Mchakato wa kumrejesha Alex Massawe waiva
Mchakato
wa kumrejesha nchini, mfanyabiashara maarufu Alex Massawe, aliyekamatwa
Dubai, Falme za Kiarabu, umeanza rasmi baada ya Mahakama ya Hakimu Mkazi
Kisutu, kutoa hati ya kumkamata na kumrejesha nchini kujibu mashtaka.
Hati hiyo
ilitolewa juzi na Hakimu Mkazi Geni Dudu, kufuatia maombi ya Jamhuri,
yaliyotolewa na Wakili Mwandamizi wa Serikali Tumaini Kweka, baada ya
kumfungulia kesi ya jinai.
Katika kesi hiyo namba 150 ya mwaka 2013, Massawe anakabiliwa na mashtaka ya kughushi na kuwasilisha hati za nyumba.
Massawe
ambaye alikamatwa hivi karibu na Shirika la Kimataifa la Polisi
(Interpol), amekuwa akitafutwa akihusishwa na matukio ya uhalifu.
Mahakama hiyo ilitoa usahihi wa majina yake, kuwa ni Alex Siryamala
Massawe.
Kwa
mujibu wa Kweka, mtuhumiwa anayeshikiliwa katika nchi nyingine
anapoombwa kurejeshwa nchini,lazima kuwe na kesi ambayo anatakiwa kujibu
mashtaka, vinginevyo inaweza kuwa vigumu kwa sababu inaonekana kuwa
anatakiwa kwa masuala ya kisiasa.
Massawe
alikamatwa kati ya Juni 20 na 25, mwaka huu wakati wa ukaguzi kwenye
Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Dubai, kufuatia notisi ya Interpol
walioombwa na polisi wa Tanzania kumnasa mfanyabiashara huyo.
Siku
chake baada ya kumnasa, Interpol lilimtangaza mfanyabiashara huyo kwenye
tovuti yake kama mtu anayetakiwa kukamatwa na kurudishwa Tanzania
kujibu tuhuma za uhalifu.
Utaratibu
wa Interpol unaelekeza kuwa lazima litolewe tangazo la mtuhumiwa
kutakiwa kukamatwa na kurudishwa katika nchi anayotuhumiwa kufanya
makosa pale anaponaswa kwenye nchi ya kigeni.
Tangazo hilo kwa kawaida huwekwa picha, maelezo ya mtuhumiwa na alama nyekundu.
Taratibu
za Interpol zinasema kuwa mtuhumiwa anayewekewa alama nyekundu ni yule,
ambaye anatakiwa kukamatwa na kusafirishwa kwenye nchi anayotafutwa.
Hivyo
katika tangazo hilo, lililowekwa kwenye tovuti ya Interpol, picha ya
Massawe pia iliwekewa alama hiyo nyekundu kuashiria kuwa anatakiwa
kurejeshwa nyumbani kutoka UAE.
Mbali na
kesi hiyo, Massawe aliwahi kutajwa katika kesi ya mauaji ya
mfanyabiashara Onesphory Kituly.Kituly aliuawa katika mazingira ya
kutatanisha Novemba 6, 2011 akiwa nyumbani kwake Magomeni, Dar es Salaam
:chanzo mwananchi.
Comments
Post a Comment