Skip to main content

Profesa Kabudi: Niliandika barua ya kujiuzulu lakini ilichanwa

 Dar es Salaam. Waziri wa Mambo ya Nje nchini Tanzania, Profesa Palamagamba Kabudi amesema kuna wakati aliandika barua ya kujiuzulu lakini alinyang’anywa na ikachanwa.
Mbunge huyo wa kuteuliwa na Rais ameeleza hayo leo Ijumaa Januari 24, 2020 Ikulu jijini Dar es Salaam katika hafla ya utiaji saini makubaliano kati ya Serikali ya Tanzania na kamati ya madini ya Barrick.
Kabudi anasema alichukua uamuzi wa kuandika barua hiyo baada ya mchakato wa majadiliano na wajumbe wa Barrick kuwa magumu, kwamba aliona aibu kushindwa kazi aliyotumwa.
Amemtaja aliyemnyang’anya barua hiyo ambayo haikuifafanua kwa kina ni Kasmir Simbakuki.
“Nilifikia hatua nikafanya dhambi ya kukata tamaa nikasema jambo hili haliwezekani, niliona ni bora aibu na fedheha hiyo niibebe lakini barua niliyoandika sikufanikiwa kuileta.”
“Nilisema sijawahi kutumwa kazi na mkuu wangu wa nchi ikanishinda,” amesema Kabudi.
Amesema wakati huo alikuwa katika wakati mgumu kwani Rais wa Tanzania, John Magufuli alikuwa akiuliza mambo yanayoendelea, huku bungeni wabunge wakihoji majadiliano ambayo wakati huo hayakuwa yakienda vizuri.
“Kuna wakati walikuja Wachina tofauti wa kuwekeza tukaongea nao ila wakaingia mitini, huku bungeni unapigwa mijeledi, huku Wachina wale wameingia mitini, huku Rais anasubiri umalize, huku unajiuliza utatoka kwa aibu ila Mungu akasimama na sisi,” amesema Profesa Kabudi.
Waziri huyo ameomba radhi kwa lolote litakalopungua, akibainisha kuwa utakuwa upungufu wa kibinadamu, “ila tulifanya kazi kwa moyo wote na akili zote.”
Amesema katika hafla hiyo itasainiwa mikataba tisa.
Rais Magufuli wakati akianza kuzungumza baada ya kukamilika kwa utiaji saini huo aligusia suala la Profesa Kabudi, “ni kweli mengine Kabudi hajayasema, nilikuwa nampigia simu usiku na simu zake zote na akipokea ni matusi lakini nashukuru amekuwa mvumilivu, hongera sana Kabudi. Watanzania wavumilivu wapo.” SC mwananchi

Mwananchi


Ad 

Comments

Popular posts from this blog