CCM YAPINGA UWEPO WA SERIKALI TATU....



Chama Cha Mapinduzi (CCM), kimepinga muundo wa Muungano wa Serikali tatu unaopendekezwa katika rasimu ya Katiba Mpya iliyotolewa na Tume ya Mabadiliko ya Katiba mwanzoni mwa wiki iliyopita. Chama hicho tawala kimesema bado kinaamini katika muundo wa Serikali mbili.  


Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM, Nape Nnauye aliwaambia waandishi wa habari mjini Dodoma jana kwamba mapendekezo yaliyowasilishwa mbele ya Tume hiyo yanabaki kama yalivyo, hivyo msimamo wao ni kuwapo kwa muungano wenye muundo wa Serikali mbili.

“Mapendekezo ambayo ndiyo msimamo wa chama tulishayawasilisha kwenye Tume kuwa sisi tunapendekeza mfumo wa Serikali mbili na siyo tatu wala moja,” alisema Nape alipokuwa akitoa taarifa ya uamuzi wa Kamati Kuu (CC) ya CCM iliyokutana usiku wa kuamkia jana kujadili suala hilo.

  Kauli ya Nape inafanana na matamshi ambayo yamewahi kutolewa na baadhi ya wanasiasa wakongwe ambao ni makada wa CCM wakiwamo, mawaziri wakuu wastaafu, Frederick Sumaye na John Malecela, Waziri wa Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Samuel Sitta na baadhi ya wabunge ambao mara kadhaa wamekaririwa wakipinga pendekezo la Serikali tatu.  


Hata hivyo, Nape alisema matamshi ya viongozi hao yalikuwa ni maoni yao binafsi na kauli yake ndiyo rasmi ya chama hicho... “Mimi ndiye msemaji wa chama hiki. Ndiye ninayeeleza msimamo wa chama chetu, yanayozungumzwa na watu wengine hata kama ni viongozi siyo msimamo wa chama ni maoni yao binafsi.”  


Habari ambazo gazeti hili ilizipata zinasema katika kikao hicho cha CC kulijitokeza hofu ya suala la wananchi kuwa na mamlaka ya kuwang’oa wabunge ikiwa hawatatekeleza masilahi yao na kwamba pendekezo hilo lina upungufu kwani halitafsiri masilahi hayo ni yapi.

Waunda kamati

Nape alisema rasimu iliyotolewa na Tume siyo waraka wa mwisho kwani bado unatoa fursa kwa Watanzania kuijadili na kutoa maoni yao na kwamba CCM kitatumia nafasi hiyo kuwasilisha maoni yake kuhusu jambo hilo.


 Alisema chama hicho kitawasiliana na wanachama wake zaidi ya 6,000 nchini ili waendelee kutoa maoni yao kuhusu suala hilo. “Wengi wanadhani rasimu hii ndiyo ya mwisho… hii ni ya mwanzo tu, itajadiliwa italetwa ya pili na ya tatu, kwa hiyo hatuwezi kusema kilichoelezwa kwenye tume ndiyo msimamo. 


Ndiyo maana tumeamua kurejesha suala hili kwa wanachama wetu liendelee kujadiliwa,” alisema na kuongeza:
“Kama wanachama wetu wakiamua kuwepo kwa Serikali tatu, hatutachakachua, tutayachukua na kuyapeleka kama msimamo wetu, lakini tutakubaliana ikiwa uamuzi utakuwa umewahusisha wanachama wetu katika ngazi zote.

“Hatuangalii kipengele kimoja tu. Tutapitia vipengele vyote hadi kuzimaliza kurasa zote zaidi ya 70 zinazoainisha mapendekezo ya Tume ya Jaji (Joseph) Warioba.”  

Alisema wanachama wake wanapaswa kuipitia na kuijadili rasimu hiyo kwa kuzingatia mapendekezo kilichoyatoa awali wakati wa mchakato wa kukusanya maoni ya Katiba Mpya. “Tulitoa maoni yetu na sasa tunaijadili Rasimu ya Katiba Mpya kwa kuzingatia maoni yetu yale, CCM tunakwenda kwa mujibu wa sheria,” alisema.


 Habari kutoka ndani ya CC ya CCM zinasema chama hicho kimeipa kazi kamati ambayo ilitumika kuandaa mapendekezo yake awali, kupitia rasimu hiyo na kufanya ulinganisho wa yale ambayo chama hicho kilipendekeza dhidi ya yale yaliyozingatiwa katika Rasimu ya Katiba hiyo.


“Kamati itafanya ulinganisho na baada ya hapo tutakwenda kwa wanachama kuwaeleza ni yapi tulipendekeza kama chama na ni yapi ambayo Tume imeyazingatia na hapo tutapata mawazo yao ambayo tutayatumia katika ngazi ya mabaraza ya Katiba,” kilisema chanzo chetu

Comments

Popular posts from this blog