WATOTO WATATU WATEKETEA KWA MOTO- MAMA YAO AZIRAI



 Kamanda wa Polisi Mkoa wa Geita, Leonard Paul
Watoto watatu wakiwamo wawili wa familia moja, wamekufa kwa kuungua kwa moto usiku wa kuamkia jana na kusababisha mama yao kuzirai na kulazwa kituo cha Afya cha Katoro kwa matibabu.
Tukio hilo lilitokea katika Kitongoji cha Ludete Kijiji  cha Katoro Wilaya ya Geita  mkoani hapa.
Inadaiwa kuwa chanzo cha tukio hilo ni moto wa kibatari kushika  godoro katika nyumba waliyokuwa wanalala watoto hao  na wenzao wengine wawili wenye umri kati ya miaka 13 na 15 ambao wamenusurika.
Afisa Mtendaji wa Kata ya Katoro, Aloyce Kamuli, aliwataja watoto wa familia moja  waliokufa kuwa ni Japhet Boniface (5); Clavery Boniface (8) na wa jirani yao,  Farida Binamungu (8) alikuwa na mazoe ya kwenda kulala kwenye nyumba hiyo.
Kamuli alisema kuwa  Clavery na Farida walikufa baada ya kufikishwa Hospitali ya Wilaya ya Geita na Japhet alikufa papohapo baada ya kuungua kwa moto.
Aliwataja walionusurika kuwa ni Yasinta Binamungu (15) na Meliciana Boniface (13)
Baba wa watoto hao, Boniface Juma akizungumza na NIPASHE alisema kuwa alishtushwa na kelele kutoka kwenye nyumba waliyokuwa wakilala watoto hao.
Juma alisema alipokwenda kwenye nyumba hiyo iliyoezekwa kwa bati alikuta moto ukiwaka na kupiga yowe kuomba msaada kutoka kwa majirani zake na kwamba jitihada zake hizo hazikuwa za  mafanikio.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Geita, Leonard Paul amethibitisha kutokea kwa tukio hilo na kuanza upelelezi  ili kufahamu chanzo chake

Comments

Popular posts from this blog