GEORGE BUSH NA MKEWE KUTUA NCHINI KESHO



RAIS mstaafu wa Marekani, George W. Bush na mkewe, Laura wanatarajiwa kesho kuwa nchini kuhutubia kongamano linalojadili wajibu wa wake wa marais katika kuinua wanawake duniani.


Kuwasili kwa Bush, ni mwendelezo wa wiki hii Jiji la Dar es Salaam kuwa katika pilikapilika za kupokea ugeni wa watu maarufu. Kongamano hilo limeandaliwa na Taasisi ya George Bush na litafanyika kesho na keshokutwa.

Taarifa iliyotolewa na taasisi hiyo kwa vyombo vya habari , inasema kongamano hilo litahudhuriwa na wake mbalimbali wa marais akiwemo mke wa Rais wa Marekani, Michelle Obama.


Pia Mwanzilishi wa Taasisi ya Wanawake ya Cherie, Cherie Blair atahudhuria. Wake wa marais wa Afrika watakaohudhuria ni Mama Salma Kikwete, Chantal Campaore wa Burkina Faso, Roman Tesfaye wa Ethiopia, Maria da Luz Dai Guebuza (Msumbiji), Penehupifo Pohamba (Namibia), Sia Nyama Koroma (Sierra Leone), Janet Museveni (Uganda) na Christine Kaseba wa Zambia.


Kongamano hilo litajikita zaidi katika kujadili masuala ya kuwekeza kwa wake, kuimarisha Afrika lakini pia wajibu wa wake wa marais katika kuhamasisha wanawake katika maeneo ya elimu, afya na kuwakwamua kiuchumi.


“Kongamano hili litawakutanisha pamoja wake wa marais kutoka nchi mbalimbali duniani, maofisa wa Serikali, mashirika binafsi, Asasi zisizo za Kiserikali (NGOs) na wasomi kwa ajili ya kujadili mambo muhimu ya kuchukuliwa hatua ili kuweza kuwanufaisha wanawake,” ilisema taarifa hiyo.




Aidha mada zitakazowasilishwa na kujadiliwa katika kongamano hilo ni pamoja na kuinua wajasiriamali wanawake kiuchumi kupitia mafunzo na teknolojia, kuwapatia fursa wanawake wakulima kupata mafunzo ya kilimo cha kisasa, mafunzo kuhusu saratani ya matiti na umuhimu wa elimu kwa wanawake.


Amani, utulivu na uimara wa mfumo wa demokrasia ni miongoni mwa mambo yanayotajwa kuvutia viongozi hao wa kimataifa kuja nchini.

Comments

Popular posts from this blog