughuli hizo huku serikali na wahisani wakubwa tukiwasubiri kwa mambo makubwa ambayo sisi wananchi hatuwezi kuyafanya "alisema Kiswaga
Kuwa akiwa kama mkazi wa jimbo la Kalenga alipata kulazwa katika Hospital hiyo na moja kati ya changamoto kubwa alizokutana nazo hapo ni pamoja na suala la upungufu wa vitanda na changamoto nyingine nyingi hivyo kulazimika kwa upande wake kwa kushirikiana na marafiki zake waliopo jijini Dar es Salaam kuchangishana fedha za kununua vitanda hivyo vya kisasa ili kusaidia kupunguza uhaba wa vitanda .
Aidha alisema kuwa ataendelea kuangalia uwezekano wa kuisaidia zaidi Hospital hiyo ambayo ni mkombozi mkubwa kwa wakazi wa jimbo la Kalenga na wilaya ya Iringa kwa ujumla na kuahidi kusaidia kuingiza maji katika chumba cha kuhifadhia maiti katika Hospital hiyo ambayo ina chumba chenye uwezo wa kuhifadhi maiti sita pekee ila hakuna maji ya kusaidia kuosha maiti .
Hata hivyo alisema kuwa msaada huo umelenga kusaidia jamii ya wana Kalenga na mkoa wake wa Iringa na hauna malengo ya kisiasa na kuwa baadhi ya watu wamekuwa na dhana potofu kuwa mtu anapojitolea kusaidia shughuli za kimaendeleo nyumbani kwake kuwa anataka nafasi ya kisiasa na kuwa katika hili mbunge wa jimbo hilo la kalenga Dr Wiliam Mgimwa anatambua msaada huo .
Kwa upande diwani wa viti maalum Tarafa ya Kalenga Shakra Kiwanga akishukuru kwa niaba ya wakazi wa Kalenga alisema kuwa msaada huo ni chachu kwa wadau wengine kuendelea kufika katika Hospital hiyo na jimbo la Kalenga kuendelea kusaidia shughuli mbali mbali za kimaendeleo na kumpongeza Bw Kiswaga kuwa amekuwa mdau mkubwa wa maendeleo katika tafara ya kalenga .
" Sisi kama wana kalenga tunaendelea kukuombea afya njema na Mungu azidi kukuongezea pale unapopunguza kwani huu ni msaada wa kwanza kutoa kwetu ulipata kutusaidia ujenzi wa vyumba viwili vya madarasa katika shule ya Sekondari ya Lipuli ....na maeneno mengine mengi "alisema Bi kiwanga

Comments

Popular posts from this blog