SERIKALI YATANGAZA AJIRA KWA WALIMU WAPYA 36,071

Na Mwandishi Wetu, Dar es Salaam

KATIKA kukabiliana na uhaba wa walimu nchini serikali imetangaza kuajiri walimu wapya 36,071 ambapo watapangiwa vituo vya kazi mwezi ujao.
Hatua hiyo ni mikakati ya serikali katika kukabiliana na uhaba wa walimu ambapo sasa watakuwa na upungufu wa walimu 21684 kutoka 57755 iliyokuwepo kabla ya kutanga ajira hizo mpya.
Naibu waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu TAMISEMI anayeshughulikia Elimu, Kassim Majaliwa, alisema jana kuwa walimu hao watasambazwa katika shule za msingi na sekondari nchini.
Alisema taratibu zote za ajira kwa walimu hao wapya zimekamilika na kwamba mwezi ujao wote walioajiriwa watakuwa wamepangiwa vituo vyao vya kazi.
Majaliwa alisema majina ya walimu wote walioajiriwa na vituo vyao vya kazi tayari kwa kuanza majukumu na serikali itaendelea kuhakikisha uhaba wa walimu nchini unakuwa historia.
Hata hivyo alisema kati ya walimu hao wapya 36021 watakuwa chini ya TAMISEMI na waliobaki watapelekwa kuwa chini ya Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi.
Aliongeza kuwa kati ya walimu hao wa ngazi ya cheti ni 17,928 stashahada 5416 na wale wa ngazi ya shahada ni 12,677.
Alisema mgawanyo wa walimu hao uatazingatia na kutoa kipaumbele kwa maeneo na shule zenye uhaba mkubwa ili kuhakikisha changamoto hiyo inaendelea kutatuliwa.
"Tumepanga walimu kulingana na mahitaji ya shule husika ili kuifanya ikama itoshe. Tumetoa maelekezo kwa maofisa elimu na wakurugenzi nchini kuacha tabia ya kuwajaza walimu wengi katika kituo kimoja. Tutasimamia kikamilifu kuwasambaza walimu hao ili kuhakikisha shule zenye uhaba mkubwa zinapewa kipaumbele," alisema.
Alisema baada ya kukamika kwa taratibu walimu wapya wanatakiwa kuanza kuripoti katika vituo vyao vya kazi kuanzia aprili mosi mwaka huu.
Alisema idadi hiyo inajumuisha walimu wa masomo ya sayansi wa shule za msingi, sekondari, vyuo vya ualimu na walimu wa elimu maalumu.
Kwa mujibu wa vyanzo mbalimbali kutoka Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi kila mwaka zaidi ya walimu 40,000 huitimu nchini kutoka kwenye vyuo mbalimbali.
Mwaka jana serikali ilitoa ajira mpya kwa walimu 26,537 wa shule za msingi, sekondari na vyuo vya ualimu ambapo mwaka juzi walimu 23,907 waliajiriwa.

Comments

Popular posts from this blog