Aveva Amuandikia Barua Rais Magufuli Ya Kuomba Radhi


aveva1
Rais wa timu ya Simba, Evans Aveva.
UONGOZI wa Klabu ya Simba umemuandikia barua Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, John Pombe Magufuli, ukiomba radhi kwa kitendo cha mashabiki wao kufanya uharibifu kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar.
Wakati barua hiyo ikiwasilishwa serikalini, upande wa pili Simba chini ya rais wake, Evans Aveva, imeteua kamati maalum ya wajumbe wenye uwezo mzuri wa kifedha kwa ajili ya kuiwezesha kufanya vizuri msimu huu, kamati ambayo ilianza kazi kuanzia katika mechi dhidi ya Yanga.
nape-3
Sehemu ya viti vilivyog’olewa na mashabiki wa Simba siku ya mechi ya Ligi Kuu Bara dhidi ya Yanga.
Kabla hujaijua kamati hiyo, upande wa kuomba radhi ni kuwa hatua hiyo imefikiwa siku chache tangu serikali kupitia Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo ikiwakilishwa na waziri wake, Nape Nnauye kuzisimamisha Simba na Yanga kuutumia uwanja huo baada ya uharibifu kutokea wakati wa mechi baina ya timu hizo, Jumamosi iliyopita.
magufuli
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, John Pombe Magufuli.
Akizungumza na Championi Ijumaa, Mkuu wa Kitengo cha Habari na Mawasiliano wa Simba, Haji Manara, alisema wamemuomba radhi Magufuli kupitia kwa waziri, Nape kwa kitendo hicho cha uharibifu kilichotokea uwanjani hapo.
Manara alisema uongozi wao unakemea vikali kitendo cha uharibifu wa rasilimali ambazo serikali inatumia gharama kubwa kuziendesha, hivyo kinachotokea siyo sahihi kukikalia kimya na badala yake kuiomba radhi serikali kupitia wizara husika.
“Kwa niaba ya Rais wa Simba, Aveva, benchi la ufundi na sekretarieti kwa jumla tunamuomba radhi rais, Magufuli kufuatia uharibifu uliofanywa na wanaodaiwa ni mashabiki wa Simba.
1-1-9
Waziri wa Habari, Utamaduni, Wasanii na Michezo, Mhe. Nape Nnauye.
“Vilikuwa vitendo vya kipuuzi, kwani huo ni uharibifu wa rasilimali zetu zinazoendelezwa na serikali yetu, kitendo hicho hakitajirudia tena na uongozi wetu upo kwenye uchunguzi na kama ukibaini kuwa uharibifu ulishirikisha baadhi ya wanachama, basi watachukuliwa hatua kali za kinidhamu.
“Uongozi wetu, tayari umepeleka barua ya kuomba radhi kwa Nape ambayo itapelekwa kwa Magufuli tukiomba radhi kwa kilichotokea.
Aveva awakabidhi timu matajiri
“Katika kuhakikisha tunachukua mataji mbalimbali msimu huu, rais wetu Aveva ameteua kamati mpya ya mashindano itakayopambana kuleta makombe.
“Kamati hiyo iliyoanza kazi tayari tangu mechi na Yanga, itaongozwa na mwenyekiti wake Musley Al Rawahi, makamu wa rais wawili ambao ni Mohammed Nassoro na Hassani Hasanoo huku wajumbe wakiwa ni Cosmas Kapinga, Juma Pinto, Bitulo na Manesh.
Waomba kubaki Taifa
“Tumeshapata uwanja baada ya serikali kutuzuia kuutumia Uwanja wa Taifa.
“Pamoja na hivyo tunaiomba serikali ituruhusu kuendelea kuutumia Uwanja wa Taifa, tunaamini serikali watalisikia ombi letu na wataturuhusu kubaki Taifa,” alisema Manara.
Kuleta waamuzi nje ya nchi
Manara alizungumzia suala la waamuzi kwa kusema: “Ili kuepusha matatizo kama haya ya uharibifu yaliyotokea kwenye mechi ya ‘derby’ ya Simba na Yanga, tumewaomba TFF mechi zetu dhidi ya Yanga, tulete waamuzi kutoka nje ya nchi ili kuepukana na hili la akina Saanya (Martin).
“Simba ipo tayari kugharamia fedha yoyote kwa ajili ya kuleta waamuzi, tunajua gharama za kuwaleta ndiyo tatizo, lakini Simba tupo tayari kutumia dola 800 (Sh 1,707,560) ili kuleta waamuzi kutoka nchi za Magharibi na siyo Afrika Mashariki na Kati ambazo nchi hizo wapo baadhi ya waamuzi wenye mapenzi na klabu hizi za Simba na Yanga.”
Jeshi la Polisi
“Jeshi la Polisi linahitaji kuongeza umakini uwanjani na kikubwa wanatakiwa kufanya kazi yao vizuri ya kuangalia usalama na siyo kutazama mpira uwanjani.
“Tunaamini tukio lililotokea kama kungekuwa na umakini katika usalama basi hali isingekuwa kama ilivyokuwa,” alisema Manara.

Comments

Popular posts from this blog