RAIS KIKWETE AINGILIA KATI KODI ZA LINE.....
HATMAYE RAIS KIKWETE AMEZITAKA MAMLAKA HUSIKA ZIKUTANE HARAKA ILI TATIZO LIISHE
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,
Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete ameagiza Wizara za Serikali zinahusika
na kodi na mawasiliano pamoja na makampuni ya simu za mikononi nchini
kukutana mara moja kutafuta jinsi gani ya kumaliza mvutano wa kodi mpya
ya kadi za simu hizo za mikononi.
Rais
kikwete ametoa maelekezo hayo jioni ya leo, Jumanne, Julai 23, 2013
wakati alipokutana na viongozi wa Wizara ya Fedha, Wizara ya
Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia na wawakilishi wa makampuni ya simu
ya TTCL, Airtel, Vodacom, Tigo na Zantel katika kikao cha pamoja
kilichofanyika Ikulu, Dar es Salaam.
Rais
Kikwete amesema kuwa lengo kuu la mkutano huo wa pamoja kati ya Wizara
hizo za Serikali na makampuni ya simu yawe ya kupendekeza jinsi gani ya
kuziba pengo la Sh. Bilioni 178 ambazo zitapotea katika Bajeti iwapo
kodi hiyo kwa kadi za kuongelea za simu za mikononi italazimika kufutwa
na Serikali kupitia marekebisho kwenye Muswada wa Fedha wa Bajeti ya
Mwaka 2013/2014.
Rais
Kikwete amewaambia wawakilishi wa pande hizo mbili kuwa huwezi tena
kuifuta moja kwa moja kodi hiyo bila kutafuta njia nyingine za kupata
fedha za kujaza pengo hilo la Sh. Bilioni 178 ambazo tayari Bunge
limezipangia matumizi.
“Nawaombeni
kaeni pamoja, wekeni bongo zenu pamoja, wekeni akili yenu pamoja
tutafute namna gani tunaweza kujaza pengo hili la Sh. Bilioni 178 endapo
tutakubaliana kuwa kodi hii inawabebesha wananchi mzigo mzito na kuwa
pengine menejimenti ya kodi yenyewe ni ngumu,”Rais Kikwete amewaambia wawakilisho hao.
Katika
Bajeti ya Serikali ya mwaka 2013/2014, Serikali imeweka kodi ya Sh.
1,000/= kwa mwezi kwa kila mtumiaji simu kwa ajili ya kufanya
mawasiliano kwa kutumia simu ya mkononi.
Imetolewa na:
Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais,
Ikulu.
Dar es Salaam.
23 Julai, 2013
Comments
Post a Comment