MFALME MSWATI WA SWAZILAND AAONDOKA NCHINI NA AMEWATAKA WATANZANIA WABADILIKE


Mfalme Mswati wa Swaziland akisindikizwa na Waziri Mkuu, Mizengo Pinda wakati alipoondoka kwenye uwanja wa ndege wa Mwalimu Julius Nyerere jijini Dar es salaam kurejea nyumbani baada ya kufungua maonyesho ya Biashara ya Kimataifa kwenye uwanja wa Mwalimu Nyerere Julai 1,2013.

Waziri Mkuu, Mizengo Pinda akiagana na mfalme Mswati wa Swaziland ambaye aliondoka nchini baada ya kufungua maonyesho ya Kiataifa ya Biashara kwenye uwanja wa Mwalimu Julius Nyerere jijini Dar es salaam Julai 1, 2013. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu) 
 ---------
 MFALME Mswati (III) wa Swaziland amewataka Watanzania kubadilika kwenda sambamba na Soko la Pamoja la Afrika Mashariki kwa kubuni bidhaa mbalimbali zenye ubora.
 
 Alisema watanzania pia wanapaswa kuzipa kipaumbele bidhaa zinazozalishwa nchini kwa lengo la kushindana katika biashara duniani.
Mswati aliyasema hayo jana wakati akifungua Maonyesho ya 37 ya Kimataifa ya Biashara katika Viwanja vya Mwalimu Nyerere, barabara ya Kilwa, Dar es Salaam .

Alisema endapo wafanyabiashara wataibua bidhaa zenye ubora na kuziendeleza itasaidia nchi kukua katika uchumi pamoja na kunufaika na Soko la Pamoja la Afrika Mashariki (EAC).

Tanzania ni miongoni mwa nchi tajiri na endapo kama itazingatia bidhaa zinazozalishwa na wananchi wake uchumi wa nchi utakuwa kwa kasi na nchi itahesabika kama ni miongoni mwa nchi tajiri duniani.

“Maonyesho haya yanatoa fursa kwa watanzania kubuni na kujifunza mbinu mbalimbali za biashara kufanya ushindani wa biashara duniani,”alisema Mswati.

Pia alisema maonyesho hayo yanatoa fursa ya kuendeleza bidhaa zenye ubora wa hali ya juu ikiwa ni miongoni mwa agenda kuu ya mdahalo waliojadili viongozi mbalimbali wa ushirikiano wa biashara.

Alisema anaamini serikali ya Tanzania inatoa kipaumbele kwa bidhaa zinazozalishwa nchini zinazoingizwa katika soko la ndani kwa sababu kufanya hivyo kutasaidia kuinua uchumi wa nchi.

Mfalme Mswati alisema anaamini ushirikiano kati ya Tanzania na Swaziland utadumu ikiwa ni pamoja na kutangaza bidhaa za ndani na kuutangaza utamaduni wa nchi.

Comments

Popular posts from this blog