Mshitakiwa Afariki Mahakamani

SHUGHULI zilisimama kwa muda katika Mahakama Kuu mjini Mbale nchini Uganda baada ya mtuhumiwa kuanguka na kufariki dunia.

Simon Mayuya mwenye umri wa miaka 54 ambaye ni mkazi wa kijiji Buyobo Wilaya ya Sironko nchini Uganda, alifariki dunia muda mfupi baada ya kuanguka katika chumba cha watuhumiwa kabla ya kupandishwa kizimbani.

Mayuya alikuwa amekaa miezi sita rumande katika gereza la Maluku ambapo alikua anakabiliwa na tuhuma za jaribio la mauaji. Anatuhumiwa kwa jaribio la kumuua binamu yake ambaye amemuajiri kama dereva wa lori.

Mwanasheria wa Mayuya aitwaye David Moli amesema mteja wake alikuwa anasumbuliwa na maumivu ya uti wa mgongo kutokana na kunusurika kwenye ajali ya gari aliyopata kabla ya kukamatwa na kuwekwa rumande.

Moli ameongeza kuwa kabla hali ya mteja wake kuwa mbaya aliiomba mahakama kumpa dhamana ili apelekwe hospitali kupatiwa matibabu kabla ya kurejea tena gerezani.

“Leo tulitakiwa kuwepo mahakamani kwa ajili ya kusikiliza maombi ya dhamana, lakini nimeshtushwa moyoni mwangu kusikia mteja wangu ameanguka na kugonga kichwa chake kwenye kiti kabla ya kupoteza maisha,” amesema mwanasheria wa Mayuya.

Mtoto wa marehemu, Tom Wetaka,  ambaye alishuhudia baba yake akianguka, amesema kuwa baba yake alianguka na kugonga kichwa kwenye kiti kilichokuwa kimekaliwa na mmoja wa walinzi wa wafungwa.

“Baba yangu alikuwa anaumwa na tayari hali yake ilikuwa imedhoofika. Alikuwa hawezi kutembea vizuri peke yake bila msaada. Walinzi wa wafungwa walikuwa wanamlazimisha kukimbia kama wafungwa wengine, ndiyo maana alikosa nguvu na kuanguka. Asingepoteza maisha kama angepata mtu wa kumsaidia kutembea kwa sababu wafungwa wengine pia wanajua kuwa ni mgonjwa,” amesema kijana huyo.

Comments

Popular posts from this blog