Tumekwishaa! Poda Zadaiwa Kusababisha Kansa


PODA
Boniphace Ngumije na Gladness Mallya, RISASI Mchanganyiko
DAR ES SALAAM: Kuna neno moja tu linaloweza kusemwa kwa sasa, kuwa tumekwisha, baada ya kubainika kuwa poda iliyotumika kwa miaka mingi nchini, ambayo ni maarufu kama Johnson’s Baby Powder inadaiwa kusababisha kansa ya kizazi inayoleta maafa ikiwemo vifo.
Taarifa zilizopatikana kupitia mitandao ya internet, zinadai kwamba kampuni inayotengeneza poda hiyo ya Johnson and Johnson ya Marekani, Februari 25, mwaka huu ilihukumiwa kulipa faini ya kiasi cha dola milioni 72 (sawa na shilingi bilioni 144) katika Mahakama ya Missouri kama fidia kwa mwanamke mmoja aliyefariki dunia kwa kansa ya kizazi iliyotokana na matumizi ya vipodozi hivyo.
VIPODOPZIFamilia ya mwanamke huyo, Jacqueline Fox ilitakiwa kulipwa kiasi hicho cha fedha baada ya mahakama kuridhika kuwa ugonjwa na kifo chake kilitokana na matumizi ya vipodozi hivyo kwa zaidi ya miaka 35, akitumia poda pamoja na losheni ya bidhaa hiyo.
Kampuni hiyo ya Johnson & Johnson ilikabiliwa na tuhuma kwamba kwa miongo mingi, kwa lengo la kufanya biashara zaidi, haikuwaonya wateja wake kuwa miongoni mwa viungo vinavyotengeneza bidhaa hiyo, vinasababisha kansa. Zaidi ya kesi 1000 zimefunguliwa huko Missouri na 200 New Jersey, zote zikiilalamikia bidhaa hiyo.
1.Waziri wa afya,Maendeleo ya jamii, Wazee na watoto, Ummy Mwalimu akisoma taarifa yake.Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Mh. Ummy Mwalimu
Fox, aliyeishi Birmingham, Alabama, alisema alitumia Baby Powder na losheni kwa kiwango kikubwa kwa takriban miaka 35, kabla ya kugundulika kuwa na kansa miaka mitatu iliyopita. Alifariki Oktoba mwaka jana akiwa na umri wa miaka 62.
Jere Beasley, ambaye ni wakili wa familia ya Fox, alisema kampuni hiyo ilitambua kuwa inawaongopea wateja wake na mamlaka zinazohusika na vipodozi, wakati akizungumza na waandishi wa habari.
Msemaji wa kampuni hiyo, Carol Goodrich, alionyesha masikitiko yake kwa hatua hiyo, akisema kwa miaka yote, walitambua kuwa ni jukumu lao kuhakikisha afya na usalama wa walaji wa bidhaa zao.
“Tunaumia pamoja na familia ya mlalamikaji, lakini siku zote tuliamini bidhaa zetu ni bora kutokana na ushahidi wa kisayansi.”
Ushahidi wa kisayansi unaoonyesha kiungo kinachosababisha kansa katika vipodozi hivyo siyo jambo la kificho, kwani kimemo kimojawapo kilichopatikana kutoka kwa mshauri wa kitaalamu aliyeajiriwa na kampuni hiyo kilisema ‘mtu yeyote atakayepinga uhusiano wa matumizi ya talc (kiungo hicho) na kansa ya kizazi ni sawasawa na mtu anayepinga hadharani uhusiano kati ya uvutaji sigara na kansa’.
Gazeti hili lilikwenda hadi ofisini kwa Mkemia Mkuu wa serikali ili kutaka kujua kama wana taarifa hizo, lakini ofisa aliyeomba hifadhi ya jina lake kwa vile siyo msemaji, alisema kiutaratibu, kazi hiyo inapaswa kufanywa na Mamlaka ya Chakula na Dawa (TFDA).
Msemaji wa Mamlaka hiyo, Gaudensia Simwanza alikiri kusajiliwa kwa vipodozi hivyo hapa nchini, lakini akasema bado hawana taarifa za kuwepo kwa watu walioathirika kutokana na matumizi ya poda hizo.
“Dawa ambazo zimesajiliwa hapa kwetu zinatokea Afrika Kusini na Ufaransa, hazitoki Marekani. Kabla ya kusajili, huwa tunafanya mawasiliano na mamlaka husika huko inakotoka (FDA) ambao wanatueleza wamepaki kiasi gani na ubora wake.
“Tunaisajili dawa baada ya kupokea banchi ya kwanza, sasa baada ya hapo mwagizaji anaendelea kuileta tu, sasa kwa maelezo yako, itabidi tuingie kazini kuangalia kama bidhaa ina ubora unaotakiwa au la, baada ya hapo tutakuwa na la kusema,” alisema.
Alisema watakusanya upya sampo za bidhaa hizo na kuzipeleka maabara ili zichunguzwe kwa mara nyingine. Endapo zitakutwa na madhara zitapigwa marufuku na pia kuwasiliana na taasisi husika Marekani ili kuwataarifu juu ya hilo pamoja na kuwasiliana na kiwanda kinachozalisha bidhaa hizo.
source:GPL

Comments

Popular posts from this blog