NHIF YAKUSANYA MICHANGO SH237 MILIONI

nhif cc322
Mfuko wa Taifa wa Bima ya afya (NHIF) mkoa wa Iringa umekusanya Sh236.8m ikiwa ni michango ya wanachama kutoka kwa waajiri wao katika kipindi cha mwaka 2013/2014.
Akizungumza na mwandishi wa gazeti hili, Meneja wa NHIF mkoa wa Iringa, Emmanuel Mwikabe amesema kuwa kiasi cha Sh milioni sita hakijakusanywa kutoka kwa waajiri kutokana na kutowasilisha kwa wakati na wengine kuwa na malimbikizo ya michango.
Akichanganua Mwikabe amesema Hospitali teule ya Tosamaganga inadaiwa malimbikizo ya sh490, 298, Halmashauri ya wilaya ya Iringa Sh3.2milioni na Halmashauri ya wilaya ya Mufindi Sh2.4milioni.


Aidha amesema moja ya changamoto waliyoibaini baada ya kufanya ukaguzi ni vituo na hospitali kutokuwa na uwazi wa mapato yatokanayo na bima ya afya na fomu za bima ya afya hasa kwenye vituo vya serikali hazijazwi vizuri.
Changamoto nyingine ni baadhi ya watumishi katika vituo vinavyotoa huduma kujihusisha na vitendo vya kughushi ambapo madai ya Sh6.7 milioni hayakulipwa kutokana na sababu hiyo.
Amezitaja sehemu ambazo hazikulipwa kutokana na kughushi kuwa ni pamoja na Hospitali ya wilaya ya Mufindi Sh 1.8milioni, Zahanati ya polisi ya Iringa Sh1.4milioni, Zahanati ya Magereza ya Iringa Sh1.2 milioni na Kituo cha afya cha Mkwawa Sh 2.2milioni.
Amesema pia katika kipindi cha miezi sita wanachama 50,778 walihudhuria kwenye vituo vya matibabu ambapo gharama zilizowasilishwa kwa ajili ya malipo ni Sh651milioni.
Amesema Sh80.1 milioni zililipwa kwa madhehebu ya dini, Sh124.6 milioni zililipwa kwenye vituo binafsi, na Sh378.4 milioni zililipwa kwenye vituo vya serikali na kuwa Sh68.3 milioni hazikulipwa kutokana na kutofuata taratibu na misingi ya tiba, bei elekezi ya bima ya afya na kutojaza taarifa muhimu katika fomu ya madai. Chanzo: Hakimu Mwafongo

Comments

Popular posts from this blog