Jinsi Vyakula Vinavyosababisha Magonjwa

Jarida la Emerging Infectious Diseases linasema kwamba zaidi ya magonjwa 200 yanaweza kusababishwa na chakula. Hata hivyo, vijidudu vinavyosababisha magonjwa hayo yote si vingi sana.

Huenda takwimu zifuatazo zinaweza kufanya mtu afikiri hivyo. Kulingana na Shirika la Afya Ulimwenguni (WHO), kila mwaka watu milioni 130 hivi katika Eneo la WHO huko Ulaya wanaambukizwa magonjwa yanayosababishwa na chakula.
Katika mwaka wa 1998, zaidi ya watu 100,000 nchini Uingereza walikuwa wagonjwa kwa sababu ya kula chakula kibaya, na 200 kati yao walikufa. Inakadiriwa kwamba kila mwaka watu milioni 76 hivi wanapata magonjwa yanayosababishwa na chakula huko Marekani, na 325,000 kati yao hulazwa hospitalini, na 5,000 hufa.
Si rahisi kujua hesabu kamili ya ulimwenguni pote. Hata hivyo, shirika la WHO linaripoti kwamba watu milioni 2.2 hivi walikufa kutokana na magonjwa ya kuharisha katika mwaka wa 1998, na milioni 1.8 kati yao walikuwa watoto. Ripoti hiyo inasema: “Wengi kati ya wagonjwa hao waliambukizwa magonjwa yanayosababishwa na chakula au maji machafu.”
Huenda ukashtuka kusikia takwimu hizo kubwa, Lakini je, takwimu hizo zikufanye uwe na wasiwasi mwingi juu ya chakula? Bila shaka la. Ebu fikiria mfano mwingine. Kila mwaka watu milioni 4.2 hivi nchini Australia wanapata magonjwa yanayosababishwa na chakula, yaani watu 11,500 hivi kila siku! Huenda hiyo ikaonekana kuwa idadi kubwa sana. Lakini kwa upande mwingine: Waaustralia hula milo bilioni 20 kila mwaka, kwa hiyo ni milo michache sana inayosababisha magonjwa.
Hata hivyo, hatari ipo. Ni kwa nini chakula kinafanya watu wawe wagonjwa, na tunaweza kufanya nini kupunguza hatari hiyo?
Jarida la Emerging Infectious Diseases linasema kwamba zaidi ya magonjwa 200 yanaweza kusababishwa na chakula. Hata hivyo, vijidudu vinavyosababisha magonjwa hayo yote si vingi sana. Dakt. Iain Swadling, afisa wa shirika la Huduma ya Kimataifa ya Uchunguzi wa Chakula, anasema kwamba asilimia 90 hivi ya magonjwa yote yanayosababishwa na chakula, huenda yanasababishwa na jamii za  vijidudu “zisizozidi 24.” Visababishi vya magonjwa kama vile virusi, bakteria, vimelea, sumu, na kadhalika, huingiaje katika chakula?

Dakt. Swadling anataja mambo matano ambayo kwa kawaida husababisha magonjwa: “Kula chakula kibichi chenye vijidudu; kula chakula kilichotayarishwa na watu wagonjwa au walioambukizwa viini; kutohifadhi vyakula vizuri na kutayarisha chakula saa kadhaa kabla ya kukila; kuchafua chakula safi kwa kukiweka pamoja na chakula chenye vijidudu wakati wa kukitayarisha; kutopika chakula vizuri au kutopasha moto vya kutosha chakula kilichopikwa kimbele.”
Ingawa orodha hiyo inaweza kushtua, inaonyesha jambo zuri pia. Jambo hilo ni kwamba karibu magonjwa yote yanayosababishwa na chakula yanaweza kuzuiwa.
MAMBO YA KUFANYA
1.    SAFISHA. 
Nawa mikono kwa maji ya moto na sabuni kabla ya kuanza kutayarisha kila aina ya chakula. Nawa mikono baada ya kwenda chooni, na baada ya kushughulikia mtoto (iwe ni kumbadilisha nepi au kumpangusa makamasi), au kushika mnyama yeyote, hata mnyama-kipenzi.
Osha vyombo, mbao za kukatia, na meza kwa maji ya moto na sabuni baada ya kutengeneza kila aina ya chakula—hasa baada ya kukata nyama, kuku, au samaki na vyakula vingine vinavyotoka baharini. Gazeti la Test linapendekeza “kuosha matunda na mboga katika maji ya uvuguvugu” ili kuondoa wadudu na mabaki ya dawa ya kuua wadudu. Mara nyingi kutoa maganda na kuchemsha vyakula ni njia bora za kuvisafisha.
Toa na utupe majani ya nje-nje ya kabichi na letusi (lettuce). Katika sehemu zenye maji machafu huenda ikawa muhimu kutia dawa ya kuua vijidudu, kama vile dawa ya kung’arisha, permanganate, au mvinyo wa siki, katika maji ya kuosha matunda au mboga zitakazoliwa zikiwa mbichi.
2.    PIKA VIZURI. 
Karibu bakteria zote, virusi vyote, na vimelea vyote vitakufa ikiwa chakula kitapikwa kufikia nyuzi Selsiasi 70 (moto kabisa), na si lazima kupika kwa muda mrefu. Kuku anahitaji kupikwa hadi aive kabisa kufikia nyuzi Selsiasi 80. Chakula kinachopashwa moto chapasa kufikia nyuzi Selsiasi 75 au kuwa moto na kutoa mvuke. Usile kuku ambaye bado ni mwekundu au mayai yasiyopikwa vizuri. Samaki anapasa kupikwa hadi awe laini na kubadilika rangi.
3. USIWEKE VYAKULA PAMOJA. 
Usiweke kamwe nyama, kuku, au samaki mbichi pamoja na vyakula vingine unapofanya ununuzi, unapohifadhi vyakula hivyo, au unapovitayarisha. Usiache maji ya vyakula hivyo yatone wala kutiririka kwenye vyakula vingine. Usiweke kamwe chakula kilichopikwa kwenye chombo kilichokuwa na nyama, samaki, au kuku mbichi ila chombo hicho kiwe kimeoshwa vizuri kwa maji ya moto na sabuni.
4. HIFADHI VYAKULA IFAAVYO. 
Friji inaweza kuzuia bakteria zisiongezeke, lakini halijoto yake inapasa kuwa nyuzi centigredi 4 tu. Mashine ya barafu inapasa kuwa na nyuzi centigredi 17 chini ya kiwango cha kuganda. Weka vyakula vinavyoweza kuharibika kwenye friji kabla ya muda wa saa mbili kuisha. Ukiweka vyakula mezani mapema, vifunike ili kuzuia inzi.
5. UJIHADHARI UNAPOKULA KWENYE MIKAHAWA. 
Inakadiriwa kwamba katika nchi fulani zilizoendelea, asilimia 60 hadi 80 ya watu waliopata magonjwa yanayosababishwa na chakula walikula vyakula vilivyopikwa mikahawani. Hakikisha kwamba mkahawa unamokula unafuata sheria za usafi zilizowekwa na serikali. Agiza nyama iliyopikwa vizuri. Unaponunua chakula mkahawani na kukileta nyumbani, kile kabla ya muda wa saa mbili kuisha. Endapo muda zaidi ungepita kabla hujala chakula hicho, kipashe moto vizuri kufikia nyuzi centigredi 75.
6. TUPA CHAKULA UNACHOSHUKU KIMEHARIBIKA. 
 Afadhali utupe chakula ambacho unashuku kimeharibika. Si vizuri kutupa chakula kizuri, lakini matibabu ya ugonjwa uliosababishwa na chakula kilichoharibika yatakugharimu fedha nyingi hata zaidi.
Mengi kati ya madokezo hayo yanapatikana katika kichapo Food Safety Tips,kilichochapishwa na Baraza la Tekinolojia ya Chakula Kisichodhuru la Marekani.

source:manyandaheath

Comments

Popular posts from this blog