MAAJABU MAZISHI YA KOMBA-TINGATINGA LATUMIKA KUMZIKA

Ndugu na jamaa wakisaidiwa na kijiko cha tingatinga kushusha mfuniko wa zege kwenye kaburi la Mbunge wa Mbinga Magharibi, John Komba aliyezikwa katika Kijiji cha LItuhi, wilayani Nyasa, Ruvuma jana. Picha na Emmanuel Herman 
Na Joyce Joliga na Ibrahimu Yamola, Mwananchi
Nyasa. Safari ya mwisho ya mbunge wa Mbinga Magharibi jana ilihitimishwa saa 9.25 alasiri wakati mwili wake ulipofunikwa na mfuniko mkubwa wa zege uliobebwa na gari maarufu kwa jina la “kijiko”.Haikuwa kitu cha kawaida wakati gari hilo kubwa likishusha mfuniko huo wa zege kwenye kaburi la mwimbaji huyo maarufu wa nyimbo za uhamasishaji za CCM na kiongozi wa kundi la Tanzania One Theatre (TOT), lakini majonzi yaliwafanya waombolezaji kulichukulia tukio hilo kuwa la kawaida.Safari ya Komba, iliyoanza miaka 61 iliyopita kwenye kijiji cha Lituhi ambako aliazikwa jana, ilikamilishwa kwa salamu mbalimbali ambazo zilielezea ushupavu wa kapteni huyo mstaafu wa jeshi.
Mazishi hayo yaliyohudhuriwa na mamia ya wananchi, wakiwamo viongozi mbalimbaliwakiongozwa na Rais Jakaya Kikwete na mkewe Salma, yalifanyika katika makaburi ya Misheni,katika Kijiji cha Lituhi (Bundi) wilayani Nyasa mkoani Ruvuma.
Nyuso za majonzi zilitawala kwa waombolezaji waliojitokeza nyumbani kwa marehemu, takriban mita 500 kutoka katika makaburi hayo na baadaye katika misa iliyofanyika kwenye uwanja wa Shule ya Msingi ya Lituhi, ikiongozwa na Askofu John Ndimbo wa Jimbo Katoliki la Mbinga.
Kaimu katibu wa Bunge, John Joel, akisoma wasifu wa marehemu, alisema Kapteni Komba aliyefariki dunia Februari 28, mwaka huu akiwa njiani kupelekwa Hospitali ya TMJ jijini Dar es Salaam, alikuwa anasumbuliwa na maradhi ya shinikizo la damu na mara kadhaa Ofisi ya Bunge ilimpeleka India kwa matibabu. Pia alikuwa na tatizo la kisukari ambalo ndilo lililochukua maisha yake.
Mazishi hayo yalishuhudiwa na viongozi mbalimbali, akiwamo Edward Lowassa, ambaye alikuwa Waziri Mkuu, Waziri wa Kilimo, Chakula na Ushirika, Steven Wasira, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Utaratibu na Bunge), Jenister Mhagama na mbunge wa Songea Mjini, Dk Emmanuel Nchimbi.
Wengine ni Mbunge wa Chalinze, Ridhiwani Kikwete, Naibu Spika wa Baraza la Wawakilishi, Ali Abdallah Ali, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (Kazi Maalumu), Profesa Mark Mwandosya na Spika wa Bunge, Anne Makinda.
Uwanja wa ndege
Kwenye Uwanja wa Ndege wa Songea, viongozi mbalimbali waliwasili kwa ndege za kukodi na Lowassa ndiye aliyefungua mlango kwa ndege iliyotua saa 2:33 asubuhi akiambatana na mbunge wa Korogwe Vijijini, Stephen Ngonyani.
Haikupita muda mrefu, ndege nyingine ilitua saa 2:50 ikiwa na Spika Makinda na msafara wake uliomjumuisha mbunge wa Ludewa, Deo Filikunjombe.
Saa 3:22 ilitua ndege iliyobeba ujumbe wa CCM ukiongozwa na Kinana. Wengine waliokuwamo ni naibu katibu mkuu ambaye pia ni Naibu Waziri wa Fedha, Mwigulu Nchemba, katibu wa itikadi na uenezi, Nape Nnauye na mwimbaji wa kikundi cha TOT, Khadija Kopa. Pia baadaye Rais Kikwete alitua na ndege ya Serikali

Comments

Popular posts from this blog