POLISI 117 WATIMULIWA KAMBINI KWA UTOVU WA NIDHAMU
Wanafunzi 117 wa Polisi, wamefukuzwa katika Chuo cha Taaluma na Mafunzo ya Polisi (MPA), kilichopo Manispaa ya Moshi, mkoani Kilimanjaro.
Waliotupiwa virago na kufutwa kwenye kozi hiyo ni wale waliopoteza sifa za kuendelea na mafunzo ya kijeshi baada ya kukutwa na makosa ya utovu wa nidhamu, utoro na matatizo ya kiafya.
Kamishna Msaidizi wa Polisi (ACP), Matanga Mbushi, ambaye ni mkuu wa chuo hicho alisema katika mahojiano maalumu kwamba, waliotimuliwa chuoni ni kati ya askari wanafunzi 3,189 waliokuwa wamesajiliwa kuanza mafunzo ya kijeshi katika chuo hicho, Oktoba 25 mwaka jana.
Kati yao askari 115 ni wale wa Polisi na askari wawili wanatoka katika Idara ya Uhamiaji iliyopo chini ya Wizara ya Mambo ya Ndani.
Kufukuzwa kwa wanafunzi hao , kuna akisi moja kwa moja jinsi menejimenti ya chuo hicho ilivyojipanga upya kupunguza wimbi la baadhi ya askari walioko kazini na ambao wanalipaka matope jeshi hilo kutokana na kupotoka kimaadili kwa kutaka kujinufaisha kimaslahi.
Askari hao walikuwa waungane na wenzao ambao wanatarajiwa kuhitimu mafunzo ya awali ya polisi na uhamiaji, Julai 26 mwaka huu baada ya kupatiwa mafunzo ya medani za kivita. Mgeni wa heshima atakayeshuhudia kuagwa kwa askari 3,092 ni Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Dk. Emmanuel Nchimbi.
Kamishna Mbushi alisema askari hao pamoja na mambo mengine wamepatiwa mafunzo maalumu ya utunzaji wa amani ya nchi iliyopo, Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (ICT), Haki za Binadamu, Masuala ya mtambuka (Cross cutting issues), Usimamizi wa majanga na Usimamizi wa kazi za Polisi.
Mafunzo mengine ni pamoja na Polisi Jamii, Sheria ya ushahidi, Sheria ya mwenendo wa makosa ya jinai, Upelelezi wa makosa ya jinai, Usalama barabarani na stadi za kazi.
Taarifa za awali kutoka ndani ya chuo hicho, zinaeleza kuwa mahafali hayo ya Polisi yatatanguliwa na medani za kivita yatakayofanyika Julai 25 huko katika Kijiji cha Kilele-Pori, Wilaya ya Siha.
Comments
Post a Comment