CHADEMA YAAHIDI MAKUBWA CHALINZE ENDAPO WATAICHAGUA

 Mwenyekiti wa Baraza la Vijana  (Chadema) Mkoa wa Pwani, Elison Kinyaha amesema ili kudumisha maendeleo, upendo na amani ndani ya Jimbo la Chalinze, upo ulazima wa wakazi wa jimbo hilo kumchagua Mathayo Torongey katika uchaguzi mdogo unaotarajia kufanyika mapema Aprili 6, mwaka huu.
Kinyaha alisema kutokana na uelewa mpana wa wakazi wa jimbo hilo ni wazi kuwa chama hicho ndicho kinachoweza kuibuka na ushindi kwani mtu anayegombea nafasi hiyo ni mpigania haki za wanyonge na anayetambua shida zinazowakabili kwa kipindi kirefu.
Alisema kumpitisha mgombea huyo hawakukurupuka bali walitumia utashi na heshima kubwa iliyomo ndani ya uongozi wa Chadema, hivyo mpaka sasa wanatambua kuwa, kazi wanayoifanya sasa ya kampeni si ya kubahatisha bali ni kushika uongozi wa ubunge ndani ya Jimbo la Chalinze.

 “Sisi leo tuko Kata ya Pera na Kijiji cha Chamakweza, tukiendelea na kampeni ambayo tuliizindua tangu Jumapili. Kikubwa ni kuzungumza na wananchi kwa ustaarabu na kuwajulisha chama wanachopaswa kukichagua ambacho ni Chadema pekee kinachojali shida za wanyonge,” alisema
 
Alisema kuwa katika kipindi kifupi tangu chama hicho kilipozindua kampeni, hali ya mwitikio imekuwa ya kutia matumaini hususan katika mahudhurio ya kampeni kwenye maeneo mbalimbali na kudai hilo linaonyesha ni kukubaliwa kwa sera za chama hicho ambazo zaidi zinajikita kwenye kutetea wanyonge na usawa.
 
Alisema katika zoezi zima la kampeni, chama chao kitafanya kazi hiyo kwa ustaarabu na kuepusha vurugu na ni imani yake wana Chadema wote watajiepusha na hali yoyote inayoweza kutokea kwa upande wa vyama vingine.
 
Wakati huohuo juzi, Mkuu wa Mkoa wa Pwani, Mwantumu Mahiza alisema katika kuhakikisha Uchaguzi wa Jimbo la Chalinze unafanyika kwa amani na utulivu  ni vyema viongozi wa dini zote wakafanya maombi kwa Mungu.
 
Alisema viongozi hao wanayo nafasi kubwa kutokana na imani tangu enzi na kuwataka kuhubiri mema kwa waumini wao ambao wengi ni wafuasi wa vyama vinavyoshiriki uchaguzi huo mdogo.
 
“Ndugu zangu viongozi wa dini, msijisahau katika maombi yenu ombeeni na huu uchaguzi mdogo utakaofanyika mapema mwezi ujao ili haki, amani na hekima itawale kwenye zoezi zima la kazi hiyo muhimu,” alisema.

Comments

Popular posts from this blog