Homa ya ini ni ugonjwa hatari kuliko Ukimwi
Ugonjwa wa selimundu unasumbua wengi, umetengua ndoa za wengine, kwa sababu ya kutojua.
Hakuna shaka kwamba umewahi kusafiri nje ya nchi yako na kutakiwa kupata chanjo.
Kwa
wengine, chanjo hiyo ikiwamo ya homa ya ini imeonekana kama usumbufu na
udhia mtupu. Hata hivyo, wapo wengine ambao hawaufahamu ugonjwa huu.
Kwa wanaoujua, wanahofia kuwa ugonjwa huu una madhara makubwa pengine kuliko saratani na Ukimwi.
Homa hiyo au Hepatitis B inapewa uzito mdogo licha ya kuwa ni ya hatari kubwa.
Wataalamu
wanaeleza kuwa Hepatitis B au homa ya ini ni ugonjwa unaoambukizwa kwa
urahisi, wenye madhara makubwa na wenye uwezo wa kuambukiza kwa wepesi
kuliko Ukimwi.
Kitaalamu,
ugonjwa huu, husababishwa na virusi vya Hepatitis B (HBV) ambavyo
huathiri mfumo wa utoaji wa sumu mwilini. Inaelezwa kuwa robo tatu ya
watu ulimwenguni wameathiriwa kwa muda na homa ya ini na wengine milioni
350 wameathirika moja kwa moja.
Takwimu
zinaonyesha kuwa homa ya ini huua watu 600,000 kila mwaka katika sehemu
mbalimbali, idadi ya watu inayolingana na wale wanaokufa kutokana na
malaria.
Maradhi haya ya ini yanaelezwa kuwa yanaweza kusababishwa na kunywa kileo kupita kiasi au sumu inapoingia mwilini.
Hata hivyo, mara nyingi ugonjwa huu husababishwa na virusi.
Wanasayansi
kwa upande mwingine wamegundua virusi vitano vinavyosababisha ugonjwa
huu na wanasema kwamba huenda kuna vingine vitatu.
Matokeo
yake, sheria zimewekwa katika nchi mbalimbali ambazo zinamtaka kila raia
mgeni anayetaka kuingia katika nchi husika, kupata chanjo ya ugonjwa
huu ili kuepusha maambukizi.Kila anayechanjwa hupewa kadi maalum
itakayomwezesha kuingia katika nchi husika ili kuthibitisha kuwa
amechanjwa.
Hata
hivyo, ujanja mwingi umekuwa ukifanyika katika baadhi ya nchi ikiwamo
Tanzania ambapo watu hujipatia kadi za homa ya manjano kwa kutoa rushwa
na kukwepa kuchoma chanjo hiyo pindi wanapotaka kusafiri nje ya nchi
bila kujua madhara ya kutopata chanjo hiyo.
Vilevile,
chanjo hiyo iliwahi kukosekana nchini kwa zaidi ya mwezi mmoja kutokana
na sababu ambazo haziwekwi wazi na mamlaka zinazohusika.
Hatari
kubwa ya ugonjwa huu inatajwa ni namna ya uambukizaji wake ambapo,
unaposhika damu au majimaji ya mwilini ikiwemo mbegu za uzazi huweza
kuambukizwa.
Wataalamu
wanaeleza ubaya wake ni kuwa unaweza kuambukizwa kwa kufanya ngono na
hata kwa kushika majimaji ya mwili wa mtu aliyeathirika ikiwemo damu,
mate, machozi na mkojo.
Taarifa
za Shirika la Afya Duniani(WHO) zinaeleza kuwa kirusi cha homa ya ini
kinaweza kuishi nje ya mwili wa binadamu kwa siku saba na kwa wakati
huu, kirusi hiki kinaweza kusababisha maambukizi iwapo mtu hajapata
chanjo ya kuuzuia.
Watanzania
wengi bila kujua wamekuwa wakiugua maradhi mbalimbali yanayosababishwa
na homa ya ini na bila kufahamu ini limekuwa likiathirika taratibu.
Dk Yuki
Mark wa Hospitali ya Parktown North, Johanesburg, nchini Afrika Kusini
anasema kuwa homa ya ini aina ya B inaweza kuua kimyakimya bila
kuonyesha dalili zozote.
"Huenda
dalili zikaonekana waziwazi miaka mingi baada ya mtu kuambukizwa.
Zinapoonekana, huenda tayari ini limenyauka au lina saratani na magonjwa
hayo huua asilimia 25 ya watu walio na virusi vya HBV," anasema Dk
Mark.
Aidha,
mtaalamu huyo anasema, dalili kuu zinazojulisha kuwa mtu ana homa ya ini
ni kutapika, kuchoka kupita kiasi, kuathirika kwa ini, homa na mkojo
kuwa wenye rangi ya njano iliyokolea sana.
"Unaweza kuharisha na kutapika au kupata maumivu katika eneo fulani la tumbo lako, macho na ngozi kuwa vya njano," anaeleza.
Homa ya
ini aina ya B, inaweza kuingia mwilini mwa mtu kwa njia ya ngono, kama
ilivyo Ukimwi na magonjwa mengine ya zinaa. Hivyo basi, majimaji katika
mwili wa mwanadamu yanaweza kuwa chanzo cha maambukizi."Watu wengi
wanaendelea kuambukizwa kwa kutiwa damu yenye virusi hivyo, hasa katika
nchi ambako hakuna vifaa bora vya kuchunguza virusi hivyo katika damu.
Virusi vya HBV vina uwezo mkubwa zaidi wa kuambukiza kwa kulinganishwa
na virusi vya Ukimwi," anasema Dk Mark
Anaongeza:
"Hata kiasi kidogo cha damu yenye virusi hivyo kama ile inayobaki
kwenye wembe, inaweza kupitisha virusi hivyo na tone la damu iliyokauka
kwa juma moja au hata zaidi inaweza kumwambukiza mtu virusi hivyo."
Dk Mark
anasema, madhara mengi huweza kumkumba mtu aliyepata maambukizi ya homa
ya ini, kwani anaweza kupata shinikizo la damu, anaweza kuathirika
ubongo au hata kupooza sehemu ya mwili wake.
Angalizo
ambalo mtaalamu huyo anaeleza ni kuwa baada ya mtu kuambukizwa homa
hiyo, hawezi kupona, kwani dawa kuu ya ugonjwa huu ni chanjo ya kuzuia
homa ya manjano (yellow fever vaccination).:CHANZO MWANANCHI.
Comments
Post a Comment