NGASSA AJUTA KUWATOSA EL MERREIKH, AOMBA MSAMAHA MASHABIKI WA SIMBA, ADAI YANGA WAMEMGEUKA

ngassaMrisho Ngassa

Na Richard Bakana, Dar es salaam

MSHAMBULIAJI wa klabu ya Yanga na Timu ya Taifa ya Tanzania, Taifa Stars, Mrisho Ngassa, amejutia uamuzi wake wa kukataa kujiunga na El Merreikh ya Sudan akisema kuwa yalikuwa ni mapenzi yake makubwa kuichezea Yanga.
Akiongea na Shaffihdauda.com baada ya mchezo wa jana alipoibuka shujaa kwa kuifungia Yanga bao 2-0 dhidi ya Mtibwa Sugar, Ngassa alisema kuwa baada ya kugundua alifanya makosa makubwa kuwagomea Simba na Azam FC ambao ndio walitaka kumpeleka El Merreikh, alipofunga mabao hayo alilazimika kuwaomba msamaha mashabiki kwa uamuzi ambao sasa anaujutia.

“Nilifanya makosa kutokwenda El Merreikh ndio maana hata leo nilipofunga magoli ilibidi niombe msamaha kwa sababu Simba na Azam walitaka kunipeleka El Merreikh, Nilifanya kama kuwakosea na kwasababu nilikuwa naipenda Yanga ilibidi niichezee” Amesema Ngassa kwa hari ya uchungu ajijuta kosa alilofanya katika maisha yake la kukataa kwenda kucheza mpira wa kulipwa nchini Sudan.
Katika msimu wa 2013/2014 Ngassa alijiunga na Yanga akitokea Simba alikokuwa akicheza kwa mkopo akiwa ni mali ya Azam FC, Katika uamisho huo TFF iliamuru awalipe Simba kiasi cha Tsh. Milioni 30 kama pesa ambayo walimsajilia kutoka Azam FC pamoja na Tsh. Milioni 15 kama fidia baada ya kugundulika alikuwa amesajiliwa timu mbili zaidi ya hapo TFF ilikuwa imepanga kumfungia endapo asingelipa deni hilo.
Kufatia Yanga kuonyesha nia ya dhati ya kutaka huduma ya kiungo huyo ambaye amewahi kufanya majaribio kunako klabu ya West Ham ya Uingereza, Uongozi wa Mwenyekiti Manji uliamua kumlipia deni hilo kwa makubaliano kuwa atakuwa akikatwa kiasi cha Tsh Laki tano katika kila mshahara wake wa mwezi na ikawa hivyo kweli.
Ngassa ambaye kwa sasa amebakiza mkataba wa miezi mitano Jangwani, ameuambia mtandao huu kuwa makubaliano hayo yamevunjwa na sasa anamiezi miwili hapokei mshahara kwa kuwa wanaukata wote.
“Hadi sasa hivi nakatwa, Mshahala wenyewe sipewi,Nacheza tu kwasababu namaliza muda wangu lakini namshukuru Mungu yeye ndio anajua la mbele, Walisema watanikata laki tano, wakaja wakaanza kunikata milioni na baada ya hapo wakaanza kukata yote inamaana hadi hapa mshahara wa miezi miwili sijapewa kwahiyo siwezi kuidai timu” Amesema Ngassa ambaye ni Mfungaji bora wa kombe la Shirikisho barani Afrika mwaka jana.
 Akizungumzia namna alivyoifunga Mtibwa Sugar hapo jana, Ngassa anasema kuwa Kocha Hans Van De Pluijm alimuambia asitoke katikatika ya mabeki wawili wa  wapinzani wao ambao walionekana kuwa wazito kukimbia.
“Mwalimu aliniambia kwamba wale mabeki wa kati ni wazito ndio nikazitumia nvyema nafasi, sikuweza kutoka pale katikati” Amesema Ngassa.
Kwa upande wake Kocha Hans Van De Pluijm amesema kuwa udhaifu wa mabeki wa kati wa Mtibwa Sugar aliuona katika kipindi cha kwanza ndio maana aliamua kumuingiza Ngassa mwenye kasi kubwa.
“Kitu muhimu  ni kuwa alitakiwa kutumia fursa alizozipata  kwasababu nilijua kuwa toka kipindi cha kwanza kuwa mabeki wawili wa kati hawakuwa haraka, kwahiyo ninafurahia matokeo tuliyopata” Amesema kocha huyo aliokuwa akiongea na shaffihdauda.com.  

Comments

Popular posts from this blog