Skip to main content

Mkurugenzi wa Hanang asimamishwa akihusishwa na ubadhirifu wa Mil. 82



Baraza maalumu la Madiwani wa Halmashauri ya wilaya ya Hanang, Mkoani Manyara limewasimamisha kazi watumishi wanne wa Halmashauri hiyo, akiwemo mweka hazina wa Halmashauri hiyo kwa tuhuma za ubadhirifu wa fedha za Halmashauri ya wilaya ya Hanang, Mkoani Manyara.
Aidha katika maamuzi yake Baraza hilo pia limeazimia kwa kauli moja kwamba halina imani na Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri hiyo,Bwana Felix Mabula kutokana na tuhuma za ubadhirifu wa fedha za uchaguzi mkuu wa mwaka 2015 wa shilingi 82,873,000 na hivyo kupendekeza kwenye mamlaka zinazohusika kumsimamisha kazi mkurugenzi huyo kupisha uchunguzi zaidi wa tuhuma zinazomkabili.
Akifunga mkutano wa Baraza hilo maalumu,Mwenyekiti wa Halmashauri hiyo,Bwana George Bajuta amewataja watumishi waliosimamishwakazi kuwa ni pamoja na mweka hazina wa Halmashauri Mazengo Matonya, mhasibu msaidizi Marseli Siima, mhasibu wa matumizi Wellu Sambalu na afisa mipango wa Halmashauri hiyo Hamisi Khatimba.
Hata hivyo Bwana Bajuta ameweka wazi kwamba kwa mujibu wa kanuni,sheria na taratibu za mikutano ya Halmashauri, mkurugenzi mtendaji ndiye katibu wa vikao hivyo na kwa kuwa pamoja na kuwa na taarifa ya mkutano huo hakuweza kuonekana katika ukumbi huo,wajumbe wa mkutano huo walilazimika kumchagua,afisa kilomo wa wilaya,Paul Lukumai kuwa katibu wao.
Akizungumza baada ya kuchaguliwa kukaimu nafasi ya Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya wilaya, afisa kilimo wa wilaya hiyo, Paul Lukumai alitaka kufahamu uteuzi wake ni wa maandishi au wa maneno tu,kwani anachofahamu yeye wajumbe hao wamemchagua yeye kukaimu na siyo kumteua au kama mwanasheria ataeleza vinginevyo.
Hata hivyo mkutano huo maalumu nusura uingie dosari baada ya mkuu wa wilaya ya Hanang,Bwana Thobiasi Mwilapwa kuingia ukumbini na kutaka kumtetea Mkurugenzi mtendaji huyo,huku akiwatishia wajumbe wa mkutano huo kwamba mkutano haukuwa halali.
Ameweka bayana kwamba kutokana na sababu au mazingira yalivyo au nafasi ilivyo haikuwezekana kukutana na viongozi hao na ndipo alipofikia uamuzi wa kwenda kusimama mwenyewe kutoa ujumbe wa serikali akiwa mkuu wa wilaya kwamba mkutano huo siya halali.
Kikao hicho kilichotakiwa kuanza majira ya saa nne asubuhi kililazimika kuanza majira ya saa sita mchana kutoka na wajumbe wa mkutano huo kumsubiri katibu wa kisheria wa mkutano huo ambaye ni Mkurugenzi Mtendaji kwa saa mbili bila mafanikio,zaidi ya kumtumia Mkuu wa wilaya,Thobiasi Mwilapwa ambaye hata hivyo alijikuta akitolewa nje ya ukumbi huo.
Na Jumbe Ismailly, Hanang
DSCN0013
Baadhi ya madiwani wa Halmashauri ya wilaya ya Hanang, Manyara waliohudhuria mkutano wa kumkataa Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya wilaya hiyo kutokana na tuhuma za ubadhirifu wa zaidi ya shilingi milioni 82 za uchaguzi mkuu wa mwaka 2015.
DSCN0038
Mmoja wa watumishi wa Halmashauri ya wilaya ya Hanang, Manyara (aliyesimama) akimnong’ononeza jambo Mwenyekiti wa hiyo,Bwana George Bajuta (wa kwanza kutoka kulia) kuhusu kuchelewa kufika ukumbini kwa kaimu Mkurugenzi mtendaji,Bwana Paul Lukumai.
DSCN0066
Mkuu wa wilaya ya Hanang, Manyara, Bwana Thobiasi Mwilapwa akimsikiliza mwenyekiti wa Halmashauri hiyo alivyokuwa akimbembeleza kaimu mkurugenzi kwenda kukaa kwenye nafasi yake.
DSCN0078
Mkuu wa wilaya ya Hanang, Manyara,Bwana Thobiasi Mwilapwa akitoa ufafanuzi wa kisheria kuhusu mkutano huo kwa waandishi wa habari muda mfupi baada ya kutolewa nje ya ukumbi wa mikutano wa Halmashauri.(Picha  zote na Jumbe Ismailly)
DSCN0003
Muonekano wa jengo la Ofisi za Halmashauri ya wilaya ya Hanang, Manyara.

Comments

Popular posts from this blog