WATU MILIONI 2.9 KUCHUKULIWA ALAMA ZA VIDOLE, PICHA.

231 1dec1
Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (NIDA) imeanza zoezi la uchukuaji alama za vidole, picha na saini za kielekroniki kwa waombaji wa Vitambulisho vya Taifa katika mkoa wa Dar es Salaam ambapo watu wapatao milioni 2,900,000 wanatarajiwa kupatiwa huduma hiyo.
Zoezi hili lilianza Julai 15 katika wilaya ya Temeke ambayo imegawanywa katika kanda tano, itafuatiwa na Wilaya ya Ilala na kuhitimishwa na Kinondoni.
Kila Wilaya imegawanywa katika kanda, ili kuhakikisha wananchi wanahudumiwa vizuri na kurahisisha zoezi kwa kuwapunguzia wananchi usumbufu wa kukaa muda mrefu kusubiri katika foleni.
Zoezi la uchukuaji alama za vidole linakwenda sambamba na ujazaji fomu kwa waombaji wapya ambao hawakupa fursa ya kujaza fomu wakati wa zoezi la ujazaji fomu za maombi ya vitambulisho vya Taifa.
Waombaji wanatakiwa kufika kwenye vituo vya usajili na nyaraka halisi za kuthibitisha uraia na umri mathalan, cheti cha kuzaliwa, pasipoti, vyeti vya elimu ya msingi na sekondari, leseni ya udereva, kitambulisho cha bima ya afya na kitambulisho cha mpigakura.
Zoezi la Utambuzi na Usajili wa watu lina hatua mbalimbali ambazo zinatakiwa kufuatwa kwa lengo la kuweza kukusanya taarifa sahihi kwa lengo la kutumika na mifumo mingine. Hatua hizo ni kama ifuatavyo:-
Ujazaji wa fomu za Utambuzi na Usajili;
Uhakiki wa awali wa fomu za maombi;
Uingizaji wa taarifa kwenye mfumo wa kompyuta;
Kuthibitisha taarifa za mwombaji zilizo katika mfumo wa kompyuta;
Uchukuaji wa alama za vidole, picha na saini ya kielektroniki;
Utengenezaji wa Daftari Kuu la Taarifa za Watu;
Uhakiki wa mwisho;
Uchapishaji na Ugawaji wa Vitambulisho.
Mfumo huu una faida kubwa sana kwa taifa hili, hususan katika nyanja za kiuchumi kijamii na kiulinzi. Baadhi ya faida hizo ni kama ifuatavyo:-
Kumtambua Mtanzania, mgeni na mkimbizi
Kusidia katika kuongeza wigo wa ukusanyaji kodi ya Serikali kwa njia ya kuwatambua wachangiaji wengi zaidi
Kuondoa wafanyakazi hewa katika Mfumo wa Taarifa za Kiutumishi na Mishahara Serikalini
Kusaidia suala la utambuzi hususan kwenye mabenki na hivyo kuwasaidia wananchi kupata mikopo kwa urahisi zaidi
Kuisaidia Benki Kuu kuendesha credit reference bureau
Kusaidia katika bodi ya mikopo ya wanafunzi kwa kuwatambua wananfunzi wote waliokopa na kuwafuatailia ili waweze kurejesha miko yao na kuufanya mfuko kuwa endelevu
Kusaidia kuboresha Daftari la Kudumu la Wapigakura nchini
Kusaidia kwenye mifuko ya kijamii katika kutambua wanachama wao
Kusaidia kumtambulisha mhusika anapohitaji kupatiwa huduma katika taasisi mbalimbali kama vile benki, taasisi za mikopo na huduma za afya.
Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa inawashukuru wanahabari kwa kuendelea kutoa elimu kwa umma kuhusu Vitambulisho vya Taifa, kwa juhudi za uelimishaji wa wanahabari, sasa wananchi wanafahamu umuhimu wa Vitambulisho vya Taifa kutokana na umuhimu huo ndio maana ukienda kwenye vituo vya usajili wanataka wapatiwe hapo hapo. Kwa kweli mwitikio wa wananchi ni mkubwa na haya ni matunda ya wanahabari.
Umakini wa hali ya juu unahitajika kufanya shughuli hii ili kuhakikisha kwamba taarifa sahihi za watu zinapatikana na kutunzwa katika Mfumo kama alivyosisitiza Mhe. Rais Kikwete katika hotuba yake siku ya Uzinduzi wa Vitambulisho vya Taifa.
Kazi kubwa iliyo mbele ya NIDA ni kuhakikisha kwamba kazi hii inafanywa kwa uaminifu, uzalendo na weledi wa hali ya juu ili kuwa na taarifa sahihi za watu na kutekeleza majukumu iliyokasimishwa kwa wakati.

Comments

Popular posts from this blog