Washauri wa rais Obama wakutana kuijadili Syria ;
Mjadala huo utahusu iwapo serikali ya Syria ilitumia silaha za kemikali katika shambulio mapema wiki hii.
Maafisa wa Marekani wamesema jana Ijumaa(23.08.2013) kwamba iwapo rais Obama atashiriki katika mkutano huo , hali inayoonekana kuwa kuna uwezekano , itakuwa kikao chake cha kwanza kamili akiwa na wasaidizi wake wa ngazi ya juu wa sera za mambo ya kigeni tangu shambulio la gesi ya sumu siku ya Jumatano katika kitongoji kimoja mjini Damascus.
Uamuzi bado
Lakini afisa huyo ambaye amezungumza kwa masharti ya kutotajwa jina, ametahadharisha dhidi ya matarajio kuwa uamuzi wowote wa mwisho huenda unaweza kutolewa katika duru hii ijayo ya majadiliano.
Wakati huo huo wizara ya ulinzi inayaweka tayari majeshi yake iwapo rais Barack Obama ataamua kuchukua hatua ya kijeshi dhidi ya Syria, amesema waziri wa ulinzi wa Marekani Chuck Hagel siku ya Ijumaa.
Huku kukiwa na miito kadha ya kujingilia kati kijeshi baada ya utawala wa Syria kutumia kile kinachodaiwa kuwa ni silaha za kemikali wiki hii, makamanda wa jeshi la Marekani wamenajitayarisha kwa uwezekano mbali mbali kwa rais Obama iwapo ataamua kuanzisha mashambulio dhidi ya utawala wa Syria, Hagel amewaambia waandishi habari akiwa katika ndege yake iliyokuwa ikielekea nchini Malaysia.
Lakini amekataa kutoa taarifa zaidi kuhusiana na wapi majeshi ya Marekani yatawekwa pamoja na vifaa huku kukiwa na hali ya kuongezeka kwa vita vya wenyewe kwa wenyewe nchini Syria.
"Wizara ya ulinzi inawajibu wa kumpa rais uwezekano kwa kila aina ya hali," Amesema Hagel.
Meli zawekwa katika tahadhari
Amesema wakati afisa wa wizara ya ulinzi akisema kuwa jeshi la majini litapanua uwapo wake katika bahari ya Mediterranean kwa kuweka meli ya nne ikiwa na uwezo wa kubeba makombora.
Kikosi cha sita cha jeshi la Marekani , kikiwa na wajibika katika bahari ya Mediterranean , kimeamua kuibakisha manowari ya USS Mahan katika eneo hilo badala ya kuiruhusu kurejea nyumbani katika bandari ya Norfolk , jimboni Virginia.
Manowari nyingine tatu hivi sasa zimewekwa katika eneo hilo, USS Gravely , USS Barry na USS Ramage. Meli zote nne za kivita zina makombora kadha ya Tomahawk.
Meli hizo za ziada zinairuhusu wizara ya ulinzi kuchukua hatua za haraka iwapo Obama ataamuru shambulio la kijeshi.
"Rais ameitaka wizara ya ulinzi kutoa mapendekezo mbali mbali. Pamoja na hayo , wizara ya ulinzi iko tayari na imekuwa tayari kutoa uwezekano wa aina yoyote kwa rais wa Marekani ," Hagel amesema.
Mkuu hiyo wa wizara ya ulinzi pamoja na maafisa wengine wa wizara ya ulinzi katika utawala wa rais Obama wameweka wazi kuwa hakuna uamuzi ulikwisha chukuliwa iwapo kuchukua hatua za kijeshi dhidi ya utawala wa rais Bashar al-Assad.
Magazeti ya Marekani yamekuwa yakieleza kuwa kuna hali ya kutokubaliana ndani ya utawala wa Marekani kuhusiana na hatari ya kujiingiza katika vita vingine katika mashariki ya kati.
Comments
Post a Comment