SAKATA LA MADAWA YA KELEVYA, RIPOTI KAMILI HII HAPA
- Get link
- X
- Other Apps
Na Mwandishi Wetu
WATANZANIA ambao idadi yao inaweza kupita mamia, wameshanyongwa nchini China kutokana na kupatikana na hatia ya kujihusisha na biashara ya madawa ya kulevya.
Ripoti maalum ya madawa ya kulevya, iliyofanyiwa kazi na gazeti hili kwa kukusanya taarifa ndani ya nchi, Afrika Kusini na China kwenyewe, inaweka hadharani siri ya mamia ya Watanzania kunyongwa.
Katika ripoti hiyo, inaonesha kwamba mataifa ya Afrika Kusini na Uganda, yapo mstari wa mbele kuripoti taarifa za raia wao kunyongwa China lakini Tanzania imekuwa ikisuasua.
“Huu ukimya wa serikali yetu, unafanya wengi kukosa taarifa sahihi, matokeo yake wanajiingiza kwenye biashara hiyo haramu ambayo mtu akikamatwa tu China na akikutwa na hatia lazima anyongwe,” alisema Joel Mabruki, mfanyabiashara wa nguo na simu kati ya Tanzania na China.
Mabruki aliongeza: “Kama serikali yetu ingekuwa na utaratibu wa kutangaza kila Mtanzania anayenyongwa China, pengine vijana wengine wangeogopa na baadhi yao wangeacha kabisa. Hivi sasa idadi inaongezeka kwa sababu hawaambiwi ukweli.”NA GLOBAL PUBLISHER
KITENGO CHA MADAWA YA KULEVYA KINAJUA
Kwa mujibu wa Mkuu wa Jeshi la Polisi, Kitengo cha Kuzuia na Kudhibiti Madawa ya Kulevya, Godfrey Nzowa, ofisi yake inazo taarifa kuhusu Watanzania kunyongwa China lakini akatupa mpira kwa Mkurugenzi wa Kuzuia na Kudhibiti Madawa ya Kulevya, Christopher Shekiondo.
“Kuhusu idadi na majina, hilo suala aulizwe mkurugenzi. Ila ukweli ni kwamba Watanzania wengi wanakamatwa China na wananyongwa,” alisema Nzowa.
MAAFA PAKISTAN
Kwa upande mwingine, Nzowa alisema kuwa watu wanaizungumzia sana China lakini ukweli ni kwamba nchi nyingine ambayo inanyonga Watanzania wengi ni Pakistan.
Nzowa alisema kuwa pengine taarifa za Pakistan hazipatikani sana kutokana na mwingiliano wa Tanzania na nchi hiyo, tofauti na China ambayo Watanzania wanakwenda na kurudi kila siku iendayo kwa Mungu.
“Tunaposema madawa ya kulevya ni janga kubwa inafaa ieleweke hivyo. Watanzania wanaonyongwa China na Pakistan ni wengi sana. Tuwe makini juu ya hili na tuzingatie kwelikweli,” alisema Nzowa.
TAARIFA ZA MITANDAO YA KIJAMII
Tofauti na mataifa mengine ambayo ripoti za raia wao kukamatwa na kunyongwa China hutolewa rasmi na balozi zao, hapa Tanzania, habari huenezwa na mitandao ya kijamii.
Mfano; mitandao ya kijamii ndiyo pekee iliyoripoti kuhusu kunyongwa kwa mrembo mwanamitindo (jina tunalo) aliyeshiriki video ya wimbo Twende Zetu wa mwanamuziki Saidi Juma ‘Chegge’, aliyewashirikisha Amani James Temba ‘Mheshimiwa Temba’, Feruzi Mrisho Rehani ‘Ferouz’ na Yessaya Ambilikile ‘YP’.
Vilevile, alipokamatwa aliyewahi kushika nyadhifa za makamu mwenyekiti na katibu msaidizi kwenye Klabu ya Simba (jina tunalo), mitandao ya kijamii iliandika bila serikali kutoa tamko rasmi.
Hata hivyo, kutokana na kukosekana na taarifa rasmi kutoka serikalini, mitandao ya kijamii ilitoa habari zenye kushitua, nyingine ikidai mtu huyo aliyewahi kuwa kiongozi wa Simba alifungwa miaka 70 jela, nyingine ikieleza kwamba tayari alishanyongwa.
MWAKALEBELA ATOA USHUHUDA WAKE
Katibu Mkuu Mstaafu wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Frederick Mwakalebela, alipozungumza na gazeti hili, alisema kuwa kati ya mwishoni mwa mwaka 2009 na mwanzoni mwa 2010, alikwenda China katika safari ya kikazi.
“Nikiwa kule, niliambiwa taarifa za Watanzania wengi ambao walinyongwa baada ya kukutwa na hatia ya kujishughulisha na biashara ya madawa ya kulevya,” alisema Mwakalebela.
Alipoulizwa kuhusu kiongozi huyo wa Simba, Mwakalebela alijibu: “Nikiwa China niliambiwa amenyongwa. Niliporudi hapa nchini ndiyo nikasikia amefungwa miaka 70.”
Mwakalebela aliongeza: “Ukweli ni kwamba kwa taarifa nilizopata nikiwa China, Watanzania wengi sana wananyongwa kwa sababu ya madawa ya kulevya. Naweza kusema ni mamia. Ikiwa kwa muda mfupi niliokuwepo pale nimeambiwa karibu watu 10, je mwaka mzima inakuwaje?”
WENGINE WANAPONZWA NA WANIGERIA
Mfanyabiashara Mtanzania, Hashim Rau, ambaye hufanya biashara zake kati ya Tanzania, Afrika Kusini na China, alisema kuwa kuna Watanzania walinyongwa baada ya kuponzwa na Wanigeria.
Rau alisema, Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa O. R. Tambo, uliopo nje kidogo ya Jiji la Johannesburg, umewasababisha matatizo Watanzania wengi kutokana na tabia yao ya ukarimu.
Alisema: “Mtanzania anaweza kutoka na biashara yake kuja kuuza Afrika Kusini, baada ya hapo anapanda ndege ya moja kwa moja kwenda China. Akiwa uwanja wa ndege anakutana na Mnigeria muuza madawa ya kulevya.
“Mtanzania anakuwa hana mizigo mingi, kwa hiyo yule Mnigeria anamwomba Mtanzania amsaidie kupitisha begi lake moja kwenye mzani, akidai kuwa yeye mizigo yake ni mingi, anaogopa atatozwa fedha nyingi.
“Kumbe lile begi linakuwa na unga. Sasa Mtanzania kwa kutojua, atakubali, baada ya hapo lile begi litaandikwa jina la Mtanzania. Mbele ya safari kama litavuka salama, Mnigeria atamshukuru Mtanzania na kuchukua begi lake lakini likikamatwa, Mnigeria atakimbia, Mtanzania atabaki na mashtaka ambayo mwisho wake ni kunyogwa China.”
Akisimulia ushuhuda wake, Rau alisema kuwa aliwahi kuombwa msaada wa aina hiyo na Mnigeria mmoja lakini alipotaka kukagua begi lina nini ndani alikataa.
“Alipokataa nikague ndani ya begi kuna nini nami nikamkatalia kumsaidia kwa sababu naujua mchezo wao. Sasa pale uwanjani alikuwepo Mtanzania mwingine mwenye asili ya Tanga (jina tunalo), alipoombwa na yule Mnigeria alikubali.
“Nilijitahidi kumwonesha ishara hakunielewa, mwisho nikamwambia asikubali lakini hakunielewa. Tulipofika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Guangzhou Baiyun, China, yule Mtanga alikamatwa baada ya lile begi kukutwa na madawa ya kulevya mchanganyiko wa heroine, cocaine na methamphetamine.
“Kama kawaida, yule Mnigeria alitoweka. Mimi niliujua ule mchezo lakini nilijiweka pembeni kwa sababu ningejionesha najua chochote au namtambua yule Mtanga ningeshikiliwa. Tena pengine na mimi ningekuwa nimeshanyongwa siku nyingi zilizopita kwa sababu hiyo ni kesi ya mwaka 2008.
“Watanzania wajue kwamba China hakuna mchezo, hawana muda wa kufuatilia ushahidi, ukikutwa na unga, ikithibitika hivyo, kwao huo ni ushahidi tosha kwamba wewe ndiye mmiliki na unanyongwa,” alisema Rau.
PEMBE TATU HATARI
Uchunguzi wa gazeti hili kwa kufanyia kazi matukio ya Watanzania kukamatwa na madawa ya kulevya, umebaini kuwa pembe tatu hatari imetengenezwa na wauza unga katika nchi za Tanzania, Afrika Kusini na China.
Imebainika kwamba wafanyabiashara wa madawa ya kulevya, wamekuwa wakisafirisha idadi kubwa ya madawa hayo kwenda Afrika Kusini ambako husafirishwa kwa mafungu kwenda China.
Ripoti za hivi karibuni, zinaongeza nguvu katika madai kwamba Tanzania na Afrika Kusini, kuna udhaifu mkubwa wa udhibiti wa madawa ya kulevya ndiyo maana wafanyabiashara huingiza na kusafirisha mizigo mikubwa kwa urahisi.
Kutokana na hali hiyo, wafanyabiashara hao husafirisha madawa ya kulevya yenye uzani mkubwa tena kupitia katika viwanja vya ndege kisha kuziweka katika mafungu madogomadogo kwenda China na kwingineko ambako mahitaji ni makubwa na bei ni nzuri.
Uchunguzi umebaini kuwa sheria kali za China za kudhibiti madawa ya kulevya, zinasababisha uhaba mkubwa wa mihadarati ndani ya nchi hiyo, kwa hiyo anayefanikiwa kupitisha, huuza kwa bei kubwa sana.
WATUMWA WENGI NI WANAWAKE
Mwanamke, Janice Bronwyn Linden, 38, raia wa Afrika Kusini, alinyongwa China mwaka 2011, baada ya kukutwa na hatia ya kusafirisha madawa ya kulevya aina ya methamphetamine yenye uzito wa kilogramu tatu.
Nobanda Nolubabalo, 23, raia wa Afrika Kusini, alikamatwa Uwanja wa Ndege wa Suvarnabhumi, Bangkok, Thailand, akiwa ameficha cocaine zenye uzani wa kg 1.5.
Watanzania, Agnes Gerald na Melisa Edward, hivi karibuni walikamatwa Afrika Kusini, wakiwa na mzigo wa madawa ya kulevya aina ya methamphetamine, yenye thamani ya shilingi bilioni 6.8.
Mtanzania mwingine, Sharifa Mahmoud, yupo nchini Misri akisubiri adhabu ya kunyogwa, baada ya kukutwa na hatia ya kuingiza nchini humo, madawa ya kulevya aina ya heroine.
Saada Ally Kilongo, ni mwanamke mwingine wa Kitanzania ambaye hivi karibuni alikamatwa Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Mwalimu Nyerere, Dar es Salaam, akiwa na madawa ya kulevya aina ya methamphetamine yenye thamani ya zaidi ya shilingi milioni 170.
Zahra Thomas, kutoka Visiwa vya Sao Tome, alikamatwa mwaka jana, Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Hong Kong, akiwa na mzigo wa heroine wenye uzito wa kilogramu 12.
Mnigeria, Helen Okechukwu, alinaswa Falme za Kiarabu akiwa na madawa ya kulevya aina ya cocaine, uzani wa kg 20.
Mifano hiyo, inatosha kuonesha jinsi wanawake wanavyotumiwa na wauza unga kusafirisha mizigo yao kwa imani kwamba mwanamke ni rahisi kupita sehemu za ukaguzi bila kushtukiwa, vilevile kukwepa dhuluma.
MSEMAJI WA POLISI
Msemaji wa polisi nchini, Advera Senso, aliliambia gazeti hili wiki iliyopita kuwa Watanzania wengi wananyongwa China kwa sababu ya hatia ya kujihusisha na biashara ya madawa ya kulevya.
“Majina ya wahusika kwangu hayapo. Ila nafahamu kuwa wengi wananyongwa,” alisema Senso.
NI SIRI KUBWA
Habari zinasema kuwa mara nyingi utekelezaji wa adhabu ya kifo China ni siri lakini ubalozi wa Tanzania hujulishwa.
“Ila mara nyingi wauza madawa ya kulevya husababisha mkanganyiko wa uraia kutokana na kuwa na hati hata tatu, hii husababisha ubalozi wa Tanzania China ubaki na siri ya mtu aliyenyongwa bila kujulishwa ndugu zake,” kilisema chanzo chetu na kuongeza:
“Ikitokea ndugu wanaulizia hapo hupewa taarifa kamili kuhusu taarifa za ndugu yao kama ameshanyongwa au bado anatumikia kifungo.”
Chanzo chetu kilibainisha kuwa mbali na kunyongwa, vilevile hutokea vifo vya kimafia, kwani wauza unga huuana wao kwa wao ili kudhulumiana.
“Ikitokea mtu ameuawa, taarifa zikifika ubalozini, zinafuatiliwa lakini kama hazieleweki hubaki siri,” kilisema chanzo.
STORI YA MKUMBUKWA
Aprili mwaka jana, kijana wa Kitanzania, Mkumbukwa John Shayo, aliuawa China na maiti yake ilikaa mochwari mwaka mzima, kabla ya kuletwa nchini mwaka huu na kuzikwa mkoani Mwanza.
Mkumbukwa, anasadikiwa kuuawa na mtandao wa wauza madawa ya kulevya, ingawa haijulikani sababu yake ni nini.
TUNACHUNGUZA
Gazeti hili linaahidi kupita kila panapotakiwa ili kukamilisha orodha kamili ya Watanzania walionyongwa China kisha ripoti hiyo, tutaichapisha katika matoleo yajayo.
CHINA YAONGOZA KWA KUNYONGA
Chati iliyopo ukurasa wa kwanza ni takwimu za Shirika la Kimataifa la Haki za Binadamu, Amnesty International mwaka jana ambayo inaonesha kwamba China ndiyo kinara wa kunyonga watu duniani ambapo inanyonga maelfu kila mwaka kwa makosa mbalimbali ikiwemo kusafirisha madawa ya kulevya, ikifuatiwa na Pakistan na Falme za Kiarabu.
- Get link
- X
- Other Apps