MKE ALIYETAKA KUMUUWA MUME NA MTOTO KWA AJILI YA MALI AFIKISHWA MAHAKAMANI ARUSHA
- Get link
- X
- Other Apps
Ni
mke wa mfanyabiashara maarufu wa Tanzanite Arusha, anayedaiwa kupanga
njama za kumuua mumewe na mtoto wa kambo wa kiume anayeishi Bukoba.
Arusha.
Mwanamke anayedaiwa kupanga njama za kumuua mumewe wa ndoa na mtoto wa
mume huyo, amepandishwa mahakamani akiwa na mtuhumiwa mwingine wa mauaji
hayo.
Janeth Jackson (32), mkazi wa Moshono, Arusha na Novatus Elias,
walifikishwa jana mbele ya Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Wilaya
ya Arusha /Arumeru, Devotha Kamuzora, wakisomewa makosa mawili ya kula
njama ya kutaka kumuua Simon Jackson ambaye ndiye mume wa Janeth.
Mwendesha Mashtaka wa Serikali, Edna Kasala, alidai mahakamani hapo
kuwa washtakiwa wote walitenda kosa la pili la kula njama na kutaka
kumuua Desderi Sabas, ambaye ni mtoto wa mke mwingine kwa mume huyo
anayeishi Bukoba, mkoani Kagera.
Washtakiwa wote hawakutakiwa kujibu lolote kwa sababu Mahakama hiyo kisheria haina mamlaka ya kusikiliza kesi za mauaji.
Kasala iliomba mahakama kuwanyima dhamana washtakiwa, kwa sababu
watuhumiwa wengine wawili wanatafutwa hivyo na upelelezi haujakamilika.
Alidai kutokana na uzito wa tuhuma hizo, maombi hayo ya kuwanyima
dhamana washtakiwa yameambatana na hati ya kiapo ya Mkuu wa Upelelezi
Makosa ya Jinai Mkoa wa Arusha.
“Mheshimiwa tunafahamu kwamba dhamana ni haki ya washtakiwa kikatiba,
lakini kutokana na mazingira ya kesi hii kuwa magumu, tunaomba dhamana
isitolewe ili kuwatafuta watuhumiwa wengine wa kesi hii,” alidai Kasala.
Kwa upande wake,Wakili wa utetezi, Fidelis Peter, alipinga maombi
hayo na kutaka mahakama itoe dhamana kwa washtakiwa kwa sababu ni haki
yao ya kikatiba na kwamba hilo ni kosa lao la kwanza.
Sababu nyingine ya kupinga maombi ya upande wa mashtaka, ni kwamba
washtakiwa wanaweza kuvuruga upepelezi wakiachiwa siyo za msingi kwani
ni watu wanaoaminika katika jamii.
“Mheshimiwa sababu za kuwanyima dhamana washtakiwa hazina uzito
wowote, pia mshtakiwa wa kwanza (Janeth) ana mtoto wa miezi sita na
tangu akamatwe alhamisi iliyopita hajamwona wala kumnyonyesha hivyo
anastahili kupewa dhamana,”alidai Wakili Peter.
Hata hivyo, baada ya kusikiliza maombi ya pande zote mbili, Hakimu
Kamuzora, alikubaliana na maombi ya upande wa mashtaka na kuamuru
watuhumiwa wapelekwe mahabusu hadi Agosti 5, mwaka huu kesi hiyo
itakapotajwa tena.
Katika kesi hiyo iliyovuta hisia za watu wengi jijini hapa, inadaiwa
Janeth alitaka kumuua mumewe ambaye ni mfanyabiashara wa madini ya
Tanzanite na mwanaye wa kiume, ili arithi mali na utajiri alionao
mfanyabiashara huyo.
Akiwa amejifunika uso muda wote alipokuwa mahakamani, Janeth
alionekana kuwa na mawazo mengi na macho mekundu kwa sababu ya kulia
baada ya njama hizo kugonga mwamba.
Awali kabla ya kukamatwa kwa mwanamke huyo, taarifa zilieleza kuwa,
mwanamke huyo alitumia fedha nyingi kulipa majambazi waliotakiwa
kutekeleza tukio hilo lakini mmoja wa majambazi hao aliamua kuvujisha
siri hiyo polisi iliyofanikisha kukamatwa kwa wahusika kabla ya kutenda
mauaji hayo.
Mume wa mwanamke huyo alinukuliwa awali akisikitika na kuhoji kwa nini mke huyo alifikia kupanga hilo.
- Get link
- X
- Other Apps
Comments
Post a Comment