Wezi Watokomea na Mashine ya ATM Ikiwa na Pesa

equity-atm-mashineNAIROBI: Polisi jijini Nairobi nchini Kenya wamemkamata mlinzi wa Benki ya Equity kuhusiana na tukio la wizi lililotokea Jumamosi iliyopita ambapo watu wanaoaminika kuwa ni wezi waliiba mashine ya kielektroniki ya kutolea pesa, Automatic Teller Machine (ATM) pamoja na pesa taslim ambazo hazijafahamika kiasi chake.
Wezi hao walichimba ukuta wa nyuma wa Benki hiyo na kutoweka na sanduku la uhifadhi wa pesa pamoja na mtambo wa ATM, pesa zikiwa ndani.
Wakati wakitekeleza tukio hilo, washukiwa waliweza kuzima kamera za CCTV na pia kengele ya usalama kabla ya kutekeleza adhma yao ya kuiba mashine na pesa hizo.
Akizungumza na wanahabari, Kamanda wa Polisi wa Jimbo la Nairobi, Japheth Koome amesema kwamba polisi waliweza kupata mitungi ya gesi na vifaa vingine ambavyo hutumuka kukata chuma.
Alipoulizwa kama wezi siku hizi wamepata maarifa na mbinu nyingi kama wacheza filamu, alisema kwamba kwa siku za hivi karibuni matukio ya wizi kwenye mabenki yanazidi kuongezeka na yanakuwa ya aina tofauti na wezi hutumia mbinu tofauti kila kukicha.
Mwaka uliopita, wezi waliojifanya wakaguzi wa hesabu walifika katika benki hiyo na kuingia ndani ambapo walifanikiwa kupora pesa taslim kiasi cha dola za Marekani 300,000.

Comments

Popular posts from this blog