BILIONEA AMTWANGA RISASI MFANYABIASHARA WA MADINI ARUSHA
- Get link
- X
- Other Apps
JIJI
la Arusha na Mkoa wa Manyara, hali ya hewa ilishachafuka, wingu zito
limefunika kufuatia kuuawa kwa kupigwa risasi, mfanyakazi wa Kampuni ya
Tanzanite One, Onesmo William Mushi (pichani).
Mtuhumiwa
wa mauaji hayo ni bilionea wa madini, mkazi wa Arusha, Joseph
Mwakipesile ‘Chusa’ ambaye ni mfanyabiashara anayemiliki migodi,
Mererani wilayani Simanjiro, Manyara.NA GLOBAL PUBLISHER
ONESMO ALIVYOUAWA
Habari zimedai kwamba Onesmo akiwa eneo lake la kazi, mgodini chini, alipigwa risasi mbili kifuani ambazo ziliondoa uhai wake.
Tukio hilo lilitokea saa 8 usiku, Julai 20, mwaka huu, chanzo kikitajwa kwamba ni mgogoro wa kugombea madini.
Imedaiwa
kuwa Onesmo, akiwa na wafanyakazi wenzake wa Tanzanite One ambao
wamefahamika kwa jina mojamoja, Kennedy na Leonard, walikutana na
wachimbaji wadogowadogo hivyo kutokea mvutano wa kimaslahi.
Habari
zimedai kwamba miongoni mwa wachimbaji hao wadogo, alikuwepo Chusa
ambaye ndiye anadaiwa kufanya mashambulizi dhidi ya Onesmo.
FAMILIA YALIA KUMPOTEZA ONESMO
Julai 25, mwaka huu, Onesmo alizikwa kijijini kwao, Uswaa, Machame, Hai, Kilimanjaro hivyo kuhitimisha safari yake hapa duniani.
Vilio
na huzuni vilitanda kipindi chote cha mazishi ya Onesmo, huku sikitiko
kubwa likielekea kwa mjane wa marehemu ambaye ameachiwa watoto wawili
ambao atawalea bila baba.
Mke wa marehemu, watoto wake na ndugu wengine walikuwa wanyonge muda wote wa mazishi, kuonesha namna walivyoguswa na kifo hicho. MERERANI YATIKISIKA
Wiki
moja baada ya Onesmo kuuawa, wafanyakazi wa Tanzanite One wapatao 200,
walilitikisa eneo la Mererani na kusimamisha shughuli zote za uchimbaji
madini mpaka wapate tamko la serikali.
Kishindo
cha wafanyakazi hao kilisababisha shughuli kusimama hata katika migodi
ya wachimbaji wadogo, kwani hasira zilikuwa kali mno.
Awali,
wafanyakazi wa Tanzanite One waligoma kufanya kazi wakiitaka
menejimenti ya kampuni hiyo kufuatilia haki zote, ikiwemo mtuhumiwa wa
mauaji kukamatwa na kufikishwa kortini.
Baadaye,
wafanyakazi hao walikusanyika na mabango kisha kushinikiza sheria
kuchukua mkondo wake, vilevile wakaituhumu serikali kufumbia macho suala
hilo.
Aidha,
wafanyakazi hao walibeba mabango yenye ujumbe ambao uliwatuhumu moja
kwa moja baadhi ya viongozi wa jeshi la polisi pamoja na wale wa madini
Kanda ya Kaskazini kwamba hawaaminiki katika kutenda haki. MIGODI YAFUNGWA
Kutokana
na kifo cha Onesmo, Wizara ya Nishati na Madini, imeifunga kwa muda
migodi minne inayozunguka eneo la mgodi wa Kampuni ya Tanzanite One ili
kusafisha hali ya hewa iliyochafuka.
Wizara
imefanya hivyo kufuatia malalamiko ya wafanyakazi wa Tanzanite One
kwamba kifo cha Onesmo kimesababishwa na serikali kulea mgogoro wa
mipaka kwa muda mrefu.
Kamishna
Msaidizi wa Madini Kanda ya Kaskazini, Mhandisi Benjamini Mchwampaka,
alisema kuwa migodi iliyofungwa ni ile inayomilikiwa na wafanyabiashara
Joseph Mwakipesile ‘Chusa’, Jackson Simon, Abdulhakim Mula pamoja na
mwingine aliyetajwa kwa jina moja la Maning’oo. SERIKALI YACHUKUA HATUA
Kamanda
wa Polisi Mkoa wa Manyara, ACP Akili Mpwapwa, aliliambia gazeti hili
kuwa Chusa alikamatwa yapata wiki mbili zilizopita, baada ya jeshi lake
kujiridhisha na tuhuma dhidi yake.
“Tuliona
tuhuma dhidi yake zina nguvu ndiyo maana tukamkamata,” alisema Mpwapwa
na kuongeza: “Siku tatu zilizopita (kutoka Jumapili iliyopita),
alifikishwa mahakamani, akasomewa mashtaka kwa mara ya kwanza na sasa
hivi yupo gerezani.
“Sijajua
atarudishwa lini mahakamani lakini hii ninayokupa ni taarifa ya uhakika
kwamba huyo bwana yupo gerezani. Tulimkamata na kumfikisha mahakamani
kama mtuhumiwa wa mauaji, siyo kwa ajili ya kuisaidia polisi.” TATIZO LA MGOGORO
Kwa mujibu wa taarifa za Mererani, mgogoro wa mipaka kati ya wachimbaji wadogo na Kampuni ya Tanzanite One ni wa muda mrefu.
Imeelezwa
kwamba mara kwa mara, wafanyakazi wa kampuni hiyo wamekuwa wakikutana
na wachimbaji wadogo mgodini chini, hivyo kuibua mvutano.
Kitendo cha wachimbaji wadogo kukutana mgodini chini na wafanyakazi wa Tanzanite One, kinajulikana kama Mtobozano.
Kwa
upande mwingine, imekuwa ikidaiwa kuwa Mtobozano ni lugha ya kulainisha
mambo, kwani ukweli ni kwamba ni kitendo cha wachimbaji wadogo kuvamia
mgodi wa Tanzanite One na kupora madini.
Imeelezwa
kuwa baadhi ya wafanyabiashara wanaomiliki migodi Mererani, hujipatia
fedha haramu, kwa kuiba madini ya tanzanite katika migodi ya Tanzanite
One.
Kufuatia
hali hiyo, Mchungaji wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania
(KKKT), Usharika wa Uswaa Machame, Robinson Manga, alisema wakati wa
ibada ya mazishi ya Onesmo kwamba lazima serikali itafute ufumbuzi wa
kudumu kuhusiana na mipaka Mererani.
Mchungaji
Manga alisema: “Tatizo la migogoro kati ya wachimbaji wadogo wa madini
ya tanzanite na wawekezaji wakubwa limekuwa la miaka mingi, serikali
inatakiwa kuangalia upya mipaka na kupata ufumbuzi wa kudumu.”
- Get link
- X
- Other Apps
Comments
Post a Comment