as cannes yamwagia sifa kapombe
Shomari Kapombe akitambulishwa rasmi AS Cannes
RASMI, klabu ya Daraja la Nne
Ufaransa, AS Cannes imetangaza katika tovuti yake kwamba katika
kujiimarisha ili kutoka katika kipindi kigumu, imeboresha kikosi chake
kwa kumsajili kiungo Mtanzania, Shomari Salum Kapombe. (HM)
Klabu hiyo imesema hiyo pia itakuwa fursa kwa mchezaji huyo kutoka Simba SC ya Tanzania kujipatia uzoefu wa kimataifa akiwa na Weupe hao Ufaransa.
Imemuelezea Kapombe, kama kinda mwenye
umri wa miaka 21, ambaye hadi sasa amekwishachezea mechi 14 timu yake
ya taifa, Taifa Stars pamoja na kumkabidhi jezi kuanza rasmi mazoezi na
wenzake.
Na imevutiwa naye zaidi baada ya
wasifu wake kusema anaweza kucheza nafasi nyingine pia, zikiwemo za
ulinzi, hivyo atakuwa msaada mkubwa kwa kocha Jean-Marc Pilorget msimu
huu.
Imesema viongozi wanafanya jitihada kubwa kuhakikisha wanainua kiwango chake haraka ili aweze kufanikiwa zaidi Ulaya.
Wiki iliyopita, Simba SC ilitangaza kumuunganisha Kapombe na AS Cannes kwa mkataba wa maridhiano maalum.
Mwenyekiti wa Simba SC, Alhaj Ismail
Aden Rage, alisema kwamba katika mkataba huo mpya na wa aina yake kuwahi
kufanywa na klabu yoyote ya Tanzania, Simba imekubali mchezaji huyo
achezee timu hiyo iliyo katika ligi daraja la nne la Ufaransa kwa
makubaliano ya kumtafutia timu ya kucheza ndani ya miaka miwili kutoka
sasa.
Rage amesema timu hiyo itamgharimia
Kapombe kwa kila kitu wakati atakapokuwa nchini Ufaransa na endapo
atauzwa kwenda katika timu nyingine yoyote, Simba itapata gawio lake
kupitia mauzo hayo na lengo la mchezaji huyo kubaki Ufaransa ni pia
kumtengeneza awe bora zaidi kuliko alivyo sasa.
Rage alisema katika mkataba huo mpya
wa Kapombe, Simba imeangalia zaidi maslahi ya taifa na ya mchezaji
kuliko ya klabu kwa vile kama mchezaji huyo atapata nafasi Ulaya, hilo
litafungua milango kwa wachezaji wengi wa Kitanzania ambao kwa sasa
hawapati fursa Ulaya.
Wakala wa Kapombe, Denis Kadito,
alisema ingawa Kapombe ameonekana kuwa mchezaji mzuri, kutofahamika kwa
jina la Tanzania kumekuwa kikwazo kikubwa kwa kupata kwake nafasi ya
moja kwa moja na ndiyo maana.
Miongoni mwa nyota maarufu wa Ufaransa waliowahi kupita katika klabu hiyo ni Patrick Vieira, Zinedine Zidane na Luis Hernandez.
Klabu hiyo inafahamika kwa kuwa na
miundombinu imara ya kumwezesha mwanasoka kijana kukuza uwezo wake na ni
matarajio ya Simba Sports Club, Kadito, Cannes na Kapombe mwenyewe
kwamba atakuwa mchezaji bora zaidi kuliko sasa katika kipindi cha mwaka
mmoja kutoka sasa.
Kutokana na mkataba huo wa Kapombe na
Cannes, Simba sasa imeongeza mkataba wake na mchezaji huyo kwa muda wa
miaka mitatu zaidi, kwa vile mkataba wake wa sasa unamalizika Aprili
mwakani.
Kama Kapombe hatafanikiwa kupata timu
katika kipindi cha miaka miwili kutoka sasa, atarejea katika klabu ya
Simba kuendelea na majukumu yake. Chanzo: binzubeiry
Comments
Post a Comment