Mfanyabiashara Afia Hotelini na Kete 30 za Heroin


Mfanyabiashara wa dawa za kulevya, Kervin Mafita (40),mkazi wa Kinondoni, Dar es Salaam, amekutwa amekufa kwenye Hoteli  iliyopo jijini Arusha akiwa na shehena ya dawa hizo aina ya heroin tumboni mwake.
 
Meneja wa hoteli hiyo, Bw. Douglas Minja, alisema marehemu alifika hotelini hapo Aprili 12, mwaka huu, akiwa ameongozana na mama yake mzazi, mdogo wake na mtoto wake mwenye umri wa miaka 11 na kukodi vyumba viwili.
 
Alisema Aprili 15, mwaka huu, saa nne asubuhi, mhudumu wa hoteli alienda kugonga chumbani kwa marehemu ili aweze kufanya usafi na baada ya kufunguliwa mlango, ndani kulikuwa na marehemu, mama yake na mgodo wake marehemu.
 
Aliongeza kuwa, ndugu hao walidai muda huo walikuwa na mazungumzo hivyo hawakutaka usumbufu ambapo kutokana na majibu hayo, muhudumu huyo alilazimika kuwapisha ili waendelee na mazungumzo yao.
 
"Baada ya saa moja, ndugu wawili (mama na mdogo wa marehemu), walitoka na kutokomea kusikojulikana ila mtoto wake ambaye muda mwingi nilikuwa naye, aliniomba akamsalimie baba yake chumbani.
 
"Alipofika chumbani, alimkuta baba yake akiwa amelala hivyo alijaribu kumwamsha lakini hakuamka ndipo akamfuata mhudumu na kumweleza kuwa baba yake anamwamsha lakini haamki,"alisema Bw. Minja.
 
Mhudumu alifika katika chumba hicho akiwa ameambatana na Bw. Minja na kumkuta marehemu katika hali mbaya akitokwa mapovu mdomoni wakaamua kutoa taarifa polisi.
 
"Wakati akitolewa hotelini alikuwa hajafariki ila alikuwa kwenye hali mbaya, baada ya kufikishwa Hospitali ya Mount Meru, alifariki wakati akipatiwa matibabu," alisema.
 
Akizungumzia tukio hilo, Kamanda wa Polisi Kikosi cha Kuzuiana Kupambana na Dawa za Kulevya nchini, Godfrey Nzowa,alithibitisha kutokea kwa tukio hilo akisema marehemu alifikia katika hoteli hiyo akitokea Dar es Salaam na alikuwa safarini kwenda nchini China ili kusafirisha dawa hizo. 

Alisema polisi kwa kushirikiana na daktari wa hospitali hiyo, waliufanyia upasuaji mwili wa marehemu Aprili 18, mwaka huu na kukuta dawa hizo tumboni kete 30 za heroin.
 
"Tayari mwili wa marehemu umesafirishwa kwenda Dar es Salaam kwa ajili ya maziko," alisema Kamanda Nzowa.
 
Kamanda wa Polisi mkoani humo, Liberatus Sabas, alikiri kutokea  na kusema polisi wanafanya uchunguzi wa tukio hilo na kuahidi kulitolea ufafanuzi zaidi.

Comments

Popular posts from this blog