Kauli ya Ban K-Moon juu ya mauaji ya askari wa JWTZ Darfur





Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa (UNO), Ban K-Moon(pichani chini), amesema amesikitishwa na kuhuzunishwa na mauaji ya askari saba wa Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ), lililofanywa na waasi wa Sudan Julai 13, mwaka huu.

Askari hao wa JWTZ waliokuwa Darfur, Sudan ya Kusini kulinda amani kwa mujibu wa UNO, walishambuliwa na waasi hao karibu na kambi ya Manawashi eneo la Khor Abeche, mji wa Darfur Jimbo la Nyala ambapo pia askari wengine 17 walijeruhiwa baadhi yao vibaya.
Katika salamu zake hizo kupitia kwa Msemaji wake, Katibu Mkuu huyo wa Uno, ameelezea masikitiko yake kuhusiana na vifo hivyo na kutoa pole kwa familia za marehemu waliokuwa wakilinda amani, Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Vikosi vya Umoja wa Afrika kwa Umoja wa Mataifa vya Kulinda Amani (Unamid).

Ban K-Moon amelaani shambulio hilo dhidi ya Unamid na kuelezea matumaini yake kwamba Serikali ya Sudan itachukua hatua zinazofaa kuhakikisha kwamba wahusika wanafikishwa mbele ya sheria.
Wakati huo huo, Taarifa iliyotolewa na Unamid juzi jioni ilisema wajumbe wa Baraza la Usalama wanalaani kwa nguvu zote mashumbulizi hayo dhidi ya askari wa vikosi vya Unamid.
"Wajumbe wa Baraza la Usalama wameelezea masikitiko yao na kutuma salamu za pole kwa familia za marehemu hao pamoja na kwa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.


Aidha, wameitaka Sudan kufanya upelelezi wa kina kuhusiana na tukio hilo na kuwafikisha wahalifu hao mbele ya mkono wa sheria.
Taarifa hiyo ya Unimad iliongeza kuwa shambulio lolote dhidi ya vikosi vya Unimad halikubaliki na kuonya kuwa lisitokee tena shambulio lingine la aina hiyo huku ikisisitiza pande zinazovutana Darfur kushirikiana kwa lengo la kufikia malengo yaliyokusudiwa.

Comments

Popular posts from this blog