JK yeyote ambaye atajaribu kuchezea mipaka ya Tanzania atakiona cha mtema kuni.
- Get link
- X
- Other Apps
Rais
wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Amiri Jeshi Mkuu, Mheshimiwa
Jakaya Mrisho Kikwete amesema kuwa yeyote ambaye atajaribu kuchezea
usalama na mipaka ya Tanzania atakiona cha mtema kuni.
Aidha,
Rais Kikwete amesema kuwa Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) liko
imara tayari kulinda mipaka ya Tanzania wakati wowote na saa yoyote.
Rais
Kikwete ametoa ujumbe huo mzito leo, Alhamisi, Julai 25, 2013, wakati
alipozungumza na wananchi wakati Maadhimisho ya Siku ya Kumbukumbu ya
Mashujaa kwenye Kambi la JWTZ ya Kaboya, Wilaya ya Muleba, Mkoa wa
Kagera.
Mara
baada ya kushuhudia sherehe za kumbukumbu hizo ambako miongoni mwa
mambo mengine ametembelea makaburi ya askari wa Tanzania waliopoteza
maisha yao wakati wa kuikomboa nchi kutokana na uvamizi wa Idi Amin wa
Uganda na kuona silaha zilizotumika katika vita hivyo vya 1978/79, Rais
Kikwete amewaambia mamia kwa mamia ya wananchi waliohudhuria sherehe
hizo:
“Laleni
usingizi salama. Msisikilize maneno ya mitaani kwa sababu Jeshi letu
liko imara kabisa kulinda nchi yetu na mipaka yake. Yeyote atakayejaribu
kuivamia ama kuichokoza nchi yetu atakiona cha mtema kuni. Nchi iko
salama na Jeshi liko imara kulinda nchi yetu,” amesema Rais Kikwete na
kuongeza:
“Ujumbe
wetu mkubwa wa leo ni kwamba tuko tayari wakati wote na, saa yeyote
kuilinda nchi yetu na mipaka yake. Hatuna nchi nyingine. Hivyo, kamwe
hatuwezi kumruhusu yeyote kuicheza nchi yetu, ama kuichezea ama kuimega
nchi hii. Kama tulivyoshughulika na Amin naye tutashughulika naye vivyo
hivyo.”
Rais
Kikwete amesema kuwa shughuli ya kulinda amani ni ghali mno:“Na moja ya
gharama hizo ni makaburi haya ya ndugu zetu ambao wamelala hapa baada
ya kupoteza maisha yao katika vita dhidi ya Nduli Idi Amin. Tutaendelea
kuwaenzi kwa sababu hawa walijitolea maisha yao kulinda mipaka ya nchi
yetu, kulinda amani ya nchi yetu na usalama wake na wetu sote.” Kiasi
cha askari 619 waliopoteza maisha yao wamelazwa kwenye makaburi hayo ya
Kaboya.
Rais
Kikwete amesema kuwa Serikali yake kwa ushauri wa Jeshi la Wananchi wa
Tanzania inaangalia jinsi gani ya kuwahudumia vizuri zaidi askari wa
Tanzania ambao walipata vilema katika vita hivyo na bado wanaendelea
kuishi.
“Nimesikia
kuna malalamiko lalamiko kuhusu ubora wa jinsi tunavyowahudumia na
hivyo tutazungumza na Jeshi kuhusu njia bora zaidi ya jinsi ya
kuwahudumia. Hawa ni mashujaa wetu, ni watu waliojitolea maisha yao
kuweza kulinda uhuru wetu. Tunaendelea kuwashukuru na kuwaenzi. Hii
ndiyo sababu sherehe za leo ni sherehe kubwa kwa nchi yetu.”
Imetolewa na:
Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais,
Ikulu.
Dar es Salaam.
25 Julai, 2013
- Get link
- X
- Other Apps
Comments
Post a Comment