RAIS KIKWETE AZIONYA NCHI CHOKOZI DHIDI YA ARDHI YA TANZANIA
- Get link
- X
- Other Apps
RAIS Jakaya Kikwete amesema Serikali ya Tanzania iko tayari kukabiliana na mtu yeyote atakayejaribu kuichezea au kuichokoza kwa namna yoyote ile, ikiwamo kumega ardhi yake, itamfundisha kama ilivyomfundisha aliyekuwa Rais wa Uganda, Idd Amin Dada, katika Vita ya Kagera.
Kikwete
alisema serikali ilimshikisha adabu Amin alipojaribu kumega sehemu ya
ardhi ya Tanzania, hivyo haitosita kufanya hivyo tena kwa asiye na nia
njema na Tanzania.
Kiongozi huyo
mkuu wa nchi alitoa onyo hilo jana wakati akizungumza na wananchi
katika maadhimisho ya Siku ya Mashujaa yaliyofanyika kitaifa katika
makaburi yaliyopo Kambi ya Kaboya, wilayani Muleba, mkoani Kagera.
Rais
Kikwete alisema serikali iko tayari kukabiliana na kupambana kwa nguvu
yoyote ile bila kuogopa mtu anayejaribu kuichezea nchi ya Tanzania kwa
lengo la kukwaza amani na utulivu uliopo hivi sasa.
“Laleni
usingizi salama. Msisikilize maneno ya mitaani, kwa sababu jeshi letu
liko imara kabisa kulinda nchi yetu na mipaka yake. Yeyote atakayejaribu
kuivamia ama kuichokoza nchi yetu atakiona cha mtema kuni. Nchi iko
salama na jeshi liko imara kulinda nchi yetu.
“Ujumbe
wetu mkubwa wa leo ni kwamba tuko tayari wakati wote na saa yoyote
kuilinda nchi yetu na mipaka yake. Hatuna nchi nyingine. Hivyo, kamwe
hatuwezi kumruhusu yeyote kuichezea nchi yetu, ama kuichezea ama kuimega
nchi hii. Kama tulivyoshughulika na Amin naye tutashughulika naye vivyo
hivyo,” alisema.
Rais
Kikwete alisema shughuli ya kulinda amani ni ghali. “Na moja ya gharama
hizo ni makaburi haya ya ndugu zetu ambao wamelala hapa baada ya
kupoteza maisha yao katika vita dhidi ya nduli Idi Amin. Tutaendelea
kuwaenzi kwa sababu hawa walijitolea maisha yao kulinda mipaka ya nchi
yetu, kulinda amani ya nchi yetu na usalama wake na wetu sote,” alisema
Kikwete.
Kiasi cha askari 619 waliopoteza maisha yao wamelazwa kwenye makaburi hayo ya Kaboya.
Rais
Kikwete amesema kuwa serikali yake kwa ushauri wa Jeshi la Wananchi wa
Tanzania inaangalia jinsi gani ya kuwahudumia vizuri zaidi askari wa
Tanzania ambao walipata vilema katika vita hiyo na bado wanaendelea
kuishi.
“Nimesikia
kuna malalamiko kuhusu ubora wa jinsi tunavyowahudumia, hivyo
tutazungumza na Jeshi kuhusu njia bora zaidi ya jinsi ya kuwahudumia.
Hawa ni mashujaa wetu, ni watu waliojitolea maisha yao kuweza kulinda
uhuru wetu. Tunaendelea kuwashukuru na kuwaenzi. Hii ndiyo sababu
sherehe za leo ni sherehe kubwa kwa nchi yetu,” alisema.
Rais
Kikwete alishuhudia sherehe za kumbukumbu hizo ambapo miongoni mwa mambo
mengine, ametembelea makaburi ya askari wa Tanzania waliopoteza maisha
yao wakati wa kuikomboa nchi kutokana na uvamizi wa Amin wa Uganda na
kuona silaha zilizotumika katika vita hiyo mwaka 1978/79.
Naye Mkuu
wa Jeshi la Wananchi wa Tanzania ( JWTZ ), Davis Mwamunyange, alisema
jeshi lake liko makini na lina uwezo mkubwa wa kupambana dhidi ya wale
wanaotaka kuivunja amani iliyopo.
Alisema uwepo wa amani na utulivu nchini umechangia watu washiriki
kikamilifu kwenye shughuli za maendeleo pasipo kuhofia chochote, hivyo
anayetaka kuivuruga JWTZ haitamuachia wala kumuonea huruma.
Mwamunyange
alisema JWTZ wako mstari wa mbele kuwalinda na kuwatetea kwa hali na
mali wananchi wa Tanzania ili kuhakikisha wanakuwa katika hali ya
utulivu na amani.
Naye
Askofu Msaidizi wa Jimbo Katoliki la Bukoba, Mehtodius Kilaini, alisema
ni wajibu wa viongozi wa dini na serikali kutambua wajibu wao katika
kutenda haki na kutetea wananchi.
Askofu
Kilaini alisema hayo wakati akiongoza sala ya kuwaombea mashujaa 619
waliouawa katika vita ya Kagera kati ya mwaka 1978 na 1979 wakitetea
taifa lao.
Alisema
ushindi wa nchi unatokana na umoja, mshikamano na uvumilivu baina ya
viongozi na wananchi wanaoungana kutetea masilahi ya taifa lao kutoka
kwa adui.
Aliongeza kuwa ili nchi iendelee pamoja na kustawi vizuri kwa jamii yake, amani ni msingi mkubwa unaopaswa kuzingatiwa.
Askofu
Kilaini aliwataka viongozi wa dini na serikali kuhubiri amani pamoja na
kutekeleza wajibu wa majukumu yao kwa wakati na kufuata utaratibu ulio
sahihi kwa wananchi wake.
- Get link
- X
- Other Apps
Comments
Post a Comment