SAKATA LA ESCROW, IPTL LAIBUKA UPYA BUNGENI


Kambi ya upinzani imeliibua upya bungeni sakata la Escrow, Richmond na umiliki wa kampuni ya IPTL, huku ikihoji sababu za Rais John Magufuli kutoheshimu maazimio ya Bunge ya kumwajibisha Sospeter Muhongo, badala yake kumteua tena kuwa Waziri wa Nishati na Madini.
Hoja hizo ziliibuliwa na Waziri Kivuli wa Nishati na Madini, John Mnyika wakati akiwasilisha maoni ya utekelezaji wa bajeti ya mwaka 2015/16 na makadirio ya matumizi ya wizara hiyo kwa mwaka 2016/17.
Muhongo alikuwa akiiongoza wizara hiyo wakati kashfa ya uchotwaji wa zaidi ya Sh300 bilioni kutoka kwenye Akaunti ya Tegeta Escrow iliyofunguliwa kuhifadhi fedha za malipo umeme kusubiri kumalizika kwa mzozo wa kimkataba baina ya kampuni ya IPTL, inayozalisha umeme na Shirika la Umeme (Tanesco).
Bunge lilimuona Profesa Muhongo kuwa alishindwa kuwajibika na kusababisha Serikali kupoteza mapato.
Profesa Muhongo alilazimika kujiuzulu wadhifa huo saa chache kabla ya Rais wa Serikali ya Awamu ya Nne, Jakaya Kikwete kutangaza baraza jipya.
Hata hivyo, Baraza la Maadili ya Viongozi wa Umma lilimsafisha na kashfa hiyo iliyohusisha malipo yaliyofanywa kwa mawaziri, majaji, wabunge na watumishi waandamizi wa umma.
Jana, Mnyika, ambaye ni mbunge wa Kibamba (Chadema), alirejea maazimio ya Bunge la Kumi akisema lilishafanya maamuzi kuhusiana na mikataba ambayo Serikali inaingia na kampuni mbalimbali, hasa kwenye sekta ya nishati na madini.
“Katika maazimio ya Bunge kuhusiana na fedha, ufisadi uliofanyika katika akaunti ya Tegeta Escrow na umiliki wa IPTL yanayohusu sekta ya nishati na madini, bado hayajatekelezwa kwa ukamilifu wake,” alisema Mnyika.
Akinukuu Azimio Namba 2, Mnyika alisema liliagiza kwamba Serikali iangalie uwezekano wa kununua mitambo ya kufua umeme ya IPTL na kuimilikisha kwa Tanesco kwa lengo la kuokoa fedha inazolipa kwa kampuni hiyo binafsi.
Alisema kambi hiyo inasikitika kuona kwamba mbali ya Serikali kushindwa kununua, bado inaendelea kulipia gharama za uwekezaji na hivyo kuendelea kukiukwa kwa azimio hilo.
Akizungumzia azimio la saba linalohusu kuwajibishwa kwa mawaziri na watendaji wakuu wa wizara na bodi ya Tanesco, Mnyika alisema Profesa Muhongo naye aliwajibishwa kwa uteuzi wake kutenguliwa, lakini Rais Magufuli amemteua tena kuongoza wizara hiyo.
“Rais bila ya kujali nini Bunge lilishaazimia katika kikao ambacho na yeye alikuwa sehemu ya azimio hilo, akamteua Muhongo kuendelea kuiongoza wizara hii. Kambi ya upinzani inaliona jambo hili kama ni dharau sana kwa Bunge na ni fedheha binafsi kwake,” alisema.
Alisema kambi ya upinzani imelazimika kunukuu maazimio hayo kutokana na ukweli kwamba Serikali imeshindwa kabisa kutekeleza maazimio ya Bunge na badala yake mikataba hiyo inaendelea kutekelezwa kama ilivyoingiwa.
“Mfano mzuri ni Tanesco kuendelea kuilipa IPTL fedha za capacity charge mpaka sasa. Jambo hili linazidi kuliondolea shirika hilo la umeme uwezo wa kuwahudumia wateja wake kwa kuwa haliwezi kuwekeza zaidi katika miundombinu ya kusambaza umeme kutokana na kutokuwa na fedha za kutosha,” alisema.

Comments

Popular posts from this blog