Ndege ya Rais yadaiwa kubebea mkaa
Wabunge
wa CCM Zanzibar wameibua zengwe jipya dhidi ya Makamu wa Kwanza wa Rais,
Maalim Seif Sharif Hamad kwamba anatumia ndege ya Rais kubebea mkaa,
mihogo na ndizi kutoka Pemba kwenda Unguja.
Habari
zilizopatikana kutoka ndani ya serikali ya Mapinduzi Zanzibar zinaeleza
kuwa, tuhuma hizo zilitolewa na wabunge hao wakati wa kikao chao na Rais
wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, Dk Ali Mohamed Shein mwezi
uliopita.
Kitendo
hicho kinachodaiwa kufanyika mwezi uliopita kimeonekena kuwakera baadhi
ya viongozi wa Serikali wakiwamo wabunge wa CCM Zanzibar, ambao wakati
wa kikao hicho na Rais Dk Shein mwezi uliopita mjini Zanzibar,
walilizungumza kwa uchungu na kuomba Rais amuonye Maalim Seif kwa
kuigeuza ndege ya Rais kuwa ya mizigo.
Anayedaiwa
kuibua hoja hiyo ni Mwenyekiti wa Umoja wa Vijana Taifa (UVCCM), Sadifa
Juma Khamis, ambaye alisema kuwa kitendo hicho cha Makamu wa Kwanza wa
Rais kutumia ndege hiyo kubebea mkaa, mihogo na mikungu ya ndizi
kinadhalilisha Ofisi ya Rais.
Katibu wa
Wabunge wa CCM Zanzibar, Mbunge wa Magomeni, Mohammed Chombo
alipoulizwa na gazeti hili kuhusiana na suala hilo alikiri wabunge hao
kulifikisha suala hilo kwa Rais Shein.
"Tulimweleza
Rais matatizo mengi likiwamo na hilo la Makamu wa Kwanza wa Rais
kutumia ndege ya Serikali kubebea mihogo na mkaa," alisema.
Alisema kuwa Rais aliwaambia kuwa ameyapokea malalamiko hayo na kwamba atayafanyia kazi.
Chombo alisema kuwa kwa sasa wanamsubiri Rais Shein awaite kuwapa majibu ya matatizo yao.
Baadhi ya
wabunge wa CCM Zanzibar ambao walizungumza na gazeti hili, walisema
kuwa kitendo hicho ni matumizi mabaya ya mali za umma kwa sababu kuna
vyombo vingi vya usafiri vinavyoweza kutumika kusafirishia mizigo hiyo.
Ofisa
mmoja ambaye hakutaka kutajwa jina lake kutoka Mamlaka ya Ndege za
Serikali, akizungumzia utaratibu wa viongozi wa Serikali kutumia ndege
hizo, alisema viongozi wa juu wa Serikali ya Muungano na Zanzibar hukodi
ndege zao.
Alisema hajawahi kuona ndege kubebea mkaa, hata ndege ya jeshi hajawahi kuona ikibeba mkaa.
Hata
hivyo, Katibu wa Wabunge wa CUF, Mohammed Habibu Mnyaa, alisema madai
hayo ya wabunge wa CCM ni siasa chafu dhidi ya Makamu wa Kwanza wa Rais
na kwamba wao wanaamini hawezi kufanya jambo hilo.Alisema Maalim Seif
anaheshimika na ni mzoefu katika utawala hawezi kufanya jambo hilo,
wakati kuna meli ambazo zinaweza kutumika kusafirishia bidhaa hizo
kutoka Pemba kama akitaka.
"Hizi ni
siasa chafu za wabunge wa CCM dhidi ya Maalim Seif, sisi tunaamini
hawezi kufanya jambo hilo hata kidogo," alisema Mnyaa.
Waziri wa
Nchi Ofisi ya Makamu wa Kwanza wa Rais, Fatma Abdulhabib Fereji
alipoulizwa kuhusiana na suala hilo, alisema hana taarifa na madai hayo.
"Sina taarifa na yoyote, ndiyo kwanza nayasikia kutoka kwako," alisema.
Kaimu
Katibu Mkuu wa CUF Taifa, Julius Mtatiro alipoulizwa jana kuhusiana na
suala hilo alisema kuwa Maalim Seif yuko nje ya nchi, hata hivyo msimamo
wa chama hicho ni kwamba madai hayo ya wabunge wa CCM siyo ya kweli.
Alisema
kuwa wamesikia kikao cha Wabunge wa CCM na Rais Shein, kwamba
wanachokidai kinaonyesha wazi kuwa wamekosa cha kuwafanyia wananchi wao.
Mtatiro
alisema hii siyo mara ya kwanza kwa viongozi wa CCM kumtungia tuhuma
Maalim Seif, kwani waliwahi kudai kuwa ni mwasisi wa Kikundi cha
Kiislamu cha Uamsho jambo ambalo siyo la kweli.
"Pia viongozi haohao wa CCM waliwahi kumtupia tuhuma nyingi ambazo baadaye zinakuja kuonekana siyo za kweli," alisema.
Alisema
hata kama Maalim Seif angetumia hiyo ndege kubebea zawadi kwani kuna
ubaya gani, mbona hata viongozi wa CCM hufanya hivyo?
"Kuna
ubaya gani, viongozi wa kitaifa kubebea zawadi, mbona hata viongozi wa
CCM wakiwa katika ziara wakipewa zawadi hubeba kwenye ndege?"
Huu ni
msukosuko mwingine katika serikali ya umoja wa kitaifa. Hivi karibuni
Serikali ya Umoja wa Kitaifa Zanzibar, iliingia kwenye msukosuko baada
ya viongozi wake kutofautiana kuhusu muundo wa Muungano. Maalim Seif
aliwahi kunukuliwa akisema anataka serikali ya mkataba, kauli ambayo
ilipingwa na viongozi wengine hususan kutoka CCM.
Wakati
makamu huyo wa kwanza akisema hivyo, Rais Shein alisikika akisema
anataka muundo wa sasa wa serikali mbili. Hata hivyo, wiki iliyopita
Mwanasheria Mkuu wa Zanzibar, Othman Masoud Othman alisema kuwa
mwarobani wa Muungano ni kuwa na serikali tatu:CHANZO MWANANCHI
Comments
Post a Comment