Aliyejipachika cheo cha usalama wa taifa akiona!

IMG-20160212-WA0002
Wakimfunga kamba.
Stori: Makongoro Oging’
na Issa Mnally, UWAZI
DAR ES SALAAM: Ujanja wa mjini! Jamaa aliyejipachika cheo kuwa yeye ni Afisa Usalama wa Taifa, Ofisi ya Waziri Mkuu akijitambulisha kwa jina moja la Manase amekiona cha moto baada ya kunaswa na kufungwa kamba mwilini na mtu aliyesema ni daktari wa Kliniki ya Head 2 ya jijini Dar, Fortdas Fidell.
Tukio hilo la aina yake lilitokea Jumatano ya Februari 10, mwaka huu katika kliniki hiyo inayojishughulisha na tiba ya mifupa na mazoezi iliyopo Mtaa wa Ununio, Kata ya Kunduchi wilayani Kinondoni jijini Dar es Salaam ambapo risasi sita zilipigwa hewani na mtu aitwaye Mashaka Ndonde ili kumdhibiti mtuhumiwa huyo.
UWAZI LAFIKA ENEO LA TUKIO
Baada ya kusikika kwa milio ya risasi, baadhi ya watu walilipigia simu Uwazi na kuhabarisha tukio hilo ambapo waandishi wetu walifika mara moja eneo hilo na kuweza kukutana na Dk. Fidell ambaye alisimulia kisa cha kufyatuliwa kwa risasi na kushikiliwa kwa ‘afisa usalama’ huyo.
IMG-20160212-WA0003Wakimdhibiti.
ISIKIE HII
“Siku hiyo nilikuwa kazini saa nne asubuhi, nikapigiwa simu na mtu aliyejitambulisha kwa jina la Manase akidai kuwa yeye ni Afisa wa Usalama wa Taifa na yupo Ofisi ya Waziri Mkuu, wanataka kuonana na mimi pale kwenye Chuo cha Usalama wa Taifa, Kunduchi kuna mwenzao amepata ajali, ameumia mkono hivyo walihitaji ushauri wangu kama daktari.
“Hata hivyo, nilimtaarifu daktari mwenzangu aitwaye Ndonde lakini alinitahadharisha kuwa makini maana wanaweza kuwa matapeli au watu wabaya.
“Niliondoka na gari langu kuelekea Chuo cha Usalama wa Taifa. Nilipofika eneo la geti la chuo hicho nilikuta magari mawili yenye vioo vyeusi (tinted). Walinisimamisha na kujitambulisha kuwa wao ndiyo walionihitaji.”
WAVAA SUTI
“Walikuwa wamevaa suti nyeusi isipokuwa huyo mmoja tuliyemdhibiti. Wawili walitoka kwenye magari yao na kuingia kwangu. Mmoja alikaa nyuma akiwa na bastola na mwingine, yaani huyu tuliyemkamata alikaa siti ya mbele, walinigeukia huku wakihitaji kwangu shilingi milioni 22.
“Niliwaambia sina, wakataka kadi ya ATM, niliwaambia sina, nikawaambia nina shilingi milioni 2 ofisini, yaani hapa kliniki.
WAONGOZANA KUCHUKUA PESA
“Walitangulia na magari yao mawili huku nikiwafuata. Nilikuwa chini ya ulinzi mkali wa wale wawili niliokuwa nao. Nikapata ujasiri na kutuma ujumbe wa simu kwa Ndonde kuwa nimetekwa, baadaye nilimpigia simu wanitayarishie shilingi milioni 2.
IMG-20160212-WA0004“Tulipokaribia ofisini kwenye kliniki walinitaka nitangulie nikiwa na wenzao wawili, wale wengine wakawa wanafuata. Kati yao sita, wawili walikuwa na bastola. Hawakutaka tuingie ndani, tukasimama getini kwa nje. Nilimpigia simu nesi mmoja alete hizo fedha hizo.
“Kumbe yule nesi kule ndani alishaambiwa na Ndonde kuwa, nimetekwa. Yule aliyekuwa na bastola alishuka kwenye gari langu, wakati huo, Ndonde alichukuwa bunduki na kujificha getini katika ofisi ya mlinzi. Wakati huo walishageuza magari yale mawili na kuangalia tulikotoka.
WENGINE WATIMUA MBIO
“Palepale Ndonde alifyatua risasi tatu hewani kisha akafyatua tena tatu. Nilipata ujasiri wa kuendesha gari kuliingiza ndani ya geti huku tukinyang’anyana usukani na huyu aliyebaki kwenye gari. Wale wengine waliposikia mlio wa risasi walipanda magari yao na kuondoka kwa kasi.
“Nilifanikiwa kuingia naye ndani ya geti huku huyu tuliyemkamata akitaka kutoka lakini nilimdhibiti. Mlinzi naye aliwahi kufunga geti. Baadaye walikuja wenzangu kumdhibiti. Tulimfunga kamba. Tukapiga simu makao makuu ya walinzi wetu Ultimate Security na Polisi Oysterbay ambao walitumia muda mfupi kufika.
“Alikuwepo Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kinondoni, ACP Christopher Fuime na magari mengine yalitoka Kituo cha Polisi Wazo Hill. Walituhoji, wakamchukuwa mtuhumiwa,” alisema Fidell.
KWA MUJIBU WA VYANZO
Wakati Dk. Fidell akisimulia hayo, vyanzo vyetu makini vilidai tofauti. Vilisema kuwa, watu hao ni matapeli waliopata taarifa kuwa, kliniki hiyo inaendeshwa bila kibali na kuwa, baadhi ya wafanyakazi (akiwemo Dk. Fidell) hawana taaluma ya udaktari, hivyo jamaa walikwenda ‘kumtoa’ fedha daktari huyo kwa madai hayo, wakijifanya ni usalama wa taifa.
“Wale jamaa walipata ishu nzima kwamba, ile kliniki ina magumashi mengi. Haiko kihalali. Nasikia hata Naibu Waziri wa Afya (Dk. Hamis Kigwangalla) aliwahi kuionya.
“Sasa nasikia wale jamaa walijifanya usalama wakampigia simu dokta yule, wakamsomea madai na kumwambia kwa usalama wake atoe shilingi milioni 30. Nasikia jamaa akalialia sana mpaka wakafika shilingi milioni 22. Lakini akasema atatanguliza kwanza shilingi milioni 2, nyingine zitafuata.
IMG-20160212-WA0005Afisa huyo akipewa kichapo.
“Lakini sasa kabla hajaamua kuwapa, alimpigia simu Dk. Ndonde, yeye ndiye akasema huenda hao jamaa si usalama wa taifa bali ni matapeli, akamwambia awapeleke pale kliniki kama fedha wakachukulie pale.
“Walipofika yule Ndonde ndiyo akapiga risasi juu baada ya kuwaona wale wa kwenye gari wakihaha kushika kwa nguvu kabla ya kuingia ndani ya geti. Wale wa nje waliposikia risasi wakakimbia na ndiyo polisi wakafika. Hivyo ndivyo ilivyokuwa,” kilisema chanzo.
KATIKA MAHOJIANO MENGINE NA FIDELL
Kuhusu madai ya kliniki yake kuwa na magumashi, Fidell alisema anaiendesha kihalali na anavyo vibali vyote huku akisema madaktari wanaodaiwa kutokuwa na taaluma hawapo.
“Hapa wanakuja watu wazito, hata mawaziri, hivyo hatuwezi kuwa na madaktari wa kubabaisha,” alisema.
WAJUAVYO POLISI
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kinondoni, ACP Fuime alipohojiwa na waandishi wetu wiki iliyopita ofisini kwake alikiri kutokea kwa tukio hilo na kusema wanamshikilia Manase huku msako mkali ukiendelea kuhusu wenzake.
IMG-20160212-WA0014
“Watu hao walimpigia simu Dk. Fidell kuwa wana mgonjwa hivyo awafuate katika geti la Chuo cha Usalama wa Taifa Kunduchi. Alipofika aliwakuta na ndipo walipomgeuka na kutaka awape fedha lakini akawaambia hana hivyo waende awachukulie ofisini ambapo huyo mmoja alinaswa na wengine kukimbia baada ya Dk. Ndonde kufyatua risasi hewani,” alisema kamanda huyo.
Timu ya Uwazi bado inafuatilia habari hii kwa mambo ambayo yanaonekana kuwa yana makengeza.

Comments

Popular posts from this blog