HELKOPTA YA CHADEMA YAPOTEA ANGANI


HELIKOPTA ya Chadema maarufu kama Chopa, juzi ilipotea angani na kusababisha viongozi wa chama hicho kushindwa kufanya mkutano katika Kijiji cha Mpwayungu wilayani Chamwino, kama ilivyokuwa imepangwa kwenye ratiba.
Kwa mujibu wa ratiba iliyokuwa imepangwa, viongozi wa kitaifa ambao ni Mwanasheria Mkuu wa chama hicho, Tundu Lissu na Mwenyekiti wa Umoja wa Vijana (BAVICHA), walikuwa wafanye mkutano katika kijiji hicho saa 4 asubuhi.
Akizungumza na MTANZANIA, Mwenyekiti wa Chadema Mkoa wa Dodoma, Steven Massawe alikiri kupotea kwa helikopta hiyo na kukanusha kwamba hakuna njama zozote zilizofanywa na CCM kutokana na kupotea kwa helikopta hiyo.
Kijiji cha Mpwayungu kipo katika Kata ya Mpwayungu, ambayo nafasi ya udiwani ipo wazi na vyama vya Chadema na CCM vyote vimesimamisha wagombea.
“Sababu kubwa ya kupotea kwa helikopta ni tatizo la mawasiliano kama mnavyojua Kijiji cha Mpwayungu hakina mawasiliano. Helikopta ilikuwa ifike katika Kijiji cha Mpwayungu saa nne asubuhi, lakini Kapteni alipotea na kusababisha kukaa angani kwa saa moja na dakika arobaini na akatua Kijiji cha Chipogolo.
“Alipofika Chipogolo akaambiwa sio kijiji hicho chenye mkutano na akatakiwa kurudi nyuma kwa upande wa magharibi kwa kilometa 40, hata hivyo hakufanikiwa ikabidi arudi mjini kujaza mafuta,” alisema Massawe.

Alisema baada ya kujaza mafuta, viongozi hao hawakwenda tena kufanya mkutano Mpwayungu badala yake wakaenda Mpwapwa ambapo kulikuwa na mkutano mwingine saa 7 mchana kwa mujibu wa ratiba.
“Leo (jana) hii viongozi hao kwa kutumia helikopta wamekwenda tena Mpwayungu na kufanikiwa kufanya mkutano majira ya saa nne asubuni na baada ya hapo waliekea Kijiji cha Segala Wilaya ya Chamwino, baadaye wataenda Kiteto na Moshi,” alisema.
Alisema sio kweli kwamba CCM walifanya njama helikopta ya Chadema ipotee ili isifanye mkutano katika kijiji hicho na kwamba Chadema na CCM vyote vilishafanya uzinduzi wa kapteni katika kata hiyo.
“Chadema ilifanya uzinduzi wake wa kampeni katika Kata ya Mwayungu, Januari 26 mwaka huu na CCM walifanya uzinduzi wao Januari 20,” alisema Massawe.
Naye Katibu Mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Dk. Willibrod Slaa, amesema iwapo Serikali ya CCM haitaweka mazingira ya haki kwa makundi mbalimbali ndani ya jamii kwa ajili ya amani ya kudumu, migogoro ya ardhi italitumbukiza taifa katika sintofahamu na hatari kubwa nchini.
Dk. Slaa aliyasema hayo kwenye mikutano ya M4C Pamoja Daima, jana alipokuwa akiwahutubia wananchi wa maeneo ya Iselamagazi, Kishapu, Mhunze, Itilima, Lugulu na Bariadi.
Alisema ni haki kwa wananchi kuwa na matumaini, kwani ndiyo misingi wa amani ya kweli ambayo haihitaji kuhubiriwa jukwaani.

Comments

Popular posts from this blog