JESHI LA POLISI LAMWAGA AJIRA.....
JESHI la Polisi nchini, limetangaza ajira mpya kwa vijana waliohitimu kidato cha nne na sita mwaka jana. Taarifa za jeshi hilo, ambazo zimewekwa kwenye mtandao wa jeshi hilo, zinasema vijana katika mikoa yote wanatakiwa kufika kwenye ofisi za makamanda wa polisi mikoa kwa ajili ya usaili.
Taarifa hiyo, ilisema kila mkoa umepangiwa siku yake na kwamba kila kijana anapaswa kuwa na vyeti halisi vya elimu yake pamoja na cheti cha kuzaliwa. “Kwa wale wote walioomba nafasi hii, wanapaswa kufika kwenye ofisi husika, hasa vijana waliohitimu kidato cha nne mwaka 2012 na wale waliohitimu kidato cha sita mwaka 2013.
“Katika kundi hili, wapo waliochaguliwa wajitokeze kwenye usaili kabla ya kujiunga na jeshi la polisi,” ilisema taarifa hiyo.
“Mwombaji anaruhusiwa kufanya usaili kwenye kituo chochote cha usaili kilicho karibu naye kulingana na tarehe zinavyoonesha, ili mradi tu awe amejiridhisha kuwa ni miongoni mwa walioitwa kwenye usaili.
“Jeshi la Polisi, halitahusika na lawama yoyote ile kwa mtu atakayekwenda kwenye kituo cha usaili ilhali jina lake si miongoni mwa walioitwa kufanya usaili.
“Mwombaji aliyeitwa kwenye usaili aje na vyeti vyake vyote vya masomo [(Academic Certificate(s)/Results slip(s) & Leaving certificate(s)], nakala halisi ya cheti cha kuzaliwa (Original Birth certificate). Hati ya kiapo cha kuzaliwa haitakubalika,” ilisema taarifa hiyo.
Taarifa hiyo, ilisema kuwa kila mwombaji anapaswa kuwa na namba ya simu itakayotumika kumjulisha endapo atachaguliwa.
“Kila mwombaji aliyeitwa kwenye usaili atajigharamia usafiri, chakula na malazi kwa muda wote wa usaili. Pia waombaji waje na kalamu za wino kwa ajili ya usaili wa kuandika.
Akizungumza na MTANZANIA jana, Msemaji wa Polisi, Advera Senso alisema ni mapema kutoa idadi kamili ya vijana wanaotakiwa kwa sababu bado wapo kwenye mchakato.
“Siwezi kukwambia tunachukua wangapi, tumetangaza nafasi za kazi bado tupo kwenye mchakato… hii inategemeana na bajeti yetu tuliyonayo, tukikamilisha tutawaambia tu,” alisema Senso.
Comments
Post a Comment