SIMBA USO KWA USO NA COASTAL UNION KESHO TANGA

Kikosi cha Simba ya Libolo
Wekundu wa Msimbazi Simba, “Taifa Kubwa” muda huu wapo Mjini Tanga kwa ajili ya mechi ya kujipima uwezo dhidi ya wenyeji wa dimba la Mkwakwani, wagosi wa Kaya Coastal Union hapo kesho.
Akizungumza kwa njia ya simu, kocha msaidizi wa Simba, Jamhuri Kiwhelo “Julio” amesema wachezaji wote  wapo salama na wapo safarini kuelekea Tanga ambapo kesho majira ya saa 10 jioni wanatarajia kucheza mechi moja kali ya kujipima ubavu  dhidi ya vijana wa Hemed Morocco, huku kivutio kikubwa kikiwa ni wachezaji wa zamani wa Simba ambao kwa sasa wapo Coastal, beki kisiki, Juma Said Nyoso na kiungo fundi, Haruna Moshi Shaaban Mnyamwezi “Boban”.
Boban na Nyoso walitemwa enzi za kocha Mfaransa, Patrick Liewig baada ya kutolewa ligi ya mabingwa barani Afrika na LIbolo ya Angola kwa tuhuma za utovu wa nidhamu pamoja na akina Ramadhan Suleiman Chombo “ Redondo”, Ferlix  Mumba Sunzu, David Luhende, Juma Abdallah, Mwinyi Kazimoto na Amir Maftah.Na Fullshangwe
Kocha Julio amesema Simba wanajipanga vziuri ili kutwaa ubingwa wao, na ndio maana wanajitahidi kucheza mechi za kirafiki kwa lengo la kujua mapungufu yako wapi na kuyafanyia kazi kabla ya kuanza kwa msimu mpya wa ligi kuu soka Tanzania bara mnamo Agosti 24 mwaka huu.
“Awali ya yote nimshukuru sana mwenyezi Mungu mwingi wa rehema, wachezaji wetu wapo salama, kwa sasa tupo njiani kuelekea Tanga ambapo kesho tutakuwa na mechi ya kirafiki dhidi ya wenyeji wetu  coastal Union”.
“Kwa watu wanaojua soka, wagosi wa kaya ni timu nzuri na imekamilika sana, kwahiyo mechi itakuwa nzuri na tutahitaji kucheza kwa kushinda”. Alisema Julio.
Kocha huyo mwenye maneno mengi aliwataka mashabiki wa Simba kuwa na subiri kwani kikosi kinasukwa vibaya sana, na msimu ujao lazima wapinzani wakione cha moto.
Simba ikiwa chini ya kocha Abdallah Kibaden “King Mputa” , mechi ya kesho ni mfululizo wa mechi za kirafiki tano mpaka sasa , kwani walikuwa ziarani mkoani Tabora, Shinyanga, Mara na hatimaye kurejea Dar es salaam.
Kwa upande wa Coastal Union, mechi ya kesho ni ya pili katika majira haya ya joto ya usajili nchini Tanzania.
Wiki iliyopita walishuka dimbani dhidi ya wakusanyaji mapato wa URA ya Uganda na kushinda bao 1-0. Bao hilo pekee lilifungwa na mshambuliaji mpya aliyesajiliwa kutoka Polisi Morogoro, Kenneth Masumbuko, huku wataalamu waliosajiliwa kutoka Simba, Nyoso na Boban wakionesha burudani kubwa kwa mashabiki waliofurika uwanjani.

Comments

Popular posts from this blog