Mfumo Mpya wa Malipo Mamlaka za Serikali za Mitaa Kuboresha Huduma kwa Wananchi
Mfumo mpya wa malipo epicor toleo
Na. 10.2 unaotarajiwa kuanza kutumika Julai 1 mwaka huu na Mamlaka zote
za Serikali za Mitaa nchini umeelezwa kuboresha huduma kwa wananchi
kutokana na kuwa wa uwazi na kurahisisha kazi kwa watumiaji wa mfumo
huo.
Akieleza lengo la uboreshaji wa
mfumo huo leo, Jijini Dodoma wakati wa mafunzo ya kuwajengea uwezo
Maafisa Manunuzi kutoka Halmashauri za Mikoa ya Kigoma, Shinyanga,
Dodoma, Arusha, Manyara na Singida, mkufunzi wa mafunzo hayo kutoka
Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) Bw.
Agustino Manda amesema mfumo huo utapunguza kazi na kuongeza ufanisi wa
kazi kwa watumishi wa Mamlaka za Serikali za Mitaa hapa nchini.
“Mfumo huu utaweka mambo wazi,
watu watawajibika na mtumiaji wa mwisho ambaye ni mteja atapata huduma
nzuri na kuridhika na huduma atakayopewa,” amesema Manda.
Ameendelea kusema, lengo la
kuboresha mfumo huo ni kutoa huduma nzuri kwa Wananchi, Wananchi
kutocheleweshewa huduma, Halmashauri husika kuwa katika nafasi nzuri ya
kutoa huduma pamoja na kukusanya mapato vile ilivyotarajiwa.
Mkufunzi wa mafunzo ya mfumo wa
malipo Epicor toleo Na. 10.2 kutoka Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na
Serikali za Mitaa (TAMISEMI), Bw. Augustino Manda (aliyesimama) akitoa
maelezo ya awali ya mafunzo hayo kwa Maafisa Manunuzi kutoka Halmashauri
za Mikoa ya Dodoma, Singida, Shinyanga, Arusha na Manyara , leo Jijini
Dodoma.
Aidha amewataka Maafisa Manunuzi
hao kutoa maelekezo mazuri kwa wateja wao namna mfumo huo unavyofanya
kazi ili wateja waweze kuelewa na kuridhika na huduma wanazohitaji.
Manda amesema Ofisi ya Rais
TAMISEMI kwa kushirikiana na Mradi wa Uimarishaji wa Mifumo ya Sekta za
Umma (PS3) kupitia mifumo mbalimbali ya kielektroniki inayoendelewa
kuboreshwa hapa nchini wamefanikiwa kupunguza gharama za watumishi
kusafiri kwenda Makao Makuu ya Serikali kufuata huduma mbalimbali.
Ametolea mfano wa Mfumo wa
Kielektroniki wa Kuandaa Mpango wa Bajeti ya Serikali za Mitaa (PlanRep)
kuwa umewezesha Halmashauri kuandaa bajeti zao wakiwa katika ofisi zao
tofauti na awali, ambapo walilazimika kusafiri kwenda Dar es Salaam au
Dodoma. Hivyo mradi huo umeipunguzia Serikali gharama za kuwalipa
watumishi hao wanapokuwa nje ya vituo vyao vya kazi.
Kwa upande wa Meneja Mradi wa PS3
Dodoma, Bw. Gideon Muganda amesema PS3 itaendelea kushirikiana na
Serikali kwa ukaribu kuhakikisha mifumo mbalimbali ya sekta za Umma
inaboreshwa hapa nchini.
Baadhi ya washiriki wa mafunzo ya
mfumo mpya wa malipo Epicor toleo Na. 10.2 ambao ni Maafisa Manunuzi
kutoka Halmashauri za Mikoa ya Dodoma, Singida, Shinyanga, Arusha na
Manyara wakifuatilia mafunzo hayo yaliyoandaliwa na TAMISEMI kwa
kushirikiana na Mradi wa Uimarishaji wa Mifumo ya Sekta za Umma (PS3),
leo Jijini Dodoma.
Mfumo wa malipo epicor 10.2 utatoa
taarifa zote zinazohusiana na fedha katika Halmashauri husika ikiwemo
mapato, matumizi pamoja na bajeti ya Halmashauri.
Mafunzo ya Mfumo huo yanaendelea
kutolewa katika vituo sita ambavyo ni Dodoma, Mwanza, Mtwara, Iringa,
Kagera na Mbeya ambapo yamehusisha watumiaji wa mfumo huo ambao ni
Waweka Hazina, Wahasibu, Maafisa TEHAMA, Maafisa Manunuzi na Wakaguzi wa
Ndani kutoka Mamlaka za Serikali za Mitaa nchini lengo ikiwa ni
kuwajengea uwezo wa namna ya kutumia mfumo huo hasa katika maeneo
yaliyoboreshwa. Mafunzo hayo yanafanyika kwa wiki tatu ambapo yameanza
Juni 4 na yanatarajiwa kumalizika Juni 21, mwaka huu.
Mkufunzi wa mafunzo ya mfumo wa
malipo Epicor toleo Na. 10.2 kutoka Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na
Serikali za Mitaa (TAMISEMI), Bw. Augustino Manda (aliyesimama) akitoa
maelekezo ya namna ya kutumia mfumo huo kwa Maafisa Manunuzi kutoka
Halmashauri za Mikoa ya Dodoma, Singida, Shinyanga, Arusha na Manyara,
leo Jijini Dodoma.
………………..
Na: Lilian Lundo – MAELEZO, Dodoma.
Comments
Post a Comment